Tuesday , 19 March 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Kubenea: Serikali imeidharau Mahakama
Habari za SiasaTangulizi

Kubenea: Serikali imeidharau Mahakama

Spread the love

KAMPUNI ya Hali Halisi Publishers Ltd (HHPL) inayomiliki na kuchapisha magazeti likiwemo la MwanaHALISI inaamini kuwa serikali imekiuka amri ya Mahakama Kuu ya kuzuiwa kulifungia gazeti hilo, labda tu kama itatumia utaratibu wa kufungua kesi mahakamani, anaandika Pendo Omary.

Mkurugenzi Mtendaji wa HHPL, Saed Kubenea ametoa tamko hilo mbele ya waandishi wa habari aliokutana nao leo kwenye ofisi za kampuni hiyo ili kuzungumzia uamuzi wa serikali kufungia gazeti hilo kwa muda wa miaka miwili.

Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Anastazia Wambura alimwandikia barua Mhariri wa MwanaHALISI mnamo tarehe 19 Septemba 2017 kumjulisha kufungiwa kwa gazeti hilo kwa kile kilichoelezwa “kutokana na mwenendo na mtindo wa kichochezi wa uandishi wa habari na makala ambao unakiuka kwa kiasi kikubwa misingi ya maadili ya taaluma ya habari.”

Kubenea ambaye pia ni Mhariri Mtendaji wa gazeti hilo, amesema amemtuma wakili kumwandikia naibu waziri huyo tamko la kumtaka kufuta amri yake hiyo ndani ya siku mbili kwa sababu amechukua hatua asiyostahili kisheria kwani hana mamlaka ya kufungia gazeti.

“Wakili wetu tayari ameshampelekea barua jana kumjulisha. Asipoheshimu wito wetu tutamfungulia kesi binafsi ya kuvunja sheria za nchi kutokana na uamuzi wa kufungia gazeti wakati hana mamlaka ya kisheria ya kufanya hivyo… tutamdai fidia ya Sh. 41 milioni kwa kila toleo la gazeti la MwanaHALISI litakalokuwa halikuchapishwa kutokana na amri aliyoitoa,” alisema Kubenea.

Kubenea ambaye pia ni Mbunge wa Ubungo kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), amesema gazeti limefungiwa wakati serikali inajua fika kuna zuio lililotolewa na Mahakama Kuu na kukatiwa rufaa ambayo haijatolewa uamuzi.

Septemba mwaka 2015, Mahakama Kuu Dar es Salaam, kupitia Jaji Salvatory Bongole, ilifuta amri ya Waziri wa Habari (alikuwa Dk. Fennela Mkangara) haikuwa halali kisheria hasa kwa kuwa waziri hakutoa nafasi kwa gazeti hilo kujitetea.

Ndani ya hukumu, Jaji Bongole – ambaye aliridhia ombi la MwanaHALISI kuomba amri nyinginezo zozote zinazofaa baada ya uamuzi – aliamuru waziri aache kufungia gazeti hilo na asiingilie shughuli za uzalishaji wa gazeti hilo.

Baada ya maamuzi hayo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Waziri wa Habari walikata rufaa Mahakama ya Rufaa Tanzania wakati Msajili wa Magazeti hakukata rufaa. Rufaa ya mwanasheria mkuu wa serikali pamoja na waziri haijatolewa uamuzi.

“Mpaka uamuzi wa rufaa utakapotolewa, amri zilizotolewa zinaendelea kuwa halali kisheria. Sasa gazeti linafungiwa wakati amri za mahakama zinafanya kazi… ndo maana tunasema naibu waziri amekiuka amri ya mahakama. Tunamtaka afute amri yake ya kufungia gazeti, si hivyo tutamshitaki na tutamdai fidia,” amesema Kubenea.

Kubenea amesema gazeti la MwanaHALISI l imefungiwa kwa sababu limekuwa likichapisha habari za ndani ya serikali ambazo viongozi waliopo hawataki kukosolewa wala kuhojiwa.

Gazeti la MwanaHALISI pamoja na Mseto na MAWIO lililowahi kuchapishwa na HHPL, yamekuwa yakisakamwa kwa msimamo wake imara wa kukataa kuandika yale yanayowafurahisha wakubwa katika serikali, alisema.

“Watu hawa wanaokataa hata maneno yao wenyewe tena mengine wakiwa wameyatoa hadharani, wanataka kutufumba mdomo tusieleze wananchi mambo yanayohusu viongozi wao na vile nchi inavyoendeshwa,” alisema.

Katika mkutano na waandishi wa habari, Mhariri wa MwanaHALISI, Jabir Idrissa, alisoma sehemu ya taarifa ya maelezo ya ufafanuzi kuhusu madai aliyoyatoa naibu waziri wa habari katika barua yake ya kufungia gazeti pamoja na yale ya

Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo, Dk. Hassan Abbasi aliyoyatoa siku alipokutana na waandishi wa habari kutangaza kufungia gazeti la MwanaHALISI.

Jabir amesema amesikitishwa na kauli kwamba MwanaHALISI wamekuwa wakitunga habari zao nyingi na kusababisha uchochezi na upotoshaji.

Amesema hayo ndio madai ya kutunga kwa kuwa hayaendani na ukweli unaohusu kazi nzuri na kiuwajibikaji inayofanywa na watendaji wa magazeti yaliyo chini ya HHPL.

Taarifa kamili ya Mhariri hii hapa.

TAARIFA MAALUM KWA UMMA

Waheshimiwa Waandishi wa Habari, mtakumbuka kwamba tarehe 19 Septemba 2017, Serikali ilichukua hatua ya kulifungia kuchapishwa kwa MIEZI 24 (Miaka miwili) gazeti la MwanaHALISI, linalomilikiwa na kuchapishwa na kampuni ya Hali Halisi Publishers Ltd (HHPL) iliyosajiliwa kwa mujibu wa Sheria ya Usajili wa Kampuni Tanzania. Hatua hii ilitangazwa mbele ya vyombo vya habari na Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO) ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali, Dk. Hassan Abbasi.

Ofisi yetu ya Hali Halisi Publishers Ltd, baada ya kuzisikia taarifa za uamuzi huo wa serikali kupitia maripota wetu waliokuwa Idara ya Habari ulipofanyika mkutano huo, ilipokea barua ya kutuarifu kuhusu hatua hiyo. Barua yenyewe imeandikwa na kusainiwa na Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Anastazia J. Wambura. Haikuandikwa kwa niaba ya waziri wala hakuna maelezo yanayoonesha kuwa naibu waziri ameelekezwa na waziri kufanya hivyo.

Katika barua hiyo, tumearifiwa kwamba uamuzi wa kulifungia gazeti umefikiwa “… kutokana na kutoridhishwa na utetezi wako uliotolewa kupitia barua yako yenye Kumb. Na. HHPL/04/02/24 ya tarehe 18 Septemba 2017.” Lakini barua ya Naibu Waziri ikaendelea kutoa maelezo kama jitihada za kuhalalisha uamuzi katili wa kulifungia gazeti. Imeelezwa kuwa uamuzi huo unatokana na “mwenendo na mtindo wa kichochezi wa uandishi wa habari na makala katika Gazeti la MwanaHALISI ambao unakiuka kwa kiasi kikubwa misingi ya maadili ya taaluma ya habari.”

Naibu Waziri anaeleza kwamba amefikia uamuzi huo wa kulifungia gazeti la MwanaHALISI baada ya jitihada za muda mrefu za Serikali kujaribu bila ya mafanikio “kulitaka gazeti kuachana na mtindo wake wa sasa ambapo habari nyingi zinazochapishwa katika gazeti ni za uongo, kejeli, upotoshaji, uchochezi na zinazolenga kuwafanya wananchi waichukie Serikali yao au viongozi wao, na kuathiri usalama na ustawi bwa taifa hivyo kukiuka vifungu vya 52 (1)(a), (c), (d) na (e) na 54 (1) vya Sheria ya Huduma za Habari Na. 12 ya mwaka 2016.”

Maelezo ya naibu waziri yanabainisha matukio saba kama kigezo cha kufikiwa kwa uamuzi katili wa kufungia gazeti la MwanaHALISI. Matukio yenyewe yanataja habari na makala zilizochapishwa na MwanaHALISI na kuchukuliwa na Serikali kuwa zimekiuka vifungu vya sheria iliyotajwa. Tutajadili habari moja baada ya nyingine kwa ajili ya kutoa picha halisi itakayowasaidia ndugu zetu waandishi wa habari pamoja na umma kuiona dhamira iliyojaa chuki ya Serikali dhidi ya gazeti la MwanaHALISI.

Kwanza kabisa, tunapendea ieleweke mapema kwamba katika utendaji kazi wetu wa miaka 12 tangu Hali Halisi Publishers Ltd ilipoanzishwa ikianzia na gazeti la MwanaHALISI, wakati huo likitoka kila Jumatano, haijapata kuwa kwamba madhumuni ya kazi yetu ni kutoa habari za uongo, za upotoshaji na za kichochezi na kadhalika za kutunga kama alivyosikika akisema Mkurugenzi wa Idara ya Habari alipokutana nanyi Septemba 19 kutangaza adhabu kwa gazeti letu.

Baadhi yenu ni mashahidi tunaposema kwamba tumekuwa tukichapisha habari za kweli na kweli tupu; habari ambazo mara kadhaa zimedhihirika na kuthibitika kuwa ni za kweli tupu baada ya muda mfupi. Isitoshe habari zetu zimepata kuinua uelewa mpana kwa umma kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu serikali yao na viongozi wao na uhusiano wao na watu wengine walioko nje ya serikali. Habari ambazo tumekuwa tukizichapisha zimesaidia pakubwa kufuta uvumi na kuieleza kweli inavopasa. Ndio kusema kwamba madai ya Mkurugenzi wa Idara ya Habari kuwa nyingi ya habari zetu ni za kutunga au kubuni ni ya upotoshaji yanayodhihirisha chuki iliyopindukia mpaka aliyonayo dhidi ya wamiliki, wachapishaji, wahariri na wafanyakazi wa MwanaHALISI. Kwetu, hayo yake ndio madai ya kutunga, maana sisi tunajivuna kuwa hakuna hata habari moja tuliyoichapisha na ikathibitishwa kuwa ni ya uongo.

Tunapenda kuwaeleza umma wa Watanzania na ulimwengu kwamba kilichofanywa na Serikali katika habari walizozibainisha kama kigezo cha kutuadhibu, ni matokeo ya kufanya TAFSIRI yao binafsi baada ya kutopendezewa na habari hiyo. Wanaichukua habari na kuitafsiri, wakishajiridhisha na wakitakacho, wanatengeneza kosa dhidi yetu na kututaka kujieleza ni kwanini tusichukuliwe hatua za kisheria kwa kuchapisha habari husika. Utamaduni huu ndio tunaouita wa serikali kuwa mlalamikaji kwa kutengeneza kosa, ikajiweka ni mshitaki, jaji, shahidi, mzee wa baraza huku yenyewe ikiwa ina gereza. Mnadhani hapo anayelalamikiwa, au mshitakiwa, ataipata haki?

Zipo habari tulilazimika kukiri makosa. Hata hivyo, isichukuliwe kuwa kukiri kwetu kwa baadhi ya habari walizozihoji, kwa mujibu wa tulivotakiwa kutoa maelezo, kuna maana halisi ya kukiri kukosea kitaaluma. Tunatoa mifano.

Habari iliyokwenda kwa kichwa cha maneno, “Ufisadi ndani ya Ofisi ya JPM.” Hii tuliichapisha Toleo Na. 376, la 30 Januari – 5 Februari, 2017. Ukiisoma habari yenyewe hakuna palipomtuhumu Rais kuhusika na ufisadi uliofanywa. Tuliiweka habari kuonesha kuwa ufisadi umefanyika katika Ofisi ya Rais, ambayo ni ukweli usiobishanika kwamba TAMISEMI ambako Shirika la Elimu Kibaha linawajibika kimajukumu, ipo chini ya Ofisi ya Rais. Hii ni baada ya Rais kufanya mabadiliko kwa kuisogeza ofisi ya TAMISEMI kwenye ofisi yake baada ya mazoea ya kuwa chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Tusaidieni, iko wapi Ofisi ya TAMISEMI sasa? Tulipohojiwa na kwa sababu tulishajua kinachotakiwa na Serikali na hasa Rais mwenyewe, tukalazimika kukiri tumekosea. Hii ni habari iliyotumika kutupa ONYO KALI.

Habari iliyokwenda kwa kichwa cha maneno, “Mwakyembe: Maisha yangu yako hatarini.” Hii ni habari tulioichapisha Toleo Na. 387 la tarehe 17-23 Aprili 2017, ambayo baada ya kuhojiwa tujitetee, tuliomba radhi haraka kama tulivyotakiwa. Lakini, ni habari ya kweli kwa sababu imetokana na maneno aliyoyatoa mwenyewe mbele ya baadhi ya wabunge. Waandishi wa habari waliokuwa ndani ya maeneo ya bunge, akiwemo mwandishi wetu, waliyasikia na kumuuliza ufafanuzi.

Wakati suala hili linakuja, Dk. Mwakyembe alishateuliwa kuwa Waziri wa Habari. Fikiria unapokuwa unatakiwa maelezo na wasaidizi wa Waziri wa Habari, kwa habari ambayo Waziri wa Habari mwenyewe anayehusika nayo, ameikanusha; unatarajia nini kitatokea usipojisalimisha? Na ifahamike hapa kuwa Waziri Dk. Mwakyembe wakati huo tayari alikuwa amefungua kesi dhidi ya MwanaHALISI kuhusu suala jingine. Huyu ni waziri mwenye rungu tayari, usipojisalimisha unataka akupende namna gani? Tuliomba radhi. Baada ya kuomba radhi gazetini, tukapigwa KARIPIO KALI.

Habari iliyokwenda kwa kichwa cha maneno, “Makinikia yakwama.” Ni habari tuliyoichapisha Toleo Na. 407 la tarehe 4-10 Septemba 2017. Tulitakiwa kutoa maelezo ya kujitetea ni kwanini gazeti lisichukuliwe hatua za kisheria. Katika maelezo yetu, tulieleza wazi kuwa maudhui ya habari yanathibitisha ukweli uliopo kwamba hakuna maafikiano yaliyofikiwa katika mazungumzo yaliyofanyika. Wawakilishi wa kampuni ya Barrick Gold inayoendesha mgodi wa dhahabu wa Bulyanhulu na Tulawaka wameondoka nchini na hakukuwa na maelezo ya namna mazungumzo yatakavyoendelezwa. Na katika habari yetu, tumenukuu maelezo ya Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais (Ikulu), Mkurugenzi wa Maelezo, na tukaonesha tulivyomkosa Waziri wa Katiba na Sheria. Wakati tumejiridhisha na maudhui ya habari tuliyoichapisha, tumehisi kuwa headline ndiyo imeleta shida. Tumeomba radhi kwa hili, hatua ambayo haikuwa na maana kuwa tumeandika habari ya uongo.

Matukio yaliyohusu makala iliyochapishwa kwa headline “Mkuu wa Wilaya ya Karagwe anachafua kazi ya Magufuli,” ni kama ilivyo kwa habari iliyosema “Siri Lipumba NEC zafichuka” zimetumika kuhalalisha adhabu dhidi ya MwanaHALISI ilhali bado ziko mikononi zikishughulikiwa baada ya malalamiko kuwasilishwa kwetu kupitia ofisi ya MAELEZO. Ofisi ya Mkurugenzi wa Idara ya Habari inajua fika kuwa inaendelea kupokea hoja za Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi baada ya sisi kutoa maelezo yetu. Na ofisi hiyo inajua vilevile kuwa malalamiko kuhusu habari ya DC wa Karagwe hayajafika mwisho. Inashangaza kuyatumia malalamiko hayo kama kielelezo cha ukorofi wetu na uvunjaji sheria upande wetu. Watendaji wanaoheshimu dhamana yao, hawafanyi kazi kwa kuvizia na kusakama.

Katika mawasiliano tunayoyafanya na ofisi ya MAELEZO, tumebaini kuwa kinachotakiwa baada ya sisi kulalamikiwa, basi ni kukiri tu makosa. Tusipokiri na tukitoa maelezo ya sababu ya kutokiri kwetu kwa hicho kinachodaiwa na ofisi hiyo, huchukuliwa kuwa tumekosea na tunastahili kuadhibiwa. Tunaadhibiwa. Huu hatudhani kama ni utaratibu wa haki hasa kwa kuwa idara ya habari MAELEZO ndiyo inayolalamika. Tumejitahidi kutaka wale wanaolalamika waelekezwe na ofisi hiyo kuwasiliana na sisi lakini Msajili wa Magazeti anashikilia kuwa wanao wajibu wa kusikiliza malalamiko.

Tunajiridhisha kuwa tunayoifanya ni kazi ya uandishi wa habari, wala sio nusu uandishi wa habari kama ilivyodaiwa na Mkurugenzi wa Idara ya Habari. Tunayo makosa ya kiuandishi tunafanya, lakini hurekebisha kila tunapojiridhisha kuwa tumekosa. Hatuamini hata kidogo dhana ya Serikali kuwa kila wanachokiona wao ni kosa, basi kila mtu na hasa sisi tunaotuhumiwa, tuamini kuwa ni kosa tumelitenda. Ndio maana mpaka sasa, tungali tunaamini kuwa njia nzuri ya kufuatwa na Serikali katika hali kama hiyo ya kuendelea kututuhumu kupotosha mambo, ni kuitumia Mahakama kutafuta haki kama vile inavyohimiza wananchi waitumie taasisi hiyo wanapohisi wameonewa au wamenyimwa haki yao wa kati wowote.

Imesomwa leo 27 Septemba 2017, kwa niaba ya HHPL, na Mhariri wa gazeti la MwanaHALISI, JABIR IDRISSA, 0774/0713 226248 au jabir.mzalendo@gmail.com

 

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

BiasharaHabari za Siasa

Zanzibar mbioni kuanza uchimbaji mafuta na gesi baharini

Spread the loveSERIKALI ya Zanzibar, imekamilisha mchakato wa uchimbaji wa mafuta na...

Habari za Siasa

Wizara ya afya yataja mafanikio 10 miaka mitatu Samia madarakani

Spread the loveWIZARA ya Afya imetaja mafanikio 10 iliyoyapata ndani ya miaka...

Habari za Siasa

Mbozi walilia kuwa manispaa, majimbo 3

Spread the loveHALMASHAURI ya wilaya ya Mbozi mkoani Songwe imeeleza dhamira yake...

Habari za Siasa

Wabunge waitaka TPDC kuongeza kasi ya kuunganisha wateja gesi asilia

Spread the love  KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini...

error: Content is protected !!