Friday , 19 April 2024
Home Habari Mchanganyiko Lissu aitwa mahakamani
Habari Mchanganyiko

Lissu aitwa mahakamani

Tundu Lissu, aliyekuwa Mbunge wa Singida Mashariki
Spread the love

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam, imemtaka Tundu Lissu, Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kuhudhuria mahakamani hapo tarehe 26 Agosti 2020 shauri lake litakapoitwa tena. Anaripoti Faki Sosi, Dar es Salaam …(endelea).

Amri hiyo, imetolewa leo Alhamisi tarehe 30 Julai 2020 na Hakimu Mkazi Mkuu Augustina Mbando wakati kesi mbili zinazomkabili Lissu zilipoitwa mahakamani hapo.

Peter Kibatala, wakili wa Lissu ameiambia Mahakama mteja wake amelazimika kujiweka karantine kwa uangalizi binafsi na mapumziko ya safari na kuumwa muda mrefu.

Kesi hizo ni namba 236 ya mwaka 2017 na kesi namba 123 ya mwkaa 2017 za uchochezi.

         Soma zaidi:-

Kesi namba 236 ya mwaka 2017 imeitwa mbele ya Hakimu Mbando ambapo wakili wa Serikali Mkuu, Simon Wankyo amedai upande huo ulitarajia kumsomea maelezo ya awali mshtakiwa hivyo ipangiwe siku nyingine kwa ajili ya kuendelea na usikilizwaji.

Pia, Wankyo ameiomba Mahakama, kuwaamuru wadhamini wa Lissu kueleza sababu iliyosababisha Lissu kutohudhuria mahakamani hapo leo.

Wakili wa utetezi, Kibatala ameiambia Mahakama kuwa, Lissu ametoka kwenye matibabu hivi karibuni hivyo anatakiwa kupumzika huku akichunga afya yake.

Hakimu Ndambo amesema, Kibatala ahakikishe tarehe 26 Agosti, 2020 Lissu anahudhuria mahakamani hapo.

Kwenye kesi hiyo, Lissu anashtakiwa kwa kutoa maneno ya uchochezi tarehe 17 Julai 2017 Kinondoni Dar es Salaam ya kujaza chuki.

Baadhi ya maneno hayo ya uchochezi ni; Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais John Pombe Magufuli ni ya kibaguzi wa kifamilia, kikabila, kikanda na kidini.

Pia, kwenye kesi namba 123 ya Mwaka 2017 iliyoitwa leo Alhamisi, mbale ya Hakimu Mkazi Mkuu, Kassian Matembele, Lissu anakabiliwa na tuhuma za kutoa maneno ya uchochezi.

Inadaiwa tarehe 11 Januari 2017 akiwa Kombeni mkoani Mjini Magharibi Zanzibar kwenye kampeni za uchaguzi mdogo wa ubunge wa Diman, alitoa maneno yenye udini na yenye kuchochea.

“Kwa hiyo hicho kinachoitwa uchaguzi wa marudio uharamia mtupu, haramu, haramu, kinachoitwa uchaguzi wa marudio ni haramu tupu, nyie ni Waislam sana naomba niseme uharamu wa uchaguzi wa marudio wa mwaka jana hautofautiani na kula Nguruwe kwa wala nguruwe…”

Kesi hii nayo, imeahirishwa hadi tarehe 26 Agosti 2020.

Lissu amerejea nchini Tanzania Jumatatu iliyopita tarehe 27 Julai 2020 akitokea Ubelgiji alikokuwa akipatiwa matibabu baada ya kushambuliwa kwa risasi zaidi ya 30 na watu wasiojulikana mchana wa tarehe 7 Septemba 2017.

Alifikwa na mkasa huo akiwa ndani ya gari kwenye makazi yake Area D jijini Dodoma akitoka kuhudhuria mkutano wa Bunge asubuhi.

Baada ya kushambuliwa, alipelekwa Hospitali ya Rufaa Dodoma kwa matibabu ya awali kabla ya usiku wa siku hiyohiyo kuhamishiwa Hospitali ya Nairobi nchini Kenya kwa matibabu zaidi.

Tarehe 6 Januari 2018 alihamishiwa Ubelgiji kwa matibabu zaidi.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

BiasharaHabari Mchanganyiko

NMB Pesa Akaunti yawavutia wakaguzi wa ndani Afrika

Spread the loveUbunifu wa bidhaa bora wa Benki ya NMB pamoja na...

Habari Mchanganyiko

Carbon First, Ruangwa wasaini makubaliano ya biashara ya hewa ukaa

Spread the love  KAMPUNI ya Carbon First Tanzania Limited na Halmashauri ya...

Habari Mchanganyiko

CBE yawakumbuka wenye mahitaji maalum Jangwani

Spread the loveCHUO cha Elimu ya Biashara (CBE), kimetoa msaada mbalimbali na...

Habari Mchanganyiko

Mume auwa mke kwa kumchoma visu, ajisalimisha Polisi

Spread the loveJACKSON Kalamji (49), anashikiliwa na Jeshi la Polisi jijini Mwanza,...

error: Content is protected !!