Friday , 19 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Kodi zilizofutwa, ongezwa Bajeti 2020/21 
Habari za SiasaTangulizi

Kodi zilizofutwa, ongezwa Bajeti 2020/21 

Dk. Phillip Mpango, Waziri wa Fedha na MIpango Tanzania
Spread the love

WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango amewasilisha Bungeni Bajeti ya Serikali ya Tanzania ya mwaka 2020/21 ya Sh. 34.87 Trilioni. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).

Kati ya fedha hizo, Sh. 22.1 trilioni ni za matumizi ya kawaida na Sh. 12. 77 Trilioni za maendeleo.

Dk. Mpango amewasilisha Bajeti hiyo leo Alhamisi tarehe 11 Juni 2020 jijini Dodoma, ikiwa ni bajeti ya tano ya utawala wa Rais John Magufuli aliyeingia madarakani tarehe 5 Novemba 2015.

Akiwasilisha bajeti hiyo,  amesema, anapendekeza kufanya marekebisho ya mfumo wa kodi, ikiwemo baadhi ya viwango vya kodi, tozo na ada zinazotozwa chini ya Sheria mbalimbali na kurekebisha taratibu za ukusanyaji na usimamiaji wa mapato ya Serikali.

Amesema, marekebisho haya yamezingatia dhamira ya Serikali ya kuendelea kuwa na mfumo wa kodi ambao ni tulivu na wa kutabirika.

Dk. Mpango amesema, marekebisho yanalenga kuchochea kasi ya ukuaji wa uchumi hususan katika sekta ya kilimo na viwanda, kuongeza kipato kwa waajiriwa na kuongeza mapato ya Serikali.

“Vile vile, maboresho haya yamezingatia uhitaji wa kuwekeza nguvu katika kuongeza upatikanaji wa vifaa tiba na dawa,” amesema

Dk. Mpango amesema, Serikali pia inaendelea kutekeleza Mpango wa Kuboresha Mazingira ya Kufanya Biashara (BluePrint) ulioidhinishwa mwaka 2017/18 kwa kupitia mfumo wa tozo na ada mbalimbali zinazotozwa na Wizara na Mamlaka za Udhibiti kwa lengo la kupunguza au kuzifuta baadhi ya tozo na ada hizi.

Waziri huyo amesema, hadi sasa, jumla ya tozo na ada 114 zimefutwa.

Dk. Mpango anasema, anapendekeza, kusamehe Kodi ya Ongezeko la Thamani kwenye bima ya kilimo cha mazao.

“Lengo la hatua hii ni kupunguza gharama na kutoa unafuu katika bima za kilimo ili kuwawezesha wakulima kuziwekea bima shughuli za kilimo na kuvutia wananchi kutumia huduma za bima kwa ajili ya kujikinga na majanga mbalimbali yanayoathiri shughuli zao za kilimo mfano ukame, mafuriko.”

“Kufanya marekebisho ya kuwawezesha wauzaji wa bidhaa ghafi nje ya nchi kuendelea kujirudishia Kodi ya Ongezeko la Thamani iliyolipwa kwenye gharama za huduma au bidhaa katika shughuli hizo ili bidhaa hizo ziweze kushindana katika masoko ya nje,” amesema.

Dk. Mpango amesema, “Hatua hii pia inalenga kuendana na msingi wa utozaji VAT kwa kuzingatia mahali bidhaa inapotumika (destination principle).”

Amesema, hatua zote za Kodi ya Ongezeko la Thamani kwa ujumla wake zinatarajiwa kupunguza mapato ya Serikali kwa kiasi cha Sh. 46 milioni.

Dk. Mpango amesema, anapendekeza “kupandisha kiwango cha mapato ya waajiriwa ili kuongeza kiwango cha mapato yasiyotozwa kodi (threshold) kutoka Sh. 170,000 kwa mwezi hadi Sh. 270,000 kwa mwezi (sawa na kutoka Sh. 2,040,000 kwa mwaka hadi Sh. 3,240,000) na kubadilisha makundi mengine.”

“Hatua hii pekee inatarajiwa kupunguza mapato kwa Sh. 517.2 milioni,” amesema.

Waziri huyo amependekeza, kuongeza kiwango cha Mapato ghafi ya Vyama vya Ushirika vya Msingi yasiyotakiwa kutozwa Kodi ya Mapato kutoka Sh. 50 milioni hadi Sh.100 milioni kwa mwaka.”

“Lengo la hatua hii ni kutoa nafuu ya kulipa Kodi ya Mapato kwa Vyama vya Ushirika vya Msingi zikiwemo SACCOS kutokana na kuwa na mitaji midogo ili kuwanufaisha wanachama wake kwa njia ya gawio na mikopo,” amesema.

 

Huku akishangiliwa, Dk. Mpango amesema anapendekeza,Kufuta msamaha wa Kodi ya Mapato kwa wazalishaji walio ndani ya maeneo maalum ya kiuchumi (Special Economic Zones) wanaozalisha bidhaa na kuuza ndani ya nchi kwa asilimia 100.”

“Hatua hii inalenga kuweka usawa katika utozaji wa kodi ya mapato baina ya wazalishaji wa bidhaa walio nje na walio ndani ya maeneo maalum ya kiuchumi,” amesema.

Amesema, kuruhusu michango ya wadau kwenye Mfuko wa Ukimwi isitozwe kodi ya Mapato (allowable deduction).

“Aidha, napendekeza pia michango iliyotolewa na wananchi kwa Serikali na itakayoendelea kutolewa katika kipindi hiki cha mapambano dhidi ya ugonjwa wa Homa Kali ya Mapafu (COVID 19) isitozwe kodi hadi hapo Serikali itakapotangaza kuisha kwa ugonjwa huu,” amesema

Dk. Mpango amesema, “Lengo la mabadiliko haya ni kuhamasisha uchangiaji wa hiari katika Mfuko wa Ukimwi na kwa Serikali ili kuongeza nguvu katika mapambano dhidi ya Ugonjwa wa Ukimwi na COVID 19.”

Kumpa Mamlaka Waziri wa Fedha kutoa msamaha wa kodi ya mapato kwenye miradi ya kimkakati yenye jumla ya kodi ya mapato isiyozidi Sh.1 bilioni kwa kipindi chote cha mradi  bila kuwasilisha mapendekezo hayo kwenye Baraza la Mawaziri.

“Lengo la hatua hii ni kuwezesha miradi yenye kiwango kidogo cha kodi ya mapato kutekelezwa kwa haraka. Waziri mwenye dhamana ya fedha atafanya mashauriano na Mamlaka ya Mapato kabla ya kutoa msamaha wa kodi husika,” amesema

Dk. Mpango amependekeza kutoza Kodi ya Ongezeko la Thamani ya Mtaji (Capital Gains) kwenye mapato yatokanayo na ubadilishaji wa leseni (concessional right) katika ardhi iliyohodhiwa (reserved land) na kupangishwa kwa mwekezaji mwingine.

Amesema, lengo la hatua hii ni kupanua wigo wa kodi na kuongeza mapato ya Serikali.

Dk. Mpango amependekeza, kutoza kodi ya zuio ya asilimia 10 kwenye malipo ya uwakala inayolipwa kwa mawakala wa Benki kama ilivyo kwa mawakala wa huduma za uhamishaji fedha za kieletroniki.

“Lengo la hatua hii ni kuweka usawa katika utozaji wa kodi ya mapato kwa watoa huduma za kibenki, kielektroniki na huduma za usafirishaji fedha kwa njia ya mitandao ya simu,” amesema

Ushuru wa Bidhaa

Waziri huyo amesema, anapendekeza, kutoza ushuru wa Bidhaa kwenye bia za unga (powdered beer) zinazotambulika kwa HS Code 2106.90.99 kwa kiwango cha Sh. 844 kwa kilo ya bia ya unga inayoagizwa kutoka nje ya nchi.

Amesema, lengo la mabadiliko haya ni kupanua wigo wa kodi kwa kuwa bidhaa hizi kwa sasa zinaagizwa toka nje ya nchi.

Dk. Mpango amependekeza, kutoza Ushuru wa Bidhaa kwenye juisi ya unga zinazotambulika kwa HS Code 2106.90.99 kwa kiwango cha shilingi 232/= kwa kilo ya juisi ya unga inayoagizwa kutoka nje ya nchi.

Amesema, lengo la mabadiliko haya ni kupanua wigo wa kodi kwa kuwa bidhaa hizi kwa sasa zinaagizwa toka nje ya nchi.

“Hatua za kutoza ushuru wa bidhaa kwenye bidhaa zisizo za petroli kwa ujumla wake zinatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha Sh. 45.8 bilioni,” amesema.

Dk. Mpango amependekeza kufanya maboresho kwenye Sheria ya Usimamizi wa Kodi Sura 438, ili kumwezesha Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania kutatua mapingamizi ya kodi kwa ufanisi na haraka.

Amesema, marekebisho haya ni pamoja na kuweka ukomo wa muda wa siku 30 za kuwasilisha nyaraka zitakazotumika kwenye utatuzi wa pingamizi.

Amesema, Aidha marekebisho haya yataweka ukomo wa miezi sita kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania kufanya maamuzi ya mapingamizi ya kodi.

“Kwa sasa, sheria haitoi ukomo kwa walipakodi kuwasilisha nyaraka zitazoisaidia Mamlaka ya Mapato kufanya uamuzi kuhusu pingamizi. Vile vile, kwa sasa sheria haitoi muda wa ukomo kwa Kamishna Mkuu kwa Mamlaka ya Mapato kufanya uamuzi kuhusu pingamizi,” amesema

Magari

Dk. Mpango amependekeza kufanya marekebisho kwenye Sheria ya Usajili wa Magari Sura 124, ili kuanzisha usajili wa magari kwa kutumia namba maalum (mfano T. 777 DDD) kwa ada ya Sh. 500,000.

“Ili kuwezesha wateja kuchagua namba ya usajili wa gari katika namba zilizopo katika regista ya namba za magari katika muda husika. Hatua hizi za marekebisho ya Sheria ya Usajili wa Magari inatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha Sh.200 milioni,” amesema

Pia, Dk. Mpango amependekeza kufanya marekebisho kwenye Sheria ya Madini, Sura 123 ili kuweka vipengele vinavyomtaka mwombaji wa leseni au anayetaka kuhuisha leseni za uchimbaji madini kuwa na Namba ya Utambulisho wa Mlipakodi na Cheti cha Kodi (Tax Clearance) kutoka Mamlaka ya Mapato. Lengo la hatua hii ni kuchochea uwajibikaji wa hiari.

“Napendekeza kupunguza kiwango cha tozo kwa ajili ya maendeleo ya ufundi stadi (Skills Development Levy) kutoka asilimia 4.5 hadi asilimia 4.”

“Lengo la marekebeisho haya ni kuwapunguzia waajiri mzigo na gharama za uendeshaji wa shughuli zao na kutimiza azma ya kupunguza tozo hizi hatua kwa hatua bila kuathiri mapato kwa kiasi kikubwa,” amesema.

Dk. Mpango amependekeza kufanya marekebisho kwenye Sheria ya Posta na Mawasiliano ya Kielektroniki Sura 306 ili kuziondoa kampuni zinazomilikiwa na Serikali na ambazo Serikali inamiliki hisa asilimia 25 na zaidi katika takwa la kuorodheshwa kwenye soko la hisa.

Amesema, hatua hii inalenga kutokusababisha kupungua kwa hisa zinazomilikiwa na Serikali baada ya Kampuni kuorodheshwa kwenye soko la hisa.

“Aidha, napendekeza kuondoa kampuni zinazokodisha minara ya mawasiliano zisiwe sehemu ya makampuni ya mawasiliano zinazotakiwa kuorodheshwa kwenye soko la hisa,” amesema. 

Endelea kufuatilia MwanaHalisi Online & MwanaHALISI TV kwa habari zaidi

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

BiasharaHabari za Siasa

Mavunde aagiza Perseus kuharakisha fidia Sengerema

Spread the loveWaziri wa Madini, Anthony Mavunde ameipongeza Kampuni ya Perseus kwa...

Habari za Siasa

Kigogo Chadema awanyooshea vidole vigogo serikalini kuhusu ripoti ya CAG

Spread the love  MWANACHAMA wa Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Boniface Jacob, amedai...

Habari za Siasa

Wabunge waikalia kooni TAKUKURU Bungeni

Spread the love  BAADHI ya wabunge wamelia na changamoto za utendaji wa...

Habari za SiasaTangulizi

Mpina ataka Waziri Majaliwa ajiuzulu, akosoa teuzi za mawaziri

Spread the love  MBUNGE wa Kisesa, Luhaga Mpina, amemtaka Waziri Mkuu, Kassim...

error: Content is protected !!