January 16, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Lissu kutua Tanzania leo, maandalizi yakamilika

Spread the love

TUNDU Antiphas Lissu, Makamu Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Upinzani nchini Tanzania cha Chadema- Bara ameanza safari ya kutoka Ubelgiji kurejea nchini mwake Tanzania. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam…(endelea).

Lissu alianza safari jana jioni Jumapili kutoka nchini humo na atatua Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam leo Jumatatu tarehe 27 Julai 2020 saa 7:20 mchana kwa ndege ya Shirika la Ndege la Ethiopia.

Picha mbalimbali za video, zinamwonyesha Lissu pamoja na mkewe na dereva wakiingia uwanja wa ndege nchini Ubelgiji ili kurejea Tanzania baada ya siku 1054 kuwa nje ya nchi yake aliyozaliwa.

Mwanasiasa huyo, amekuwa ughaibuni tangu tarehe 7 Septemba, 2017 aliposhambuliwa kwa risasi zaidi ya 30 na watu wasiojulikana akiwa nje ya makazi yake Area D jijini Dodoma.

Alifikwa na mkasa huo mchana wakati akitoka kuhudhuria mkutano wa Bunge uliokuwa ukiendelea.

Baada ya kushambuliwa, Lissu alipelekwa Hospitali ya Rufaa ya Dodoma kwa matibabu ya awali na usiku huo huo alihamishiwa Hospitali ya Nairobi nchini Kenya.

Lissu alipata matibabu hospitalini hapo hadi tarehe 6 Januari 2018 alipohamishiwa nchini Ubelgiji kwa matibabu na tayari amekwisha kueleza yeye mwenyewe amepona.

Soma zaidi…

Tayari baadhi ya viongozi wa Chadema wameanza maandalizi ya kwenda kumpokea uwanjani hapo.

Mara baada ya kupokelewa, Lissu atakwenda moja kwa moja makao makuu ya Chadema Kinondoni jijini Dar es Salaam ambako maandalizi yamekwisha kamilika ikiwamo ya wageni watakaofika hapo na mazungumzo na waandishi wa habari.

Mchungaji Peter Msigwa, akizungumza na MwanaHALISI Online, Mwenyekiti wa maandalizi ya mapokezi ya Lissu amesema, kazi ya kamati hiyo imemaliza na kwamba wanajiandaa kwenda kumpokea.

Kuhusu zuio la polisi kuhusu mikusanyiko isiyo halali, Mchungaji Msigwa amesema wao hawaendi kukusanyika bali wanakwenda kumpokea kiongozi wao.

Mchungaji Msigwa amesema, kila Mtanzania ana haki ya kumpokea ndugu ama jamaa anayetoka nje ya nchi.

“Lissu ni kiongozi wa Chadema lakini pia ana ndugu, watoto na marafiki ambao wana haki ya kwenda kumpokea. Alikuwepo nje ya nchi kwa muda mrefu hivyo tunaenda kumpokea. Na sasa yuko njiani anarudi,” amesema Mchungaji Msigwa.

error: Content is protected !!