July 26, 2021

Uhuru hauna Mipaka

M/kiti, Katibu CCM mikononi mwa Takukuru

Spread the love

BAKARI Khatibu, Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Tawi la Maisaka Kati wilayani Babati na katibu wake Juma Swalehe, wanashikiliwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) mkoani Manyara kwa tuhuma za rushwa. Anaripoti Mwandishi Wetu, Babati … (endelea).

Khatibu na Swalehe, wanashikiliwa kwa tuhuma za kuomba na kupokea rushwa kiasi cha Sh. 200,000, kutoka kwa Mwinjilisti wa Kanisa la Kilutheri ka Komoto mkoani humo.

Taarifa hiyo imetolewa leo Alhamisi tarehe 25 Juni 2020 na Holle Makungu, Mkuu wa TAKUKURU mkoani Manyara.

Makungu amesema watuhumiwa hao walimuomba rushwa hiyo muinjilisti , kwa ahadi ya kumpatia kiwanja walichodai kwamba ni mali ya CCM.

“Wawili hao waliomba na kupokea fedha hizo kutoka kwa mwinjilisti , kwa maelezo kuwa baada ya kupokea fedha hizo wangemuachia kiwanja waliokuwa wakidai ni mali ya CCM,” amesema Makungu.

Makungu amesema uchunguzi zaidi juu ya tukio hilo unaendelea, na kwamba ukimalizika wahusika watachukuliwa hatua za kisheria.

“Uchunguzi zaidi kuhusiana na uhalali wa CCM kumiliki kiwanja hicho na mamlaka ya viongozi hao kuhusiana na mali za chama, unaendelea na mata utakapokamilika hatua zaidi za kisheria zitachukuliwa dhidi yao,” amesema Makungu.

Makungu amewataka viongozi wa CCM, hasa wa ngazi za chini kuachana na vitendo vya rushwa, kwa kuwa wakibainika watachukuliwa hatua za kisheria.

“Rai yetu kwa viongozi wachache wa chama tawala hasa wa ngazi za chini wenye utajiri wa fikra haba, wanaopitapita wakiwaaminisha wananchi kuwa, hawawezi kuguswa na Takukuru kwa kuwa chama kilichowaajiri ndicho kinaongoza serikali, nawakumbusha Katiba inasema, wote ni sawa mbele ya sheria,” amesema Makungu.

error: Content is protected !!