Friday , 29 March 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Kubenea atamba kuitwaa Kinondoni
Habari za Siasa

Kubenea atamba kuitwaa Kinondoni

Saed Kubenea
Spread the love

ALIYEKUWA mbunge wa Ubungo, kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Saed Kubenea, amejigamba kushinda kinyang’anyiro cha ubunge katika jimbo la Kinondoni. Anaripoti Hamis Mguta, Dar es Salaam … (endelea).

Kubenea ambaye sasa anawania kiti hicho kupitia Chama cha ACT-Wazalendo, amewaambia waandishi wa habari, jijini Dar es Salaam, kuwa “nimekuja Kinondoni kushinda, na siyo kusindikiza.”

Alitoa kauli hiyo, muda mfupi baada ya Msimamizi Msadizi wa uchaguzi katika jimbo la Kinondoni, Aron Kagurumjuli, kumtangaza mwanasiasa huyo machachari kuwa mmoja wa wagombea ubunge katika jimbo hilo.

“Ninashukuru Mungu nimeteuliwa kuwa mgombea. Ninaamini kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu, nitashinda uchaguzi huu,” ameeleza Kubenea, mbele ya mamia ya wafuasi wake.

Akijibu swali la waandishi wa habari, kwamba kwa vipi anajihakikishia ushindi wakati amejitosa kwenye kinyang’anyiro hicho, huku wapinzani wakiwa wamegawanyika, Kubenea amesema, bado kuna nafasi ya vyama kushirikiana.

Amesema, “licha ya wagombea kuteuliwa, sheria inaruhusu wagombea kujiengua ndani ya siku 21 kabla ya siku ya uchaguzi. Hivyo basi, ni imani yangu kuwa tutaweza kushirikiana.”

Hata hivyo, Kubenea amesema, hata kama vyama hivyo havitashirikiana, amejiandaa kuucheza mziki huo peke yake, “ingawa napenda tuungane ili tushinde kiurahisi.”

Anasema, “malengo yetu siyo kushinda majimbo. Malengo yetu ni kushinda hadi urais. Hivyo kuna umuhimu wa kushirikiana ili  tuongeze majimbo kutoka sita tuliyopata mwaka 2015 hadi 10 na hiyo ndio dhamira yangu.”

Akizungumzia kampeni za uchaguzi huo, Kubenea amesema, “ni matumaini yangu kwamba watakaobahatika kupita kwenye uteuzi watafanya kampeni kistaarabu, wataeleza wananchi kile wanatarajia kuwafanyia. Mimi Kinondoni ni mgombea ninayegombea nikitokea jimboni (Ubungo). Ninalo la kuwambia wananchi.”

Akitaja vipaumbele vyake endapo atafanikiwa kushinda uchaguzi huo, Kubenea amesema, “kipaumbele changu cha kwanza, ni kutafuta suluhu ya mafuriko na miundombinu ya maji taka.

“Nimewatumikia wananchi wa Ubungo, kwa miaka mitano mfululizo. Nimemaliza mkataba wao, nimekuja Kinondoni nyumbani kwangu, ninakoishi na kufanya shuguli zangu kwa muda wa miaka 16 sasa. Nayafahamu matatizo ya Kinondoni, kwa kuwa nami ni sehemu ya matatizo hayo. Nikifanikiwa kuwa mbunge nitafanya yale ambayo wenzangu wameshindwa,” amesisitiza.

Katika uchaguzi huo, Kubenea atachuana na Abbasi Gulamhussen Tarimba, ambaye anagombea nafasi hiyo kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM); Mustafa Murro, anayegombea kupitia chama cha NCCR-Mageuzi na Susan Lyimo, anayewania kiti hicho, kupitia Chadema.

Wagombea hao wamekwisharudisha fomu zao za uteuzi pamoja na wa vyama vingine wamaogombea jimbo hilo.

Zoezi la urudishaji fomu linafungwa rasmi leo saa 10 jioni. Kesho tarehe 26 Agosti 2020 kampeni zitafunguliwa rasmi hadi tarehe 27 Oktoba 2020.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Nani anasema kuna hasara ATCL?

Spread the loveRIPOTI za makusanyo na matumizi ya fedha katika Kampuni ya...

Habari za SiasaTangulizi

CAG: Wastaafu, wenza wao chanzo NHIF kufilisika

Spread the loveRIPOTI ya ukaguzi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu...

Habari za SiasaTangulizi

Vikundi hewa 851 vyalamba bilioni 2.6 mikopo ya halmashauri

Spread the loveVIKUNDI hewa vya wajasirimali wadogo 851 kutoka katika halmashauri 19...

Habari za SiasaTangulizi

Mashirika matano yapata hasara mabilioni ya fedha

Spread the loveMASHIRIKA matano ya Serikali yanayojiendesha kibiashara, yamepata hasara ya mabilioni...

error: Content is protected !!