Friday , 29 March 2024
Home Habari Mchanganyiko Kukamatwa kwa Kabendera utata mtupu
Habari Mchanganyiko

Kukamatwa kwa Kabendera utata mtupu

Erick Kabendera
Spread the love

KUKAMATWA na kushtakiwa kwa Mwandishi wa Habari za uchunguzi Erick Kabendera kumedaiwa kuwa kuna mashaka. Anaaripoti Faki Sosi … (endelea).

Tamko la wadau wa habari na haki za binadamu lilotolewa  leo limetilia shaka kukamatwa namna askari walivyokwenda nyumbani kwake na kumkamata alivyobadilishwa kwenye vituo vya polisi tofauti bila familia yake kupewa taarifa.

Wadau hao ni pamoja Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC), Baraza la vyombo vya Habari Tanzania (MCT)  umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari (UTPC) na Jukwaa la Wahariri (TEF).

Kajubi Mukajanga, Katibu Mtendaji MCT  amesema kuwa  kitendo cha askari Polisi waliomkamta Kabendera siku ya tarehe 29, Julai 2019, kwenda nyumbani kwake kumkamata bila kutumia taratibu za kisheria kinajenga mashaka ya sababu za kukamatwa kwake.   

Amesema kuwa kwa mujibu wa maelezo ya mke wake na jirani zake, gari iliyotumika kumchukua haikuwa na namba za polisi na ilikuwa imesajiliwa kwa namba T746 DFS. Rekodi ya kamera za CCTV zinaonyesha watu waliojitambulisha kuwa ni askari polisi walimkamata na kuondoka naye nyumbani kwake. 

“Mke wake alieleza kuwa kundi la watu sita waliojitambulisha kuwa ni askari polisi ambao hawakuvaa sare, walifika na gari na kuizingira nyumba yake kwa zaidi ya saa tatu, kuanzia saa tisa alasiri hadi saa kumi na mbili jioni. Baadaye Kabendera alikamatwa kwa maelezo kuwa wanampeleka kituo cha polisi cha Oysterbay,” ameeleza Mukajanga.

Makajanga amesema kuwa kabla ya kukamatwa kwake, simu zake za mkononi zilikuwa hazipatikani na laini za simu zilikuwa hazifanyi kazi. Alipiga simu mtandao wa Vodacom kuulizia nakujibiwa kuwa wamepokea maagizo kutoka katika Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kuzuia kadi zake za simu.

Amesema kuwa inasadikiwa kuwa sababu za kuzimwa kwa simu zake ni kwa kuwa alikuwa anawasiliana na majirani na viongozi wa Mtaa kuhusu uwepo wa gari lisiloeleweka getini kwake baada ya kuwachunguza kupitia CCTV.

Amesema kuwa taarifa yenye mashaka zaidii ni juu kukosekana kwa taarifa za kuwa ni kituo gani cha Polisi alichoshikiliwa Kabendera licha  ya maafisa wa polisi katika kituo cha Oysterbay na kituo Kikuu cha Kati walikataa kuwa wanamshikilia Erick Kabendera.

“Baada ya mivutano mingi na kuonesha ushahidi wa kuwa Kabendera amechukuliwa na  Jeshi la Polisi, ndipo Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa, alikiri kuwa Kabendera alikamatwa na Jeshi la Polisi na ameshikiliwa kwa mahojiano kuhusu uraia wake”, amesema Mukajanga.

Amesema kuwa kabla ya kituo cha polisi alichoshikiliwa kujulikana, Mke wa Bwana Kabendera alizunguka vituo vingi vya polisi akijaribu kumtafuta mumewe lakini hakufanikiwa.

“Ndipo alipokutana na kamanda wa polisi, Lazaro Mambosasa, ambae alimwambia aende        Kituo cha Polisi cha Kati mnamo tarehe 31 Julai, 2019 saa 2 asubuhi. Pia Mke wa mwandishi huyo aliripoti kuwa alipokea simu  iliyomwamuru kusalimisha hati ya kusafiria ya mumewe na nakala za kitaaluma kwa Waziri wa Mambo ya ndani,” amesema Mukajanga.

Amesema kuwa ni zaidi ya masaa 44 yalipita toka Kabendera akamatwe na kuwekwa kizuizini katika kituo cha polisi ambacho hakikufahamika mara moja, mpaka tarehe 31 Julai, 2019 ilipodhihirishwa kuwa yupo katika kituo cha Polisi cha Barabara ya Kilwa.

Akizungumzia matakwa ya sheria juu ya haki ya mtuhumiwa, Onesmo Olengurumwa Mkurugenzi wa (THRDC) amesema mtu yoyote anaposhikiliwa na jeshi la Polisi, anatakiwa kuelezwa mashtaka yake kama yalivyomatakwa ya sheria namba 23  ya mwenendo wa Makosa ya jinai.

Amesema kuwa Kabendera alipokamatwa hakuambiwa chochote zaidi ya kuwa anapelekwa kituo cha polisi tena baada ya majirani kuzunguka gari na kuhoji anapopelekwa.

“Sababu za kukamatwa kwake ziliwekwa wazi baada ya siku kadhaa kupita katika mkutano na waandishi wa habari uliofanywa na Kamanda Mambosasa. Huu sio utaratibu sahihiwa kisheria,” amesema Olengurumwa.

Amesema licha kudaiwa kuhojiwa juu uraia wake Idara ya uhamiaji haijatoa taarifa yoyote kuhusu uchunguzi uliofanywa. Badala yake walimkabidhi kwa maofisa wa Jeshi la Polisi huku ikionekana hakuna tena tatizo la uraia.

 “Hadi sasa Idara ya uhamiaji hajamtangaza Erick kuwa sasa ni raia halali na pasi za kusafiria za Erick na familia yake bado pia wanazishikilia. Ikumbwe suala la uraia ndio lililokuwa kosa la kwanza alilitohumiwa nalo baada ya kukamatwa,” anasema Olengurumwa.

Olengurumwa anasema kuwa Kabendera hakufikishwa mahakamani kwa wakati uliowekwa kisheria hasaa kifungu cha 32(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai.

Amesema licha ya kukiukwa kwa sheria hiyo Kabendera hakutendewa haki ya kuwakilishwa na wakili wakati anatoa maelezo yake alipokuwa akihojiwa na jeshi la Polisi.

“Kifungu cha 54 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai mwaka 1985 kinaeleza kuhusu haki ya msingi ya mshtkiwa kuonana na wakili na ndugu wa karibu,” anasema Olengurumwa.

Deodatus Balile Makamu Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri nchini (TEF) amesema  kuwa Kabandera amekuwa amebadilishiwa mashtaka zaidi ya mara tatu ndani ya siku tano.

Amesema wakati mawakili wa Kabendera wapo mahakamani wanajiandaa kumtetea na kumuombea dhamana ya polisi kwa siku sita bila mafaniko jeshi la Polisi linaibuka naye mahakamani kwa mashtaka tofauti na aliyohojiwa nayo.

Akitoa wito Rais wa Klabu za Waandishi wa Habari nchini, Deogratius Nsokolo amesema kuwa kutokana na ukweli kwamba awali Kabendera alihojiwa kuhusu uraia wake na maofisa wa Uhamiaji kabla ya kubadilishiwa tuhuma, tunawasihi  maofisa wa uhamiaji watoe tamko kwamba Erick ni Raia wa Tanzania au vinginevyo kwa mujibu wa uchunguzi wao;

“Tunashauri  suala la uraia lisitumike kama silaha ya kuwanyamazisha Watanzania wanaopenda kuhoji mambo ya msingi ya kitaifa,” amesema.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari Mchanganyiko

Mtandao watetezi wa haki za mazingira Tanzania waundwa

Spread the loveMTANDAO wa watetezi wa haki za mazingira nchini Tanzania, umeundwa...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Kapinga kuongoza usambazaji wa mitungi ya gesi 10,000 ya Taifa Gas

Spread the loveNaibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga ameahidi kuongoza kwa ufanisi...

BiasharaHabari Mchanganyiko

Wafanyabiashara, wawekezaji China waridhia kuwekeza bil. 800 katika sekta 5 nchini

Spread the loveUJUMBE wa wafanyabiashara na wawekezaji wakubwa kutoka Jimbo la Changzhou...

Habari Mchanganyiko

Bil. 4.42 kumaliza uhaba maji kata 2 Musoma Vijijini

Spread the loveWANANCHI wa kata za Busambara na Kiriba, Jimbo la Musoma...

error: Content is protected !!