Wednesday , 24 April 2024
Home Habari Mchanganyiko Lulu: Kanumba alijiangusha chumbani
Habari MchanganyikoMichezo

Lulu: Kanumba alijiangusha chumbani

Elizabeth Michael (Lulu) akitokea katika Mahakama Kuu mara baada ya kutoa utetezi wake
Spread the love

MSANII maarufu wa filamu nchini, Elizabeth Michael au Lulu, atawasilisha utetezi mahakamani dhidi yashitaka la kuua bila ya kukusudia kwa kutumia mashahidi watatu, anaandika Faki Sosi.

Ni kauli ya wakili wake Peter Kibatala, mbele ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, baada ya kukamilisha utaratibu wa kisheria wa utetezi kwa mshitakiwa huyo ambaye anadaiwa kuhusika na kosa la kuua bila ya kukusudia.

Lulu ambaye sasa ana umri wa miaka 22, amekutwa na kesi ya kujibu kutokana na shitaka hilo, akidaiwa kumuua Steven Kanumba, tarehe 7 Aprili 2012, nyumbani kwa Kanumba, Sinza, Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam.

Kanumba alikuwa pia ni msanii wa maigizo aliyejipatia umaarufu mkubwa ndani na nje ya nchi kutokana na ustadi wake katika sanaa hiyo. Alibainika kufariki dunia baada ya kufikishwa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNF) baada ya mwili wake kufanyiwa uchunguzi wa kitaalamu.

Baada ya upande wa mashitaka uliomsomea mshitakiwa shitaka lake hilo kwa mara ya kwanza tarehe 11 Aprili 2012, kukamilisha ushahidi wake mahakamani, ukiwakilishwa na wakili wa serikali, Faraja George, Mahakama Kuu inayosikiliza kesi hiyo, ilimkuta na kesi ya kujibu.

Jaji Sam Rumanyika alisoma uamuzi wake leo baada ya Wakili huyo wa Serikali kufunga ushahidi wake dhidi ya Lulu, kwa kutumia mashahidi wanne akiwemo Sethi Bosco, mdogo wa marehemu Kanumba, ambaye alikuwa akiishi naye Sinza.

Shahidi wa mwisho wa upande wa mashitaka, alikuwa Innocent Mosha, daktari wa Muhimbili aliyejitambulisha mahakamani kuwa ndiye alifanyia uchunguzi mwili wa marehemu Kanumba siku mbili baada ya tukio.

Baada ya uamuzi huo wa Lulu kukutwa na kesi ya kujibu, mahakama ilitoa muda kama alivyoomba Wakili Kibatala, kwa ajili ya maelezo ya utetezi. Lulu alitumia fursa hiyo ya kikatiba, kujitetea akiongozwa na wakili Kibatala.

Akijitetea, Lulu aliieleza mahakama kuwa siku ya tukio alikuwa na Kanumba chumbani kwake. Alikana kumsukuma na kuanguka chini kama ilivyodaiwa na upande wa mashitaka wakati wa ushahidi.

Kabla ya hapo, Dk. Mosha akiongozwa na wakili wa serikali, Faraja, alidai kuwa uchunguzi ulibaini kwenye ubongo wa marehemu kuna mgandamizo uliotokana na kugongwa na kitu kutoka nje, kama vile mtu amejigonga sehemu ngumu.

Amedai kuwa ubongo kichwani mwa marehemu Kanumba, ulionekana umevimba na kwamba neva zilionekana kuvilia damu.

Daktari Mosha alieleza kuwa baada ya hapo alipasua moyo wa marehemu Kanumba ambako hakukuta tatizo; baadaye walichukua (akiwa na daktari mwingine waliyeshirikiana kufanya uchunguzi) sampuli ya majimaji ya ubongo na sehemu nyengine ili kupeleka kwa Mkemia Mkuu wa Serikali kwa ajili ya uchunguzi zaidi.

Matokeo ya uchunguzi huo kwa kawaida hayarudi kwa daktari aliyepeleka; bali hukabidhiwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) anayesimamia ushahidi.

Ikaja zamu ya Lulu kujitetea akianza na kukiri kuwa Kanumba alikuwa mpenzi wake. Baada ya Kamumba kuanguka, alifika nyumbani kwake Sinza baada ya kuitwa na Kanumba majira ya saa 5 usiku siku ya tukio.

Alipofika alikwenda moja kwa moja chumbani ambako alimkuta Kanumba ameketi kwenye dressing table, akimaanisha meza ya kuhifadhia nguo na vipodozi.

Akiwa ndani, Lulu alieleza mahakama kuwa alipigiwa simu na kuipokea.

Lulu alieleza kwamba mvutano ulianza baada ya hapo, Kanumba akionesha hasira kwa kitendo cha yeye kupokea simu; Kanumba alikasirika kwa kulalamika Lulu akiongea na rafiki yake wa kiume. Lulu alidai alisikiliza simu nje ya chumba cha Kanumba; ukumbini.

Mvutano huo uliwafikisha hadi yeye kuburuzwa na Kanumba na kuingizwa chumbani ambako Kanumba alifunga mlango. Alidai hapo alianza kupigwa.

Lulu alieleza kuwa alijitahidi kuziba uso ili kunusuru kujeruhiwa usoni. Ghafla alimsikia Kanumba akihema kwa kasi huku akiwa ametupa panga ambalo Lulu alidai Kanumba alilitumia kumpiga nalo kwa kwenye ubapa.

Alidai ghafla akakuta Kanumba ameanguka na kuangukia ukuta uliokuwa karibu na kitanda na kuona anatapatapa.

Lulu alidai kuwa alikimbilia chooni kujificha ili kujinusuru na kipigo akiamini kuwa kingempata iwapo Kanumba angeinuka.

Akiwa chooni, alidai, alisikia kishindo kikubwa akadhani labda ni mlango au mtu alidondoka. “Nilihisi isije ikawa ameanguka (Kanumba) katika kujifanyisha kama amezimia. Nilikuwa namsemesha kuwa umenipiga na kujifanyisha kuwa umezimia,” alieleza mahakamani.

Hatua hiyo ya kishindo kikubwa ndiyo ilimshawishi Lulu kumuita mdogo wa Kanumba, Sethi (shahidi wa kwanza wa upande wa mashitaka). Lulu alidai Sethi alipofika aliamua kumpigia simu daktari ambaye Lulu alidai huwa Kanumba anamtumia kwa matibabu na ushauri.

Lulu alieleza kuwa baada ya Sethi kutoka kumfuata daktari wao aitwaye Dk. Paplas, yeye aliamua kuondoka kwa gari yake kwenda Coco Beach alikodhani ni mahala salama kwa muda ule.

Lulu alieleza mahakamani kuwa baada ya kukamatwa na Polisi asubuhi ya tarehe 7 Aprili, na kuwekwa mahabusu kituo cha Oyserbay, ndipo alipata taarifa kuwa Kanumba amefariki dunia.

Baada ya kutoa utetezi huo, Lulu aliulizwa na Wakili Faraja: Wewe na Kanumba mlikuwa na mahusiano kwa muda gani

Lulu: Miezi minne.

Wakili Faraja: Hekaheka ya ugomvi ilianza muda gani.

Lulu: Wakati nilipomaliza kuzungumza na simu na marafiki zangu.

Wakili Faraja: Umeieleza mahakama ulisema kuwa ulipokimbizwa na Kanumba alikuwa amevaa taulo; taulo hilo halikumvuka au alikuwa anashika.

Jaji: Katika maelezo yake hajatuambia kama alikuwa anakimbia huku akitazama nyuma.

Wakili Faraja: Ulishawahi kupigwa na mama yako mzazi?

Lulu: Ndio.

Wakili Faraja: Mama yako akiwa anakupiga akidondoka ghafla utakimbia.

Lulu: Hapana sitakimbia.

Jaji Rumanyika alimwambia wakili kuwa mazingira ya kupigwa na mama yake hayawezi kufanana na mazingira aliyoyahadithia mtuhumiwa ya kupigwa na panga.

Baada ya hapo, wazee wa baraza walimuuliza Lulu wakianza na kama anajua kuwa anatuhumiwa kwa mauaji bila kukusudia, anaweza kuiambia nini Mahakama.

Lulu: Sijahusika kwa namna yoyote na kifo cha Kanumba na kwamba kutokana na mimi ndiye niliyekuwa nikishambuliwa na nilihitaji kujinusuru sikuweza kumfanya chochote.

Wakili Kibatala aliileza Mahakama kuwa yupo shahidi mwengine ambaye yuko nje ya nchi, ila yapo maelezo ya ushahidi wake aliyoyatoa alipohojiwa Polisi; atayawasilisha akikubaliwa. Alimtaja kuwa anaitwa Josephine Mushumbusi.

Wakili wa Serikali alieleza kuwa Shahidi huyo aitwe kwa wito wa mahakama ili mahakama ijiridhishe kuwa hapatikani.

Kesi itaendelea kesho.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari Mchanganyiko

THRDC yaongeza mkataba wa ushirikiano na ABA

Spread the love  MTANDAO wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC),...

Habari Mchanganyiko

Rufaa ya Equity Benki, State Oil yakwama

Spread the loveMAHAKAMA ya Rufani, jijini Dar es Salaam, imeshindwa kuendelea na...

Habari Mchanganyiko

Bodaboda waeleza mafanikio mafunzo usalama barabarani

Spread the loveMADEREVA bodaboda katika Jiji la Dodoma wameeleza jinsi mafunzo ya...

BiasharaHabari Mchanganyiko

NBC yaahidi kuendelea kuunga mkono Serikali za Mitaa

Spread the loveBenki ya Taifa ya Biashara (NBC) imesisitiza dhamira yake ya...

error: Content is protected !!