July 29, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Lissu kufunga kazi Dar, Magufuli Dodoma

Tundu Lissu

Spread the love

TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) nchini Tanzania, imetoa ratiba ya mwisho ya lala salama ya kampeni za wagombea urais katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Jumatano tarehe 28 Oktoba 2020. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Ratiba hiyo toleo la sita, imeanza kutumika leo Jumamosi tarehe 17 hadi 27 Oktoba 2020 ikionyesha, wagombea 15 wa urais na makamu wa urais wanavyochuana kujinadi kwa wananchi.

Kati ya wagombea 15 wa urais, mchuano uko kwa wagombea wawili ambao ni Rais John Pombe Magufuli wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Tundu Lissu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Rais Magufuli, anayetetea nafasi hiyo kwa muhula wa mwisho kwa mujibu wa Katiba, alianza kampeni zake jijini Dodoma na atahitimisha kampeni zake jijini humo tarehe 27 Oktoba 2020.

Kwa upande wake, Lissu aliyeanza kampeni zake jijini Dar es Salaam, ratiba hiyo inaonyesha atafunga kampeni zake jijini humo tarehe 27 Oktoba 2020.

Rais Magufuli, ambaye amekuwa na mapumziko ya siku nne tangu tarehe 14 Oktoba 2020, alipofunga kampeni zake jijini Dar es Salaam katika Uwanja wa Tanganyika Packers, ataendelea na kampeni tarehe 19 Oktoba 2020 Bagamoyo mkoani Pwani na jijini Tanga katika majimbo ya Handeni na Korogwe.

Ratiba hiyo, inaonyesha Rais Magufuli akitoka Tanga atakwenmda Kilimanjaro, Arusha, Manyara na kurejea Dodoma kuhitimisha kampeni zake.

Miongoni mwa maeneo ambayo Rais Magufuli hatokwenda kufanya kampeni ni mikoa ya Kusini ya Lindi, Mtwara na Ruvuma ambako huko alikwenda mgombea wake mwenza, Samia Suluhu Hassan.

Mshindani wake wa karibu Lissu, leo Jumamosi yuko Singida na Dodoma kisha atakwenda baadhi ya majimbo yaliyopo mikoa ya Manyara, Arusha, Kilimanjario, Tanga, Kusini Pemba, Mjini Magharibi, Lindi, Mtwara na Ruvuma.

Kisha atarudi kwenye majimbo ambayo hakuwa ameyafikia ya mikoa ya Singida, Dodoma, Kilimanjaro, Tanga na atahitimisha jijini Dar es Salaam.

Lissu ambaye kuanzia tarehe 3 hadi 9 Oktoba 2020, alifungiwa kutokufanya kampeni kwa siku saba kutokana na kulalamikiwa na vyama vya CCM na NRA kuwa alitoa lugha za uchochezi zisizothibitika, ilimfanya kukosa mikutano kadhaa.

Mikutano aliyoikosa ni baadhi ya majimbo yaliyopo mikoa ya Mbeya ikiwemo Mbeya Mjini, Pwani, Iringa na Njombe ambako huko alikwenda mgombea wake mwenza, Salum Mwalimu.

error: Content is protected !!