January 18, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Kubenea atikisa kambi ya Tarimba

Spread the love

MGOMBEA Ubunge wa Kinondoni kupitia ACT-Wazalendo, Saed Kubenea, amefanya kampeni ya nyumba kwa nyumba katika Kata ya Hananasif, Wilaya Kinondoni jijini Dar es Salaam. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam…(endelea).

Kata ya Hananasif ilikuwa inaongozwa na Abbasi Tarimba, ambaye kwa sasa ni Mgombea wa Ubunge wa Kinondoni kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Kubenea aliishambulia kata hiyo jana Alhamisi tarehe 8 Oktoba 2020 ambapo wananchi wengi wa Hananasif walijitokeza kusikiliza sera zake huku yeye amewaahidi kuboresha maisha yao wakimchagua katika Uchaguzi Mkuu wa tarehe 28 Oktoba 2020.

Mwanasiasa huyo, aliwaomba wananchi wa Kata ya Hananasif wamchague kwa kuwa atawaletea maendeleo na wasimchague mtu aliyewahi kuwa diwani wao ambaye hakuwasaidia chochote.

“Mgombea ubunge wa sasa hivi aliyekuwa diwani wa Hananasifu (Tarimba) kulikuwa na mikataba miwili tata ya ujenzi wa shule kutokana na udanganyifu wa gharama za ujenzi huo,” alisema Kubenea.

“Abbasi Tarimba alikuwa kiongozi wa Klabu ya Yanga leo anatembea anasema ataleta maendeleo Kinondoni. Yaani ameshindwa kuiongoza Yanga ikawa ombaomba ataweza kuongoza wananchi wote wa Kinondoni,” alihoji Kubenea

Kubenea aliwaomba wananchi hao kutochagua wagombea wa CCM kwa maelezo chama hicho kilichangia ugumu wa maisha yao kwa kusitisha utoaji wa mikopo ya kina mama, watu wenye ulemavu inayopaswa kutolewa na Halmashauri.

https://youtu.be/bLXQ7wWRcPo

 

Alisema, wakati Halmashauri ya Kinondoni ilipochukuliwa na vyama vya upinzani, ilikuwa inatoa mikopo kwa wananchi lakini tangu iliporudi mikononi mwa CCM mikopo hiyo ilisitishwa.

“Tulipokuja tukakuta mikopo ya kina mama na vijana haitolewi lakini tulipofika tukatoa, tulipoondoka mwaka 2017 halmashauri ya Ubungo ilipoundwa CCM walifanya vurugu hakuna mkopo hata sumni iliyotolewa Kinondoni,” alisema Kubenea.

Wakati huo huo, Kubenea aliwanadi wagombea Udiwani wa Hananasif, Kimbita Eliakimu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na Kessy Midole wa ACT-Wazalendo.

Kubenea aliwaomba wananchi wa kata hiyo wamchague mgombea mmoja wanayemuona anafaa.

“Ninajua Hananasif sisi tuna mgombea udiwani, lakini yuko wa Chadema Kimbita anayemaliza muda wake, sisi kwenye vyama vyetu viwili, tunaendelea na majadiliano ya kuachiana kata na jimbo.”

“Mwisho wa siku tutawaeleza nani mgombea wetu, tukiona Kimbita anafaa tutampigia kampeni kama wa kwetu anafaa tutamchagua,” alisema Kubenea.

error: Content is protected !!