Saturday , 20 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Lissu anavyojitofautisha na Lowassa, Dk. Slaa
Habari za SiasaTangulizi

Lissu anavyojitofautisha na Lowassa, Dk. Slaa

Spread the love

TUNDU Lissu, Mgombea Urais wa Tanzania kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), amesema katika Uchaguzi Mkuu wa tarehe 28 Oktoba 2020, chama hicho kina mikakati ya ushindi ya kutosha ikilinganishwa na chaguzi zilizopita. Anaripoti Mwandishi Wetu, Mwanza … (endelea).

Lissu ametoa kauli hiyo leo Jumamosi tarehe 26 Septemba 2020 wakati akizungumza na wanahabari kuhusu mwenendo wa kampeni zake za urais, wilayani Nyamagana mkoa wa Mwanza.

Lissu amesema katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 ambapo mgombea Urais wa Tanzania wa Chadema alikuwa Dk. Wilbrod Slaa na Uchaguzi wa mwaka 2015 mgombea akiwa Edward Lowassa, Chadema haikuwa na mikakati ya ushindi kuanzia ngazi ya juu hadi ngazi ya chini.

Katika Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2015 Chadema ilishirikiana na vyama vitatu na kutambulika kama Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kusimamisha mgombea mmoja wa urais na kuachiana majimbo na kata.

Vyama hivyo ni; NLD, CUF, NCCR-Mageuzi na Chadema yenyewe.

Lissu amesema katika uchaguzi wa mwaka huu, Chadema ina uwezo wa kuweka mawakala katika maeneo yote nchi nzima tofauti ilivyokuwa kwenye uchaguzi wa mwaka 2010 na 2015.

“Uchaguzi wa mwaka 2020 tupo kila mahali tofauti ya 2015, ndio maana jaribio la engua engua limeongezeka. Tukitaka kuweka mawakala nchi nzima tuna uwezo huo.”

“Hatukuweza kuweka katika chaguzi zilizopita, sasa tuna uwezo huo tuna matawi kila mahali. Mimi ni tofauti ya Dk. Slaa wa mwaka 2010 na Lowassa 2015 sababu nina oganaizesheni nchi nzima,” amejigamba Lissu.

Lowassa, waziri mkuu wa zamani na Dk. Slaa wote kwa pamoja wamekwisha rejea Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Lissu amesema, kilichofanya Chadema kuwa na mizizi nchi nzima ni utekelezaji wa operesheni ya ‘Chadema Ni Msingi’ iliyoanzishwa na chama hicho baada ya mikutano ya hadhara ya kisiasa kupigwa marufuku mwaka 2016.

“Wakati…akitupiga marufuku tulitumia Chadema ni msingi kutujenga, Chadema tuna oganaizesheni ambayo hakuna chama kingine inayo na hiyo ni kazi ya miaka mitano. Leo tukisema tuitishe wananchama wetu Mwanza tunajua wote walipo sababu tunayo majina yao kwenye kanzidata,” amesema.

 

“Hiyo ndio tofauti kati ya miaka ya nyuma na mwaka huu, ndio maana hata kama hatutotangazwa kwenye televisheni tunafanya kazi tuko poa tukitaka watu waje Mwanza wanakuja bila shida sababu tuna oganaizesheni,” amesema Lissu.

Akizungumzia mwenendo wa kampeni zake, Lissu amesema katika awamu ya pili ya kampeni hizo ameshafika zaidi ya mikoa 10 huku awamu ya kwanza akimaliza Kanda zote kumi za chama hicho.

“Tangu tulipoanza raundi ya pili ya kampeni hii, mtakumbuka ya kwanza tulifanya mikutano ya uzinduzi katika kanda kumi ya nchi na hiyo raundi iliisha mwanzoni mwa mwezi huu, tangu raundi ya pili imeanza tumefanya mikutano katika mikoa 12 licha ya kuzuiwa kutumia chopa,” amesema Lissu.

Lissu amesema mwitikio wa wananchi kwenye mikutano yake umekuwa ukiongezeka kila siku.

“Tumefanya kazi kubwa kila tunapoenda tunavunja rekodi, jana Nyamagana ilivunja ya Geita, Geita ilivunja ya Bukoba. Imekuwa ni wiki ya raundi ya pili ya kuvunja rekodi kila mahali tofauti na mikutano ya CCM na watu wake.”

Tundu Lissu, Mgombea Urais wa Tanzania kwa tiketi ya Chadema

“Sisi watu wetu wanakuja bila kubebwa kwenye matrekta, mabasi bila kupewa Sh.5,000 na watoto kulazimishwa kwenda kwenye mikutano. Mikutano yetu watu wanakuja kwa hiari yao licha ya kutotangazwa kwenye vyombo vya habari mikutano yetu tunatangaza wenyewe,” amesema Lissu.

Amesema, akichaguliwa kuwa Rais atahakikisha atatengeneza mahusiano na mataifa mengine.

“Nimesema na sera yetu imesema, nitatengeneza mahusiano na nchi zote rafiki duniani, hizo mnazoita nchi za kibeberu hizo mnazitegemea kwa kila kitu karibu, zinafundisha mpaka majeshi yetu, mimi sisi tutazihitaji sana,” amesema Lissu

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

BiasharaHabari za Siasa

Mavunde aagiza Perseus kuharakisha fidia Sengerema

Spread the loveWaziri wa Madini, Anthony Mavunde ameipongeza Kampuni ya Perseus kwa...

Habari za Siasa

Kigogo Chadema awanyooshea vidole vigogo serikalini kuhusu ripoti ya CAG

Spread the love  MWANACHAMA wa Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Boniface Jacob, amedai...

Habari za Siasa

Wabunge waikalia kooni TAKUKURU Bungeni

Spread the love  BAADHI ya wabunge wamelia na changamoto za utendaji wa...

Habari za SiasaTangulizi

Mpina ataka Waziri Majaliwa ajiuzulu, akosoa teuzi za mawaziri

Spread the love  MBUNGE wa Kisesa, Luhaga Mpina, amemtaka Waziri Mkuu, Kassim...

error: Content is protected !!