Thursday , 25 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Lugola awasha moto NIDA, vigogo watatu mbaroni
Habari za SiasaTangulizi

Lugola awasha moto NIDA, vigogo watatu mbaroni

Kange Lugola, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi. Picha Ndogo IGP, Simon Sirro
Spread the love

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, amemwagiza Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai Nchini kuhakikisha anawatia mbaroni wafanyakazi wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa nchini NIDA pamoja na wamiliki wa kampuni zilizoshiriki kuliingizia taifa hasara. Anaripoti Dany Tibason, Dodoma … (endelea).

Mbali na Kangi kutoa maagizo hayo, wamiliki wa makampuni matatu yanayotuhumiwa kuhusika kufanya ubadhirifu wa fedha za umma katika mradi wa Vitambulisho vya Taifa wamekamatwa jana na kusafirishwa chini ya ulinzi ulinzi mkali wa polisi kupelekwa kwenye Mahakama ya mafisadi iliyopo  jijini Dar es Salaam.

Wamiliki hao walikamatwa jana saa tisa alasiri jijini hapa kufuatia agizo la Waziri  wa Mambo ya Ndani ya Nchi Kangi Lugola baada ya Waziri huo kueleza kuwa watuhumiwa hao ambao ni wamiliki wa kampuni wameshindwa kutoa utetezi juu ya tuhuma zao zinazowakabili.

Makampuni yanayotuhumiwa kwa kuliingizia hasara ni  Gotham International Limited, Gwiholoto Implex Limited na Aste Insurance Broker Company Limited.

Kutokana na hali hiyo, Lugola aliagiza Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai nchini (DCI) kuwakamata watuhumiwa hao jana kabla ya saa kumi na mbili jioni na kuwafikisha katika mahakama hiyo.

Alisema wanaotakiwa kupelekwa katika mahakama ya kifisadi ni watumishi wa NIDA pamoja na aliyekuwa Mkurugenzi wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), Dickson Maimu, kwa tuhuma za kuhusika  kula njama na makampuni hayo na kuihujumu serikali.

Akizungumzia hatua hiyo, Lugola alisema amemuagiza Mkuu wa Upelekezi wa Makosa ya jinai mkoa wa Dodoma (RCO) kuwakamata wamiliki hao kwa niaba ya DCI na kuwasafirisha jana hiyo hiyo kuelekea Dar es Salaam.

Waziri Lugola alisema kuwa mpaka hivi sasa serikali imefanikiwa kurejesha kiasi cha fedha ambacho kilichokuwa kimeibiwa kwa asilimia 84 kwenye mradi huo.

“Mpaka hivi sasa tangu Rais John Magufuli atoe maagizo ya kwenda kufuatilia huu uchafu uliokuwa ufanyika NIDA nimeweza kurejesha fedha kwa asilimia 84 na hiyo nyingine asilimia 16 sina muda wa kupoteza tena kuendelea kumsikiliza mtu hapa,” alisema Lugola.

Aliwataja wamiliki hao waliokamatwa kuwa ni Exavery Kayombo (Gwiholoto), Jack Ghotham na Kyaruzi (Ghotham) na Astery Mwita (Aste Insurance).

Lugola alisema kampuni ya Gotham inadaiwa Sh. 2.8 bilioni ambayo ilijipatia fedha hiyo isivyo halali kwa kuongeza gharama mbalimbali ikiwamo tozo ya ongezeko la thamani (VAT) kwa asilimia 20 badala ya 18.

Kwa upande wa kampuni ya Gwiholoto alidai kuwa Sh. 900.8 milioni ambayo ilipewa kwa ajili ya utoaji mizigo bandarini huku kampuni ya bima ya Aste ilichota zaidi ya Sh. 1 bilioni kwa kugushi bima za magari 24 ya Nida na bima ya majengo.

“Kwa upande wa kampuni ya Dk. Shija Paul Rimoy ambaye anadaiwa Sh. 27 milioni ameandika barua asubiriwe hadi atakaporudi nchini kwa kuwa yupo safarini nchini Ujerumani,” alisema.

Kadhalika, Lugola alitaja makampuni ambayo yamerejesha kiasi cha fedha zilizokuwa zinadaiwa kuwa ni IRIS Corporation dola za kimarekani 14 milioni ambazo zimekatwa kwenye deni ambalo kampuni hiyo ilikuwa inaidai serikali Dola za kimarekani 29 milioni.

“Kwa hiyo hii kampuni ya IRIS tumemalizana nayo na bado wanaidai serikali Dola za kimarekani 15 milioni, pia kampuni ya Copy Cat Tanzania Ltd iliyokuwa inadaiwa Sh. 569.2 milioni imezirejesha na kampuni nyingine ni ya Sykes Travel Agent Ltd imerejesha Sh. 5.9 milioni,” alisema.

Akizungumzia kuhusu aliyekuwa Mkurugenzi wa Nida, Lugola alisema uchunguzi unaonesha kuwa watumishi wa mamlaka hiyo walishirikiana na makampuni zilizopewa zabuni mbalimbali kufanya ubadhirifu huo.

Hata hivyo Lugola alisema kuwa uongozi wa NIDA wa sasa hausiki kabisa katika unadhilifu wa pesa zilizotumiwa na wafanyakazi kwa kushirikiana na makampuni mbalimbali za kifisadi.

“Kutokana na wizi huu kufanyika kwa kushirikiana na makampuni hayo namwagiza DCI kuwakamata watumishi wote walioshiriki pamoja na aliyekuwa Mkurugenzi mkuu wa Nida Dickson Maimu kuwakamata kabla ya saa 12 jioni leo (jana),” alisema Lugola.

Alisisitiza kuwa serikali ya awamu ya tano sio ya kutengeneza njama ya kupiga fedha za umma huku akidai kuwa hao wote waliokamatwa watafikishwa kwenye Mahakama ya Mafisadi.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

Prof. Muhongo akomalia matumizi nishati jadidifu kuondoa uhaba wa umeme

Spread the love  MBUNGE wa Musoma Vijijini (CCM), Profesa Sospeter Muhongo, ameendelea...

Habari za Siasa

Kilosa yawa mfano wa kuigwa miradi ya Mwenge nchini

Spread the love  KIONGOZI wa Mbio za Mwenge Kitaifa Godfrey Mzava amezitaka...

Habari za SiasaTangulizi

Biteko ataja vipaumbele 7 bajeti nishati 2024/25

Spread the love  NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Mwekezaji amwaga bil. 39 kujenga viwanda 3 vya uchenjuaji

Spread the loveKampuni ya Mineral Access System Limited (MAST) inayoiwakilishwa kampuni ya...

error: Content is protected !!