Thursday , 25 April 2024
Home Gazeti Makala & Uchambuzi Kujivika utukufu ni kujivika uzuzu
Makala & Uchambuzi

Kujivika utukufu ni kujivika uzuzu

Mwalimu Julius Kambarage Nyerere
Spread the love

WAPENDWA tuanze maandiko ya leo kama tulivyoanza maandiko ya mara ya mwisho. Tulikumbushana kuwa sisi wote tumekutana katika nchi hii pasipo wenyewe kuridhia! Anaandika Mwalimu Mkuu wa Watu…(endelea).

Hakuna kati yetu aliyeomba azaliwe katika nchi hii ambayo sasa inaitwa Tanzania. Nani alimchagua mwenzake
wakutane Tanzania?

Tumekutana katika nchi hii pasipo ridhaa yetu. Au tumewakuta wenzetu au wenzetu wametukuta sisi. Ndiyo kusema katika nchi hii na nchi nyingine duniani kote hakuna raia aliye na haki Zaidi ya mwingine.

Hivyo haki sawa kwa wote ndiyo busara kuu kwa nchi zote. Watawala wote waliozingatia ukweli huu walizijenga nchi zao katika amani ya kweli. Wananchi waliishi kwa amani nao wakastawi.

Mfano bora wa nchi hizo ni Tanganyika na Tanzania ya Nyerere. Wakati wa Nyerere wananchi hawakukumbuka kama kila mtu alikuwa na kabila lake. Wote walikuwa waswahili kwa lugha siyo kwa kabila.

Leo kila Mtanzania anajua kabila lake. Wachache wanajiuliza kwanini mkosi huu? Leo tuna sisi na tuna wao. Vyama vya siasa ambavyo vilianzishwa kwa matakwa ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere kwa matarajio kwamba, vingewastawisha Watanzania zaidi ndivyo vimekuwa chimbuko la mafarakano katika nchi yetu.

Na hii yote imesababishwa na hali iliyotengenezwa sasa ambapo kila mtu anaweza kuwa kiongozi. Lazima
tukubali kuwa, uongozi ni karama itokayo kwa Mwenyezi Mungu mwenyewe.

Na mtu hupewa karama hiyo toka angali tumboni mwa mama yake! Kamwe, kiongozi hatengenezwi! Kiongozi anazaliwa! Kiongozi hawezi kupatikana kwa kujaribu! Kiongozi wakweli kama alivyokuwa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere angeona ni ujinga mkubwa kuitwa mheshimiwa na watu wake mwenyewe!

Wako viongozi ambao si viongozi halisi, wanaoona ni ufahari kuitwa waheshimiwa. Nyerere alilikemea hili na nina hakika leo angesema ni ujinga.

Huu ni ujinga ulioletwa na wapinzani wakati huo wakiitwa wanamageuzi. Na kwa uroho wa utukufu waliokuwa nao watawala, wakauridhia.

Kujivika utukufu ni kujivika uzuzu. Abdulrahman Kinana mwana yule, pekee alikemea sana upuuzi huu, akiwataka viongozi kujivua utukufu, lakini zuzu anasikiaga?

Wapendwa namheshimu sana Kinana kwasababu ndiye kiongozi wa juu anayesadiki na kujua kuwa sijawahi kuwa na sina mpango wakuwa mwanachama wa chama chochote cha siasa katika maisha yangu.

Nilikuwa na wanasiasa wanne wa mfano ambao mpaka leo hawajachuja. Edward Moringe Sokoine ametangulia mbele ya haki lakini ameniachia Augustino Lyatonga Mrema, Edward Ngoyayi Lowassa na Rais wangu!

Simpendi mtu wala simchukii mtu kwa umbo lake. Hawa ni watu ambao kwa utendaji wao huko nyuma, timamu wa nchi hii hawatakuja kuwapuuza hata siku moja.

Komredi Kinana alijitofautisha zaidi na wengine katika fikra zangu pale alipokuja nyumbani kwangu jioni na kuniambia,

“Rais (siyo huyu) amenituma, nije nikuulize, unataka uwe nani?” Nikamjibu kwa kumwomba akaniombee kwa Rais ili anibakishe hivi nilivyo!

Wapuuzi wangeniona mjinga kuukataa ‘ulaji’, lakini yeye alinijibu, “Naelewa, najua ‘filosofazi’ hawataki kutawala”.

Wakati namsindikiza, huku akijishika kifuani aliniambia, “Bwana Mayega una amani kubwa sana kifuani mwako!”

Hakuna kitu kinachoweza kumpa mtu heshima kubwa kama kuusimamia ukweli anaouamini. Kubadilika kwasababu ya cheo ni kujidhalilisha na kuiaharibu heshima yako ambayo uliijenga kwa muda mrefu.

Wapendwa, akihutubia mjini Mbeya, Mwalimu Julius Nyerere alisema, “Watanzania wanataka mabadiliko.
Wasipoyapata ndani ya CCM watayatafuta nje ya CCM.”

Serikali ya awamu ya tano ndiyo iliyoko madarakani hivi sasa. Mema yote yanayotendeka nchini mwetu hivi sasa yanahesabiwa kuwa yanafanywa na serikali. Vivyo hivyo maovu yote yanayotendeka katika nchi hii yanahesabika yanafanywa na serikali.

Je, awamu ya tano waliishakaa na kujitathimini ni mabadiliko ya aina gani Watanzania wanayataka? Tumeshuhudia katika Uchaguzi Mkuu uliopita ambapo waliohubiri mabadiliko walivuta umati mkubwa wa wananchi kwa gharama zao kuliko waliotegemea kuitiwa watu na wasanii na wakati mwingine kulazimika kutoa usafiri na posho.

Hakuna sasa kinachosemwa kuhusu mabadiliko utadhani wananchi wameishayapata. Mabadiliko wanayoyataka ni yale yanayowahusu wao katika elimu, afya na ustawi, siyo yale ya kuwanunulia vitu!

Wakati Rais wetu anafanyakazi bila kuwa na Baraza la Mawaziri, aliwajaza matumaini makubwa wananchi kwa kufukua ufisadi mkubwa ukiwemo ule wa makinikia ambao walidhani matokeo yake maisha yao yangeboreshwa.

Kufukua madudu ni jambo la ujasiri kuonyesha uthubutu. Lakini kuonesha nchi ilivyoliwa na manyang’au kuwa pale walikula kiasi kadhaa na hapa kiasi kadhaa halafu basi, hakumsaidii yeyote.

Wahusika wako wapi? Waliochua fedha za ESCROW wako mahabusu. Walioruhusu wachukue wako wapi? Zilitoka ripoti za makinikia na sasa za gesi. Wanaotajwa ni walewale!

Wakati wananchi nchini Kenya wanafanya maandamano makubwa katika miji mikubwa ya nchi hiyo kulaani ufisadi wa mabilion ya dola katika serikali pamoja na kutokamatwa kwa baadhi ya washukiwa, huku kwetu Spika wa Bunge anasema;

“Tatizo letu kubwa lipo kwenye kitu kinaitwa mikataba. Songas ni kampuni nyonyaji. Wakishirikiana na PAET, wameiumiza sana TANESCO na TPDC. Unafika mahali vitalu vyote vinne vya Songosongo unawapa Songas, umerogwa au una kichaa?” Halafu basi, yameisha!

Kwanini kutumia mapesa mengi kufichua madhambi ambayo yametendwa na watu tunaowahofia kuwachukulia hatua? Timamu gani atatupongeza kwa utendaji kama huu?

Wananchi waliipokea dhana ya Tanzania ya Viwanda kwa ari kubwa. Lakini alipokuja kijana wake na kufafanua walichomaanisha, kuwa hata vyerehani vinne tu ni kiwanda, akaifanya dhana nzima ionekane ni mzaha mtupu!

Anayekusifia kwa hili anakung’ong’a! Wapendwa tukubali awamu ya tano ina deni kubwa kwa wananchi kuwaeleza
hofu ya wasiojulikana ilitoka wapi!

Serikali ya watu kukiri mbele ya watu wake kuwa, kuna watu waovu wanaowadhuru watu wake lakini haina uwezo wakuwakamata na hata kuwajua tu, ni sawa na kukiri kuwa imeshindwa kuwalinda.

Kazi ya kwanza ya serikali ya watu ni kuwalinda watu wake na mali zao. Kukiri kushindwa ni kukiri kuwa haifai!

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

BiasharaMakala & Uchambuzi

Kanda ya Ziwa yaonyesha NMB inavyosaidia afya ya mama na mtoto

Spread the loveMafanikio inayozidi kupata Tanzania katika kupunguza vifo vya mama na...

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

‘Mwanapekee’ wa Rais Samia: Atabadili nini Arusha?

Spread the loveMAPEMA wiki hii, baadhi ya viongozi walioapishwa na Rais Samia...

Habari MchanganyikoMakala & Uchambuzi

Kipunguni waihoji serikali, ziko wapi fedha za fidia?

Spread the loveWATU wanaodai kwamba serikali ya Chama Cha Mapinduzi ni sikivu,...

Habari za SiasaMakala & UchambuziTangulizi

Askofu Bagonza: Tusichonganishwe; tusichokozane na tusikufuru

Spread the loveJOTO la chaguzi linapanda kila siku hapa nchini. Upo umuhimu...

error: Content is protected !!