Tuesday , 23 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Lissu aeleza atakachomwambia Rais Magufuli wakikutana
Habari za SiasaTangulizi

Lissu aeleza atakachomwambia Rais Magufuli wakikutana

Spread the love

ALIYEKUWA mgombea urais wa Tanzania kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika tarehe 28 Oktoba 2020, amemshauri Rais John Pombe Magufuli kuitisha meza ya majadiliano na wapinzani ili kuleta Umoja wa Kitaifa. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Makamu huyo mwenyekiti wa Chadema (Bara) ametoa wito huo jana Ijumaa tarehe 13 Novemba 2020 wakati anahojiwa na Idhaa ya Kiswahili ya Sauti ya Amerika (VOA), kuhusu msimamo wake juu ya matokeo ya uchaguzi huo.

Lissu ametoa ushauri huo siku kadhaa tangu Rais Magufuli aingie madarakani katika muhula wake wa pili wa uongozi wa Serikali ya awamu ya tano, baada ya kuapishwa tarehe 5 Novemba 2020 kufuatia kushinda uchaguzi wa kiti cha Urais wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Katika uchaguzi huo, Rais Magufuli aliyetangazwa mshindi na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kwa kupata kura milioni 12 kati ya milioni 15 zilizopigwa sawa na asilimia 84, alichuana vikali na Lissu aliyetangazwa kupata kura milioni 1.9 sawa na asilimia 13.

Alipoulizwa endapo akipata nafasi ya kuonana na Rais Magufuli atampa ushauri gani Lissu amesema, “Ningemwambia rais itisha mkutano wa kitaifa wa maridhiano utengeneze nchi ambayo makundi mbalimbali ya kisiasa yataridhiana, kuwe na nchi ambayo itakua ya umoja wa kitaifa.”

Lissu amesema kama suala hilo halitafanyika, Taifa la Tanzania litakuwa na wakati mgumu na hata kutengwa na Jumuiya za Kimataifa.

Mwanasiasa huyo ambaye kwa sasa anaishi nchini Ubelgiji alikokwenda kwa madai ya kulinda usalama wa maisha yake, amemshauri Rais Magufuli, arudi nyuma kwa kutafuta maridhiano ili wananchi wa kada zote wapate nafasi ya kulijenga Taifa lao.

“Huko unakoelekea, unakwenda kutumbukiza kwenye shimo kubwa na kuangamia, rudi nyuma fanya maridhiano tujenge nchi ya pamoja na kidemokrasia, sisi tunahitaji dunia zaidi ya dunia kutuhitaji sisi,” amesema Lissu.

Anachokisema Lissu, kinafanana na alichokieleza Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia alipozungumza na waandishi habari tarehe 12 Novemba 2020 makao makuu ya chama hicho, Ilala jijini Dar es Salaam aliposema “Tanzania tunaihitaji dunia kuliko dunia inavyoihitaji Tanzania, hatuwezi kusema eti sisi hatuihitaji dunia hasa kipindi hiki cha teknolojia.”

Mbatia alisema “sisi NCCR-Mageuzi tumetafakari na kukubaliana utajiri uko na ulichonacho na sisi utajiri wetu ni ilani yetu na ilani yetu tulipoizindua, ajenda namba moja ni muafaka wa kitaifa. Sisi tunahitaji kuwapo na muafaka wa kitaifa, chuki zinaendelea, watu wanauana.”

“Kila kukicha chuki inaendelea, tunatoa rai kwa viongozi wetu wote wa kijamii kutumia ndimi zetu vizuri na kwa njia chanya kwa sababu Tanzania tunaihitaji dunia kuliko dunia inavyotuhitaji sisi,” alisema Mbatia aliyekuwa mgombea Ubunge wa Vunjo Mkoa wa Kilimanjaro

Alisema, vyombo mbalimbali vya habari duniani “vinazungumzia mambo hasi kuhusu Tanzania, tunakokwenda siko. Mmesikia Mahakama ya Jinai, matamko ya Uingereza, Umoja wa Ulaya, Marekani, yatupasa sisi tulipofika kuchunga sana ndimi zetu. Tukubali kutokubaliana kwamba maslahi ya mama Tanzania kwanza. Kichaka kilichotuhifadhi tusikitie moto.“

James Mbatia, Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi

Itakumbukwa, Lissu aliondoka nchini Tanzania kuelekea Ubelgiji Jumanne ya tarehe 10 Novemba 2020, kwa maelezo kwamba hatua hiyo imelenga kunusuru uhai wake lakini pia kujipanga upya na mapambano ya kuhami demokrasia nchini humo.

Wito huo wa Lissu umekuja katika kipindi ambacho baadhi ya vyama vya siasa vya upinzani nchini Tanzania, vimeweka msimamo wa kutotambua matokeo ya uchaguzi mkuu huo kwa madai haukuwa huru na wa haki.

Chadema, ACT-Wazalendo, Chama cha Wananchi (CUF), Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma) na NCCR-Mageuzi ni miongoni mwa vyama vilivyopinga kutambua matokeo ya uchaguzi huo huku baadhi yao vikitaka meza ya majadiliano kutafuta suluhu ya sintofahamu hiyo.

Vyama hivyo vimepinga matokeo hayo yaliyotangazwa na NEC, ambayo yalikipa ushindi wa kishindo Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika uchaguzi wa urais, ubunge, uwakilishi na udiwani.

1 Comment

  • Ndugu lissu asante lakini tambua hakuna muda wa kusikia habari zako uchaguzi umekwisha siasa imeamia bungeni na wananchi wanajenga taifa lissu umekimbia kujenga taifa letu

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Mwekezaji amwaga bil. 39 kujenga viwanda 3 vya uchenjuaji

Spread the loveKampuni ya Mineral Access System Limited (MAST) inayoiwakilishwa kampuni ya...

Habari za SiasaTangulizi

Mpwa wa Magufuli mbaroni kwa kusambaza picha za utupu

Spread the loveJESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limewakamata...

Habari za Siasa

Serikali kuanzisha mradi wa Gridi ya maji ya Taifa

Spread the loveWaziri wa Maji, Jumaa Aweso amesema katika mwaka wa fedha...

Habari za SiasaTangulizi

Shibuda amlima waraka mzito Bulembo

Spread the loveMKONGWE wa siasa nchini, John Shibuda amemshukia kada maarufu wa...

error: Content is protected !!