April 11, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Lissu kumuaga Mkapa

Tundu Lissu, Makamu Mwenyekiti wa Chadema

Spread the love

MWANASIASA mashuhuri wa upinzani nchini Tanzania, Tundu Lissu, anatarajiwa kushiriki mazishi ya Rais mstaafu Benjamin Mkapa. Anaripoti Yusuf Katimba, Dar es Salaam … (endelea).

Lissu ambaye amekuwa akiishi uhamishoni nchini Ubelgiji kwa takribani miaka miwili sasa, kufuatia kushambuliwa kwa risasi anatarajiwa kukanyaga ardhi ya Tanzania, Jumatatu wiki hii.

Makamu Mwenyekiti huyo wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), anatarajiwa kupokelewa katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JN), saa saba na dakika 20, ikiwa ni miaka mitatu tangu kushambuliwa kwake na kuondoka nchini.

Taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika imesema, Lissu baada ya kutua kesho muda huo, taratibu za kichama zitaendelea ikiwa ni pamoja na kupumzika.

         Soma zaidi:-

Amesema, “…Jumanne ya tarehe 28 Julai 2020, Lissu atakwenda kutoa heshima za mwisho kwenye mwili wa rais mstaafu Benjamin Mkapa anayeagwa katika viwanja vya Uhuru kwa siku tatu kuanzia leo tarehe 26 Julai 2020.”

Mkapa alifariki dunia Alhamisi iliyopita – tarehe 23 Julai 2020 – katika hospitali moja jijini Dar es Salaam. Alifikwa na mauti, kutokana na mshituko wa moyo.

Mwili wa Mkapa umepangwa kuzikwa Jumatano tarehe 29 Julai 2020, kijijini kwake, Lupaso, wilayani Masasi, mkoani Mtwara.

Taarifa aliyoweka kwenye ukurasa wake wa twitter leo Jumapili, Mnyika amesema, “Ratiba ya Tundu Lissu ni ile ile 27 Julai 2020, saa 7:20 mchana. Tutampokea Airport (uwanja wa ndege) wa Dar es Salaam. Huu ni uhuru wetu na haki yetu.”

Amesema, “tarehe 28 Julai 2020, atakwenda kumuaga Mzee Mkapa. Mwenyezi Mungu atujalie tuwe na upendo, utu, haki, hekima, umoja na Amani.”

Kauli ya Mnyika, imekuja siku moja, tangu jeshi la polisi nchini Tanzania, litangaze kuzuiwa upokeaji wa mwanasiasa huyo.

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, iliyosainiwa na Msemaji wake, David Misime,  jeshi hilo limesema, limelazimika kuzuia mikusanyiko ya aina yoyote katika kipindi hiki cha maombolezo ya kifo cha Mkapa.

Jeshi hilo limekana taarifa kuwa limejulishwa ujio wa Lissu, badala yake, limedai kuwa taarifa za ujio wa kiongozi huyo, imezipata kupitia mitandao ya kijamii.

Amesema, “jeshi la polisi hatuna taarifa kuhusu kurudi kwa Lissu. Jeshi la Polisi limefuatilia nchi mzima kuona kama kuna taarifa (notice), iliyofikishwa kituo chochote cha Polisi kwa ajili ya kusanyiko linaloitishwa katika muda uliotolewa kisheria, lakini hakuna.”

Hata hivyo, MwanaHALISI Online limeelezwa kuwa wakili wa Lissu anayefahamika kwa jina la Robert Amsterdam, anayefanyia kazi zake nchini Uingereza na Marekani, ameliandikia barua jeshi hilo, tokea tarehe 23 Julai mwaka huu, kulijulisha kuwasili kwa mteja wake.

Katika barua yake ambayo wakili huyo amewaandikia watu mbalimbali, akiwamo Simon Sirro, mkuu wa jeshi la polisi nchini Tanzania (IGP), Amsterdam anasema, “Lissu anatarejea Tanzania, Jumatatu ana anataka kushiriki uchaguzi mkuu wa Oktoba.”

error: Content is protected !!