Wednesday , 24 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Lissu aondoka Tanzania, aacha ujumbe
Habari za SiasaTangulizi

Lissu aondoka Tanzania, aacha ujumbe

Spread the love
TUNDU Antipas Lissu, aliyekuwa mgombea urais wa Tanzania, katika uchaguzi mkuu uliyopita, kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), ameondoka nchini kwenda Ubeljiji. Anaripoti Hamis Mguta, Dar es Salaam … (endelea).

Lissu ameondoa nchini leo, Jumanne saa 11 jioni, tarehe 10 Novemba 2020, kwa ndege ya Shirika la ndege la Ethiopia, kuelekea Ubelgiji ambako alikuwa akiishia kwa takribani miaka miwili kwa ajili ya matibabu.

Katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam (JNIA), Lissu ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Chadema (Bara), amesindikizwa na maofisa wa Ubalozi wa Ujerumani, Marekani, ndugu, jamaa na marafiki.

Akizungumza na MwanaHALISI Online, Lissu amesema, ameamua kuondoka nchini, pamoja na mambo mengi, kunusuru maisha yake na “kujipanga upya kisiasa.”

         Soma zaidi:-

Lissu anasema, amekuwa akitishiwa maisha yake, mara baada ya kumalizika kwa uchaguzi mkuu wa Oktoba, hali iliyomfanya yeye na wasaidizi wake watatu, kukimbilia kwenye makazi ya Balozi wa Ujerumani, jijini Dar es Salaam, ili kuomba hifadhi.

Mwanasiasa huyo amekuwa nyumbani kwa balozi huyo tangu Jumatano ya tarehe 4 Novemba 2020.

Katika uchaguzi huo, Lissu alitangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), kushika nafasi ya pili kwa kupata kura 1.9 milioni, huku Rais John Pombe Magufuli wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), akitangazwa mshindi kwa kupata kura 12 milioni kati kura 15 milioni zilizopigwa.

Kupatikana kwa taarifa kuwa maisha ya mwanasiasa huyo machachari wa upinzani nchini Tanzania yako hatarini, kunakuja miaka mitatu, tangu aliposhambuliwa kwa risasi na wanaoitwa, “watu wasiojulikana,” nyumbani kwake Area D, mjini Dodoma.

Shambulio dhidi ya Lissu, lilifanyika mchana wa tarehe 7 Septemba 2017, wakati alipokuwa akirejea nyumbani, akitokea viwanja vya Bunge, kuhudhuria mkutano wa Bunge la asubuhi.

Mara baada ya tukio hilo ambalo lilimjeruhi vibaya, mbunge huyo wa zamani wa Singida Mashariki (Chadema), alisafirishwa hadi nchini Kenya kwa matibabu zaidi na baadaye nchini Ubelgiji.

Lissu alirejea nchini Jumatatu, tarehe 27 Julai 2020, kutokea nchini Ubelgiji na kujitumbukiza moja kwa moja kwenye kinyang’anyiro cha urais wa Tanzania.

Katika hatua nyingine, mke wa Lissu, Alicia Magabe, ameondoka Tanzania kuelekea nchini Ubelgiji. Magabe aliondoka nchini, mwishoni mwa wiki iliyopita.

Haikuweza kufahamika mara moja, iwapo Magabe amekwenda Ubelgiji kuomba hifadhi ya kisiasa.

Lakini katika ujumbe wake kwa mmoja wa marafiki zake na ambao MwanaHALISI limeupata, Alicia amesema, “…Tanzania siyo salama. Ninaondoka na kurudi Ubelgiji. Natarajia Lissu naye ataondoka wiki ijayo. Tunaondoka kwa kuwa maisha yetu, hasa ya Tundu hayako salama.”

Akiwa katika uwanja wa ndege wa Dar es Salaam, Lissu amemueleza mwandishi wa habari hizi, kwamba haendi uhamishoni Ulaya; na au kama mkimbizi wa kisiasa. Amesema, “nakwenda kama mtu anayerudi alikokuwa ili kujipanga upya kisiasa.”

Saed Kubenea akifanya mahojiano na Tundu Lissu muda mchache kabla ya kuondoka nchini

Ameongeza, “mimi siyo mtu wa kukimbia vita. Maisha yangu yote, nimekuwa mtu wa mapambano,” amesema mbunge huyo wa zamani wa Singida Mashariki aliyewahi kuwa Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS).

Alipoulizwa anatoa wito gani kwa wananchi waliompigia kura na Watanzania wengine, Lissu amesema, “ujumbe wangu kwao, ni kwamba mimi sikimbii mapambano. Nakwenda kufungua uwanja mwingine mpya wa kudai haki, demokrasia na utu wetu kwa nchi yetu.”

MwanaHALISI Online na MwanaHALISI TV, litachapishwa kwa undani mahojiano yake na Lissu, kesho Jumatano, tarehe 11 Novemba 2020, ikiwa ni pamoja na jinsi alivyopata hati ya kusafiria, alivyofika kwenye makazi ya balozi na malengo yake ya baadaye ya kisiasa, hasa baada ya kumalizika kwa uchaguzi mkuu 2025 – Mhariri.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Mwekezaji amwaga bil. 39 kujenga viwanda 3 vya uchenjuaji

Spread the loveKampuni ya Mineral Access System Limited (MAST) inayoiwakilishwa kampuni ya...

Habari za SiasaTangulizi

Mpwa wa Magufuli mbaroni kwa kusambaza picha za utupu

Spread the loveJESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limewakamata...

Habari za Siasa

Serikali kuanzisha mradi wa Gridi ya maji ya Taifa

Spread the loveWaziri wa Maji, Jumaa Aweso amesema katika mwaka wa fedha...

Habari za SiasaTangulizi

Shibuda amlima waraka mzito Bulembo

Spread the loveMKONGWE wa siasa nchini, John Shibuda amemshukia kada maarufu wa...

error: Content is protected !!