Friday , 29 March 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Lema arejea uraiani, Arusha yasimama
Habari za SiasaTangulizi

Lema arejea uraiani, Arusha yasimama

Spread the love

GODBLESS Lema, Mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini amerejea tena uraiani, ikiwa ni takribani miezi minne tangu alipokamatwa na Jeshi la Polisi na kusafirishwa kutoka mkoani Dodoma mpaka Arusha, kisha kupandishwa kizimbani na dhamana yake kuzuiliwa, anaandika Mwandishi Wetu.

Mahakama Kuu Kanda ya Arusha imetoa uamuzi wa kumpa dhamana Lema leo, ikiwa ni siku tano tu tangu Mahakama ya Rufaa ilipomuonya Mkurugenzi wa mashtaka wa serikali DPP kwa kuzuia dhamana ya Mbunge huyo bila sababu zenye mashiko.

Kabla ya uamuzi huo, Jeshi la Polisi mkoani Arusha lilisababisha mtafaruku mkubwa baada ya kuwashambulia wananchi waliofika mahakamani kufuatilia kesi hiyo na kuwazuia kuingia katika lango la mahakama.

Polisi iliwashambulia baadhi ya wananchi na wengine wakiripotiwa kukamatwa baada ya kukusanyika nje ya eneo la Mahakama Kuu ambapo magari ya maji ya kuwasha, yenye polisi waliojihami kwa silaha za moto walilizingira eneo hilo na kuendesha doria.

Faraja Nchimbi na Paul Kadushi mawakili wa serikali walilazimika kuomba dakika 15 ili waweze kujibu hoja za Peter Kibatala aliyeongoza jopo la mawakili wa utetezi, ambapo Jaji Salma Magimbi alikubali na kuwapa saa moja na mahakama kuahirishwa mpaka saa saba mchana.

Baada ya mahakama kurejea mchana na wakili wa serikali kujibu hoja za mawakili wa utetezi, Jaji Salma Magimbi alitoa uamuzi wa kutoa dhamana kwa Lema kwa maelezo kuwa hoja za mawakili wa serikali hazina mashiko.

Uamuzi huo wa Mahakama Kuu umepokelewa na kwa shangwe katika mitaa mbalimbali ya jiji la Arusha ambapo baadhi ya wananchi walikuwa wakishangilia na kuimba jina la Mbunge huyo katika viunga vya nje ya mahakama na hata mitaani.

Baadhi ya viongozi wa Chadema taifa waliohudhuria mahakamani leo na kushuhudia Lema akipewa dhamana ni pamoja na Freeman Mbowe, mwenyekiti wa chama hicho na Mbunge wa Hai, Mawaziri wakuu wastaafu Frederick Sumaye na Edward Lowassa, Dk. Vincent Mashinji, Katibu Mkuu na John Mnyika, Naibu Katibu Mkuu Bara.

Wengine ni Calist Lazaro, Meya wa Jiji la Arusha, Patrobasi Katambi, mwenyekiti wa Baraza la Vijana wa Chadema taifa, wabuge na madiwani wa jiji la Arusha.

Kiongozi wa jopo la mawakili wa utetezi, Kibatala ameiambia MwanaHALISI Online kuwa, “Lema ameelekea nyumbani kwake. Hajakaa na familia yake muda mrefu hivyo chama kimeona ni vyema kwa sasa akapumzike na familia yake kabla ya kuendelea na majukumu ya ubunge.”

Lema alikamatwa mkoani Dodoma wakati vikao vya Bunge vikiendelea mnamo tarehe 02 Novemba, 2016 na kusafirishwa mpaka mkoani Arusha ambako alihojiwa na hatimaye kupandishwa kizimbani kwa tuhuma za uchochezi.

Lema alidaiwa kufanya uchochezi baada ya kunukuliwa akisema kuwa ameota kuwa Rais John Magufuli atakufa kabla ya mwaka 2020, iwapo hatabadili aina ya utawala wake. Hakupewa dhamana mpaka siku ya leo.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Nani anasema kuna hasara ATCL?

Spread the loveRIPOTI za makusanyo na matumizi ya fedha katika Kampuni ya...

Habari za SiasaTangulizi

CAG: Wastaafu, wenza wao chanzo NHIF kufilisika

Spread the loveRIPOTI ya ukaguzi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu...

Habari za SiasaTangulizi

Vikundi hewa 851 vyalamba bilioni 2.6 mikopo ya halmashauri

Spread the loveVIKUNDI hewa vya wajasirimali wadogo 851 kutoka katika halmashauri 19...

Habari za SiasaTangulizi

Mashirika matano yapata hasara mabilioni ya fedha

Spread the loveMASHIRIKA matano ya Serikali yanayojiendesha kibiashara, yamepata hasara ya mabilioni...

error: Content is protected !!