May 8, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Lissu atua Ubelgiji, aahidi makubwa

Tundu Lissu, aliyekuwa Mgombea Urais wa Tanzania kwa tiketi ya Chadema akiwasili nchini Ubelgiji

Spread the love

KIONGOZI wa upinzani nchini Tanzania, Tundu Antipas Lissu, amewasili salama jijini Brussel, nchini Ubelgiji leo asubuhi ya Jumatano tarehe 11 Novemba 202. Anaripoti Saed Kubenea, Dar es Salaam … (endelea).

Lissu aliwasili katika uwanja wa ndege wa Zaventen Brussel, majira ya saa 3 na dakika 26 asubuhi na kupokelewa na baadhi ya Watanzania waishio nchini humo na marafiki zake wengine.

Makamu Mwenyekiti huyo wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), aliondoka Tanzania jana Jumatatu kwenda Ubelgiji kwa ndege ya shirika la ndege la Ethiopia, kwa maelezo kuwa anahofia usalama wa maisha yake endapo ataendelea kuishi Tanzania.

Alikuwa mmoja wa wagombea urais katika uchaguzi mkuu wa tarehe 28 Oktoba 2020, ambako alitangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya Tanzania (NEC) kuwa mshindi wa pili, nyuma ya Rais John Pombe Magufuli wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Tokea kumalizika kwa uchaguzi huo, Lissu aliyedai kuwa uchaguzi mkuu uliyopita uligubikwa na udanganyifu na wizi wa kura, amekuwa akidai kupokea vitisho dhidi ya maisha yake.

Tundu Lissu akipokewa na mke wake

Mwanasiasa huyo aliyewahi kushambuliwa kwa risasi na wanaoitwa, “watu wasiojulikana,” akiwa nje ya nyumba yake, Area D, mjini Dodoma, amesisitiza kuondoka kwake nchini, hakumaanishi anakwenda kuomba ukimbizi.

Lissu alishambuliwa kwa risasi, wakati akitokea bungeni tarehe 7 Septemba 2017, ambako alishiriki mkutano wa Bunge la asubuhi.

“Nimeondoka Tanzania kuja hapa Ubelgiji, ili kuokoa maisha yangu yaliyokuwa hatarini,” ameeleza Lissu, muda mfupi baada ya kutoka nje ya uwanja wa ndege wa Zaventen, Brussel.

Aliongeza, “sijakimbia mapambano. Sijawakimbia wananchi wangu walionipigia kura na wanaoniunga mkono. Bali, nimekuja kuanzia uwanja mpya wa mapambano.”

Akiongea kwa kujiamini, Lissu ambaye aliwahi kuwa Rais wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS), ameeleza anatarajia kurejea Tanzania mara baada ya kujihakikishia kuwa usalama wake hauko mashakani.

error: Content is protected !!