TUNDU Lissu, mgombea urais wa Tanzania kupitia Chadema amesema, wamefanya utafiti wa kuangalia mwitikio wa wananchi kwenye mikutano yao, upigaji kura na kubaini katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Jumatano tarehe 28 Oktoba 2020 watashinda urais kwa asilimia 65 hadi 75. Anaripoti Mwandishi Wetu, Lindi…(endelea)
Lissu amesema hayo leo asubuhi Jumamosi tarehe 24 Oktoba 2020 alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kabla ya kuendelea na ratiba yake ya mikutano ya kampeni majimbo ya Tunduru, Nyasa na Songea Mkoa wa Ruvuma.
Amesema, tangu kuanza kwa kampeni za uchaguzi huo tarehe 26 Agosti 2020, tumefanya mikutano mingi ya kampeni kuliko mshindani wangu mkuu Rais John Magufuli (wa CCM), kuliko hata mgombea wake mwenza (Samia Suluhu Hassan) au waziri mkuu (Kassim Majaliwa).”
“Hakuna mkutano ambao imebidi tusafirishe mtu yoyote, ni waliokuja kwa kutembea wao wenyewe, usafiri wanaoujua wao, yaani kwa kujitegemea. Mikutamno yao ya Rais Magufuli, mgombea mwenza au waziri mkuu wanabeba watu ili kujaza,” amesema Lissu
Amesema, wamewatumia wataalamu kufanya utafiti maeneo mbalimbali nchini juu ya upigaji kura na, “wataalamu wetu wa mahesabu wanaofuatilia na kufanya utafiti, jinsi ya tulivyofanya mukutano, mwelekeo wa uchaguzi ni kwamba tunashinda uchaguzi huu kati ya asilimia 65 hadi 75.”
Lissu ametumia fursa hiyo kuwaomba, wananchi katika siku hizi tatu zilizosalia kuwa makini hususan mawakala ili kutofanyiwa mchezo mchafu wa kisiasa utakaowawezesha washindani wao kutumia mwanya huo.
Mgombea huyo wa Urais amesema, wamepokea hivi karibuni daftari wa wapiga kura na wanaendelea kulichambua ili kubaini wapiga kura na vituo kama vipo hewa na siku chache zijazo, watazungumza na waandishi wa habari juu ya kile watakachokuwa wamekibaini.
“Wataalamu wetu wanaendelea kulifanyia kazi kwa kulichambua na taarifa itatoka kabla ya Jumatatu. Wameandika majina ya watoto na tumeona wanafunzi wanafundishwa kupiga kura wakiwa darasani na mgombea mmoja wa ubunge wa CCM.”
“Watu wetu ndani ya CCM, tume na huko mitaani wanatupa taarifa za kutosha juu ya baadhi ya hujumu zinazoweza kufanywa,” amesema
Lissu amesema “mara nyingi nimesema na ninarudia tena, wakitaka kuharibu uchaguzi, wanataka kupelekwa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC), kuna uchunguzi umekwisha kuanza kwa yaliyofanyika na yatakayofanyika, hivyo niwaonye, wanaotaka kuuharibu uchaguzi huu, wasifanye hivyo.”
Amesema, tayari kuna orodha ya watu imekwisha kuanza kuwafuatilia “yeyote atakayetumia mbinu za kiharimia kuharibu uchaguzi, anajiingiza mwenyewe kwenye orodha ya ICC, kama wanafikiri watavuruga uchaguzi, yakatokea maafa halafu wakabaki salama, wanajisahau.”
Lissu ametoa wito kwa “wakuu wa vikosi, wakuu wa majeshi yetu, nawaombeni, nawasihi, kumbukeni viapo vyetu kwamba ninyi ni wanajeshi wa wananchi, msitumie silaha zenu dhidi ya sisi wananchi.”
Leave a comment