Tuesday , 16 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Lissu Vs Ndugai; Mambo hadharani leo
Habari za Siasa

Lissu Vs Ndugai; Mambo hadharani leo

Alute Mungwai
Spread the love

HATIMA ya mvutano kati ya mawakili wa Jamhuri na utetezi upande wa Tundu Lissu, aliyekuwa Mbunge wa Singida Mashariki unatarajiwa kutatuliwa leo tarehe 26 Agosti 2019. Anaripoti Faki Sosi … (endelea).

Mahakama Kuu Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, inatarajiwa kufikia uamuzi kama maombi ya Lissu yanaweza kusikilizwa na mahakama hiyo, pia mfungua maombi (kwa niaba ya Lissu) kama ana haki hiyo.

Jaji Sirilius Matupa wa mahakama hiyo, ndiye anayetarajiwa kutoa uamuzi huo yaliyowasilishwa na mfungua maombo wa Lissu. Mawakili wa Jamhuri waliwasilisha sababu nane kupinga maombi hayo kwa madai ya kutokidhi vigezo vitano kati ya sita.

Upande wa utete ukiongozwa na Peter Kibatala, ulipinga hoja za Jamhuri kwa maelezo kwamba hazina uzito wowote na kutaka mahakama izitupilie mbali.

Kwenye mvutano huo uliochukua zaidi ya saa 11 saa zilizoandamana na vipindi viwili vya mapumziko, Kibatala aliieleza mahakama kuwa madai ya kutoambatanisha uamuzi wa Spika uliomvua ubunge Lissu, sio jambo la msingi na la kisheria.

Kwenye shauri hilo linalovutua watu wengi, Lissu kupitia mawakili wake, anaomba kibali cha Mahakama Kuu ili afungue kesi ya kutaka uamuzi wa kuvuliwa ubunge, utenguliwe na arejeshwe kutumikia wananchi.

Katika shauri hilo, Lissu anawashitaki Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Spika Ndugai ndiye alitoa tangazo rasmi la uamuzi wa kumvua Lissu ubunge mnamo tarehe 28 Juni 2019.

Kwa mujibu wa Kibatala, Kanuni ya 5 ya Mwenendo wa Mashauri ya Mapitio ya Maamuzi ya Mamlaka za Kiserikali, hakuna mahali ambapo panataja kuwa lazima kuambatanisha uamuzi.

Pia kwenye utetezi huo, Wakili Kibatala ameieleza mahakama hiyo kwamba Spika Ndugai hakutoa tangazo, na kuwa alitoa taarifa kwa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi kuwa kiti cha ubunge wa Singida Mashariki kiko wazi.

Clement Mashamba, akiwaongoza Mawakili wa Serikali walidai mpeleka maombi (upande wa Lissu), hawakukidhi vigezo.

Abubakar Mrisha, Wakili wa Serikali Mwandamizi ameieleza mahakama, maombi yaliyowasilishwa mahakamani hayakidhi vigezo kwa sababu maombi au mashauri yanapofikishwa mahakamani, lazima yawe yamezingatia vigezo sita.

Akitaja vigezo hivyo amesema, Kwanza; maombi hayo yaliletwa ndani ya miezi sita baada ya jambo husika kutolewa uamuzi.

Pili; mwombaji awe anaelewa vizuri shauri, tatau; maamuzi yawepo kisheria, nne; iwe hakuna namna nyingine ya kufanya kuhusu huo uamuzi.

Tano; kama mahakama itasikiliza na kuona kuna haja ya kutoa uamuzi na mwisho maombi yanatakiwa yawe katika nia njema na wala si kwa kupotosha au kuwa na lengo la kujinufaisha binafsi.

Pia mahakamani hapo, wakili wa serikali wamedai kuwa mpeleka hoja (Alute Mughwai), hana sifa ya kufungua maombi hayo wa niaba ya Lissu.

Wakili Kibatala akijibu hoja hizo alianza na hoja ya kuambatanisha maombi sambamba na uamuzi wa Mahakama akieleza kuwa kifungu cha 5(2) cha Sheria ya Viapo, hakishurutishi kuwekwa nakala za uamuzi wa mahakama mbalimbali.

“Sio kwa bahati mbaya mleta maombi na kwamba si mara zote muombaji atalazimishwa kuleta maombi; ingekuwa ni sharti la lazima sheria ingeweka wazi bila ya kumung’unya maneno,” wakili Kibatala ameieleza mahakama.

Wakili Kibatala ameitaja kesi Na. 9 ya mwaka 2018 ya Bernad Msoza dhidi ya mwanasheria mkuu wa serikali iliyokuwa Mahakama Kuu Kanda ya Shinyanga.

Hoja nyengine amedai, kwenye Sheria ya Uchaguzi, kifungu 37(3) ambamo imeelezwa mazingira ya mbunge akijiuzulu au akipoteza maisha au sababu nyingine, spika atatangaza pia kumuandikia barua Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi kutokana na uamuzi huo.

Akijibu hoja ya nyaraka ya mamlaka ya kisheria, ameeleza kuwa kiapo na nyaraka hizo hazina tatizo kisheria kwa kuwa muapaji ambaye ni Lissu, ameapishwa na Wakili Magai ambaye ameidhinishwa kuwa ni Kamshina wa viapo nchini.

Wakili Kibatala alieleza kuwa kisheria, kwa sasa Miraji Mtaturu si mbunge bali “mbunge mteule” asiyeweza kushiriki shughuli yoyote ya kibunge mpaka atakapoapishwa.

Kuhusu hoja ya walalamikiwa kuwa Lissu arudi bungeni kukata rufaa, wakili Kibatala aliita ni “hoja mfu” kwa kuwa “Lissu hawezi kurudi bungeni kutokana na yeye kuwa si mbunge sasa.”

Kwenye maombi hayo, pamoja na mambo mengine Lissu anaomba zuio la muda la kuapishwa kwa Mbunge Mteule, Jimbo la Singida Mashariki, Miraji Mtaturu na maombi ya kupinga kuvuliwa ubunge.

Amefungua shauri hilo chini ya hati ya dharura, kupitia kwa kaka yake Wakili Alute Mughwai, ambaye amempa mamlaka ya kisheria kufanya hivyo.

Related Articles

Habari za Siasa

CAG abaini madudu katika vyama 10 vya upinzani

Spread the loveUKAGUZI wa Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali...

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

‘Mwanapekee’ wa Rais Samia: Atabadili nini Arusha?

Spread the loveMAPEMA wiki hii, baadhi ya viongozi walioapishwa na Rais Samia...

Habari za Siasa

Hivi kweli Ole Sendeka alishambuliwa kwa risasi?

Spread the loveMIMI siamini kwamba yupo mtu mwenye nia ya kuua ambaye...

Habari za SiasaTangulizi

Makonda kung’oka tena

Spread the loveUWEZEKANO wa Paul Makonda, kuendelea na wadhifa wake wa mkuu...

error: Content is protected !!