GODLUCK Mlinga, Mbunge wa Ulanga (CCM) amesema kuwa, Wilaya ya Ulanga inaongoza kwa kuwa na wagonjwa wa kifafa Tanzania na duniani. Anaripoti Danson Kaijage, Dodoma … (endelea).
Mlinga ametoa kauli hiyo leo bungeni wakati akiuliza swali la nyongeza. Alitaka kujua, ni lini serikali itaweza kutoa dawa za kutosha kwa wagonjwa wa kifafa katika wilaya hiyo iliyopo kwenye Mkoa wa Morogoro?
“Kwa kuwa Wilaya ya Ulanga ni kinara wa ugonjwa wa kifafa duniani, na kwa kuwa kifafa kinaendana na ugonjwa wa akili, na wagonjwa wa kifafa wanaweza kuanguka muda wowote katika maji au kwenye moto. Je, ni lini serikali itaweza kutoa dawa za kutosha kwa watu wenye ugonjwa huo,” amehoji Mlinga.
Awali katika swali la msingi Edward Mwalongo, Mbunge wa Njombe Mjini (CCM) alitaka kujua, serikali inawahudumiaje wagonjwa wa akili wanaozurura mitaani hasa katika masuala ya matibabu, mavazi na makazi.
Akijibu maswali hayo Dk. Faustine Ndugulile, Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto amekiri kwamba, Ulanga kuna tatizo la kifafa pia kiasi cha dawa zinapelekwa eneo hilo.
Kuhusiana na wagonjwa wanaorandaranda, Dk. Ngugulile amesema, kwa mujibu wa sheria ya afya ya akili ya mwaka 2008, inawataka ndugu na jamii kuibua wagonjwa wa akili na kuwapeleka kwenye vituo vya kutolea huduma.
“Wagonjwa wakishapata nafuu, huruhusiwa kwenda kukaa na familia zao na kwenye jamii wanazotoka. Jukumu la kwanza la kulinda afya huanzia katika ngazi ya familia lakini jamii zetu zimekuwa zikiwanyanyapaa, kuwabagua na kuwatenga wagonjwa wa akili,”amesema.
Amesema, kwa mujibu wa sheria ya afya ya akili ya mwaka 2008, sehemu ya tatu kifungu cha sheria namba 9 kifungu kidogo 1-3 imeeleza wazi kuwa, ofisa wa polisi, ofisa usalama na ofisa ustawi wa jamii ngazi ya wilaya, wana jukumu la kubainisha mtu yeyote anayerandaranda kwa kutishia amani.
Leave a comment