Thursday , 28 March 2024
Home Habari Mchanganyiko Kifo cha Dilunga chashtua tasnia ya habari, serikali
Habari Mchanganyiko

Kifo cha Dilunga chashtua tasnia ya habari, serikali

Spread the love

KIFO cha Godfrey Dilunga, mwandishi wa habari za mtafiti, mhariri na mchokonozi, kimeumiza tasnia nzima ya habari na kada zingine nchini. Anaripoti Regina Mkonde…(endelea).

Dilunga ambaye ambaye alikuwa akifanya kazi kwenye gazeti la JAMHURI la Kampuni ya Jamhuri Media, amefariki alfajiri ya leo tarehe 17 Septemba 2019 katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH).

Deodatus Balile, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Jamhuri Media, amesema Dilunga amepoteza maisha MNH alikokuwa akipatiwa matibabu, kutokana na kusumbuliwa na maradhi ya tumbo tangu tarehe 9 Septemba 2019.

“Nasikitika kutangaza kifo cha Mhariri wa gazeti la Jamhuri, Godfrey Dilunga kilichotokea alfajiri ya tarehe 17 Septemba 2019 katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, alikuwa akisumbuliwa na maradhi ya tumbo. Bwana ametoa, Bwana ametwaa jina lake lihimidiwe,” inaeleza taarifa ya Balile.

Taarifa hiyo inaeleza kuwa, familia ya marehemu Dilunga na Kampuni ya Jamhuri Media Limited, inaandaa taratibu za kuuaga, kisha mwili wake kupumzishwa mkoani Morogoro, mahala alikozaliwa.

“Msiba uko Kimara Stop Over kwa dada yake Dilunga, mwili utasafirishwa kwenda Morogoro Kesho Septemba 18, 2019. Tunaandaa taratibu za kuaga mwili hapa Dar es Salaam, na maziko yanatarajiwa kufanyika Morogoro katika siku itakayotangazwa na familia,” inaeleza taarifa ya Balile.

Marehemu Dilunga alilazwa MNH tarehe 9 Septemba 2019 akitokea Hospitali ya Mwananyamala kwa rufaa kutokana na tatizo la maumivu ya tumbo.

Kabla ya kuhamia Jamhuri, Dilunga amepata kufanya kazi kwenye magazeti mbalimbali ikiwemo ya hivi karibuni Raia Mwema na Mtanzania.

Serikali na vyama vya siasa katika nyakati tofauti, imetuma salamu za rambirambi kufuatia kifo hicho.

Dk. Hassan Abbasi, Msemaji Mkuu wa Serikali, kupitia ukurasa wake wa Twitter amesema amepokea kwa amsikitiko kifo cha mwanahabari huyo.

“Kwa niaba ya Serikali nimepokea kwa masikitiko kifo cha mwanahabari Godfrey Dilunga. Nilimfahamu Dilunga kuwa mmoja wa wanahabari vijana lakini aliyeipenda sana kazi yake na alijituma kuifanya kwa ukamilifu. Mungu ampe pumziko la amani na la milele,” ameandika Dk. Abbasi.

Zitto Kabwe, Kiongozi Mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo kupitia ukurasa wake wa Twitter ametuma salamu za pole kwa familia, na wadau wa tasnia ya habari hapa nchini.

“Godfrey Dilunga, Mhariri wa gazeti la Jamhuri na kwa muda mrefu sana Mhariri Mkuu wa gazeti la Raiamwema ametangulia mbele ya haki. Salaam zangu za pole kwa familia yake, Jukwaa la Wahariri na waandishi wote nchini. Mmoja wa wahariri mahiri kabisa wa magazeti katika Nchi yetu,” ameandika Zitto.

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kupitia Freeman Mbowe, Mwenyekiti wake Taifa, kimeeleza kusikitishwa na kifo cha Dilunga, na kueleza kwamba kitaendelea kuukumbuka mchango wake katika chama hicho.

“Nimepokea kwa huzuni na masikitiko makubwa taarifa za msiba huu. Tumefanya kazi na Dilunga kwa ukaribu sana. Kimsingi alikuwa mmoja wa waandishi wa habari kwenye timu ya waandishi wa habari kutoka vyombo vya habari vya kitaifa na kimataifa tuliozunguka nao nchi nzima kuanzia mwaka 2000. Pumzika kwa amani Dilunga,” inaeleza taarifa ya Mbowe.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Kapinga kuongoza usambazaji wa mitungi ya gesi 10,000 ya Taifa Gas

Spread the loveNaibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga ameahidi kuongoza kwa ufanisi...

BiasharaHabari Mchanganyiko

Wafanyabiashara, wawekezaji China waridhia kuwekeza bil. 800 katika sekta 5 nchini

Spread the loveUJUMBE wa wafanyabiashara na wawekezaji wakubwa kutoka Jimbo la Changzhou...

Habari Mchanganyiko

Bil. 4.42 kumaliza uhaba maji kata 2 Musoma Vijijini

Spread the loveWANANCHI wa kata za Busambara na Kiriba, Jimbo la Musoma...

BiasharaHabari Mchanganyiko

Soko nepi za watoto lashuka, watu wazima lapaa

Spread the loveKiwanda cha kutengeneza nepi cha Japan kimetangaza kuwa kitaacha kutengeneza...

error: Content is protected !!