Tuesday , 19 March 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Kibatala amhenyesha ‘mbaya wa Zitto’  
Habari za SiasaTangulizi

Kibatala amhenyesha ‘mbaya wa Zitto’  

Spread the love

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam, imeanza kusikiliza ushahidi kwenye kesi ya uchochezi inayomkabili Zitto Kabwe, Kiongozi Mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo. Anaripoti Faki Sosi …(endelea).

Leo tarehe 23 Aprili 2019, upande wa mashtaka katika kesi hiyo, umeweza kumleta shahidi wake wa kwanza, mkuu wa upelezi mkoa wa Kipolisi, Kinondoni, SSP John Malulu.

Mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Huruma Shahidi, Wakili wa serikali, Nassoro Katuga, alimuongoza shahidi aliyetoa ushahidi wake chini ya kiapo na kuieleza mahakama kuwa alimuona Zitto akitoa maneno ya uchochezi.

Alisema, “tarehe 28 Oktoba 2018, niliona video kwenye mtandao wa Youtube iliyokuwa ikionyesha mkutano (press conference), kati ya Zitto na wandishi wa habari.

Shahidi huyo ameieleza mahakama kuwa hakutilia maanani video hiyo isipokuwa siku ya pili yake ya tarehe 29 Oktoba 2018, akiwa kwenye majukumu yake, akielekea kitoa cha polisi cha Gogoni, kilichopo Kimara, ndipo alipoona kundi kubwa la watu ambalo  lilimfanya avutiwe nalo; na kwamba aliamua kushuka ili kujua kinachoendelea.

Wakati huo, Malulu anasema, alikuwa akitokea Osterbay na alikuwa ameshika eneo la Manzese.

“Kwa kuwa nilikuwa nimevaa kiraia, niliamua kushuka ili watu wasinijue. Niliwasogelea ili kusikia kile wanachokizungumza. Watu wale, walikuwa wakizungumzia press release (taarifa kwa vyombo vya habari), iliyotolewa na Zitto juu ya kile alichodai kuwa jeshi la polisi ni la kinyama limefanya mauaji kwa raia,” ameeleza.

Amesema, “watu wale walikuwa wanahasira na kuzungumza kwa jazba na kuonyesha kuchukizwa na kile walichokisikia kuwa jeshi la polisi linafanya matendo ya kinyama.”

Amedai kuwa alimvuta mmoja wa watu waliokuwepo kwenye kundi lile ambaye alimtaja kwa jina la Shabani Hamis. Anasema, alirejea maneno yaleyale kuwa jeshi la polisi limetenda mambo ya kinyama na limewatoa watu hospitali kisha kuwauwa.

Anasema, aliamua kuendelea na safari yake ambapo alipofika eneo la Kimara Korogwe, alishuhudia kundi jingine la watu 15 na zaidi wakijadili masuala hay ohayo. Anasema watu hao, walionekana wamekasirishwa na yale waliyoyasikia kwenye taarifa ya Zitto.

Anasema, alizungumza na mmoja wa watu walikuwepo eneo hilo.

“Hawa walikuwa wanamoto kweli kweli, nao walikuwa wakisema jeshi la polisi ni la kinyama, napo nilipata taarifa za mtu mmoja aliyekuwepo hapo,” ameeleza shahidi huyo wa serikali.

Wakili Katuga ameomba kulitaja jina la mtu huyo ambapo shahidi aliomba kujikumbusha kwenye kitabu chake cha kumbukumbu.

Kufuatia hali hiyo, wakili wa utetezi, Peter Kibatala, alirejea kifungu cha 172 ushahidi, kinachoeleza kuwa upande wa utetezi wanahaki ya kuona kilichopo kwenye kitabu hicho.

Mahakama ikaridhia upande wa utetezi kupitia kitabu hicho; na kisha shahidi akaendelea na kumtaja mtu huyo kuwa ni Mashaka Juma.

Amesema, “nilirejea ofisini na kuchukua juu ya nilichokisikia kwa yale niliyoyasikia kwenye makundi haya mawili.”

Anasema, aliporejea ofisini kwake aliwaita makachelo na askari wengine wanaoshughulikia makosa ya mtandaoni – Cyber Crime – ili kuanza kufuatialia na baadaye kuwasiliana na askari mwenye cheo kama chake mkoani Kigoma, SSP Martin Gerlad ili kufahamu ukweli wa kile ambacho Zitto amekieleza.

Anasema, SSP Gerlad alikana madai ya Zitto na kuongeza kuwa watu waliotajwa na mwanasiasa huyo kufariki, bado wako hai na wamefunguliwa mashtaka.

Baada ya kumaliza kutoa ushahidi wake, ndipo sasa ukaja wakati wa wakili Kibala kumhoji na kufanya mapitio maelezo ya shahidi huyo wa serikali.

Mahojiano kati ya Kibatala na shahidi huyo yalikuwa kama ifuatavyo:

Kibatala: Shahidi mimi napenda kujua elimu ya mtu ninayezungumza naye ili kujua nazungumza na mtu wa aina gani. Je, una elimu ya kiwango gani?

Shahidi: Darasa la Saba.

Kibatala: Darasa la saba umemaliza mwaka gani, na ulipata ufaulu gani na ulisoma shule gani na mkoa gani?

Shahidi: Ufaulu wangu ni mkubwa.

Kibatala: Mwaka gani.

Shahidi: Miaka ya 90.

Kibatala: Ofisa Mwandamizi wa jeshi la polisi hukumbuki ni mwaka gani ulimaliza shule?

Shahidi: Mwaka 1990.

Kibatala: Shahidi nijibu, nakuuliza ufaulu wako na shule uliyosomea inaitajwe?

Shahidi: Shule ya msingi Kinangu, mkoani Mwanza. Suala la ufaulu wangu hauusiani na ushahidi ninaoutoa mahakamani hapa.

Wakili Katuga akasimama na kueleza mahakama kuwa  “…mheshimiwa Hakimu, tunaiomba mahakama yako itupe muongozo. Wakili anamuuliza shahidi maswali ambayo hayahusiani na shauri hili.” Hakim Shahidi akaruhusu Kibatala kuendelea na mahojiano na SSP Malulu.

Kibatala: Ni sahihi PGO (kitabu cha mwongozo kwa jeshi la polisi), kuwa ndio kinachokuongoza kwenye shuhuli zake.

Shahidi: PGO na sheria.

Kibatala: Ni sahihi kuwa uchunguzi wowote wa kosa la jinai, unaanzishwa na taarifa inayotolewa na mtu kwenye kituo cha polisi?

Shahidi: Sio kila mara.

Kibatala: Mchakato huu umeanzishwa na taarifa kipolisi?

Shahidi: Kimya.

Kibatala: Nakala ya maelezo tulipewa na wakili wa serikali umeeleze hakimu kuwa hayo ni maelezo yako na tunapewa kwa mujibu wa sharia?

Shahidi: Haya maelezo yangu.

Kibatala: Nakutaka uyatoe mahakamani kama kielelezo cha utetezi Mahakamani.

Wakili Katuga: Kielelezo hakitoki kama gazeti tena anayomwambia aitoe ni nakala tu. Kwa nini anataka kutolewa kwa maelezo yasiyokuwa na kiapo mahakamani. Tufuate misingi ya kisheria.

Hakimu Sahidi: Kibatala ungeendelea na cross-examination (kuyapitia malezo ya shahidi na kuuliza maswali) na tuone kama kuna sababu ya kutaka yatolewe hayo maelezo.

Kibatala: Mahakama ijielekeze kwenye uamuzi wa Abdallah Zombe, juu kutolewa kwa maelezo aliyoyakubali shahidi kuwa ni maelezo yake.

Kibatala: Shahidi ananisemesha chinichini, ananiambia nimechemsha; ilhali anajua kuwa yeye hatakiwi kunisemesha zaidi ya kujibu maswali yangu.

Kibatala: Naomba usome juu haya maelezo ya majina yako.

Shahidi: Kungu John

Kibatala: Lakini chini ya kiapo ulijitambulisha kwa Kungu John Malulu.

Kibatala: Maelezo hayo yapo kwa mujibu wa sheria. Ni sahihi majina hayo ni lazima kwa mujibu wa sharia?

Shahidi: Ni muhimu.

Kibatala: Ni lazima au ni hiyari kwa mujibu wa sheria? Tamko lisemwe limefanywa mahali fulani ieleze mahakama kuwa  tamko hilo umelifanyia wapi?

Shahidi: Hapajatajwa.

Kibatala: Kuna mahala pameandikwa muda uliotoa maelezo haya.

Shahidi: Hapajaandikwa muda.

Kibatala: Ni sahihi kuwa hapo ni mahala muhimu ili kuzuia kuchakachua maelezo?

Shahidi: Ni muhimi.

Kibatala: Naomba umwambie mheshimiwa hakimu, iwapo kurasa ya kwanza na ya pili, tatu na nne zinafanana.

Shahidi: Zinafanana

Kibatala: Upo chini ya kiapo karatasi ya kwanza inamistari ya pili ina mistari?

Shahidi: Haina.

Kibatala: Hii ni karatasi ya kisheria au sio ya kisheria?

Shahidi: Ya kisheria.

Kibatala: Jina liliosainiwa ni nani?

Shahidi: K. J. Malulu.

Kibatala: Nataka  kujua majina hayo yanafana na lile uliandika juu?

Shahidi: Hayafanani.

Kibatala akaomba mahakama kupokea nyaraka hiyo kama kielelezo.

Wakili wa serikali Katuga akaieleza mahakama kuwa bado upande wa Jamhuri unaendelea na masikitiko juu ya njia aliyotumia wakili Kibatala kwenye kung’ang’aniza kutolewa kwa maelezo ya shahidi.

Maeleozo haya, ni nakala na nakala zinataratibu zake …nakala inatumika kama nakala halisi ipo upande wa pili.”

“Angeiomba mahakama aitumie nakala halisi kwenye kuitumia kwenye kumhoji shahidi.”

“Mfano amemuuliza shahidi juu ya tofauti wa mistari wa ukarasa wa pili na wa kwanza ikiwa alikuwa akitumia nakala ambayo sio halisi. Tunapinga maelezo hayo kwakuwa ni nakala ambayo sio halisi (photocopy).”

Kibatala akijibu hoja hizo, ameeleza mahakama kuwa jambo la msingi ni kwamba shahidi ameyatambua maelezo yake na hajikataa.

“Shahidi ametambua kama maelezo ya kisheria ambayo yanaingia kwenye kesi hii. Maelezo haya wenzetu hawajabisha kuwa wametupa sisi ndani ya mahakama kama hitaji la kesheria.

“Sijamsikia wakili yoyote aliyesema kuna tofauti na angesema kuna tofauti kati ya nakala hii na nakala halisi,tungechukua hatua za  kisheria.”

Kibatala amedai kuwa huwezi kutumia nakala isipokuwa kwenye mazingira hayo. Amesema, iwapo upande wa pili wanayo nakala halisi mahakamani, maana yake, ni kwamba kuwa na nakala halisi mahakamani sio tu kwa muda huu maana yake imetolewa mahakamani.

“Sio kweli kwamba milango imefungwa kwenye kutumia nakala.” Kibatala akaendelea na mahojiano yake na wakili Malulu.

Kibatala: Ulisema kwamba ulipata taarifa kuhusiana na mkutano wa Zitto na waandishi wa habari.

Shahidi: Naifahamu.

Kibatala: Press release ni nyaraka au tukio.

Shahidi: Tukio.

Kibatala: Na ile nyaraka inayotolewa kwenye tukio la kihabari inatwaje?

Shahidi: Nyaraka ya press-release.

Kibatala: Unafahamu tofauti ya press conference na press relise.

Shahidi: Sifahamu.

Kibatala: Kwenye maelezo yako umesema, Zitto amejipambanua kama kiongozi wa chama. Anajipambanua maanake nini?

Shahidi: Anajitangaza.

Kibatala: Unaifahamu taasisi ya msajili wa vyama vya siasa?

Shahidi: Naifahamu.

Kibatala: Ukiwa kama mkuu wa upelezi na ndiye uliyekuwa ukipeleleza kesi hii, uliwahi kwenda kuangalia kwenye nyaraka za msajili wa vyama vya siasa kujua hicho cheo?

Shahidi: Haikuwa relevant kwangu.

Hakimu akaingilia. Akasema, nimerekodi kuwa  hakwenda.

Kibatala: Tueleze eneo husika la (Press) mkutano iliyofanyika umetaja nyumba namba umetaja mtaa.

Shahidi: Nilitaja makao makuu, Kijitonyama.

Ulitaja nyumba namba.

Shahidi: Sikutaja.

Kibatala: Ulitaja plot namba?

Shahidi: Sikutaja.

Kibatala: Umetajata jina la mtaa?

Shahidi: Sikutaja.

Kibatala: Uliwataja hao makachelo uliowapa kazi ya kusimamia kazi katika eneo husika?

Shahidi: Sikutaja.

Kibatala: Ieleze mahakama iwapo umetaja aina ya simu uliyopeleza.

Shahidi: Haikutajwa.

Kibatala: Mwambie hakimu umesema uliona kwenye Youtube press conference au Press-Release.

Shahidi: Press-release.

Ulimuonesha mheshimuwa Hakimu maudhui uliyoyaona Youtube?

Shahidi: Sijamuonesha.

Kibatala: Umemsimulia Hakimu ulichokiona?

Shahidi: Nimemuhadithia.

Kibatala: Shahidi kwa kuwa wewe ndio mtu wa kwanza kuingia Youtube na ndio mtoa taarifa umetoa video clip (vipande vya video), mbele mahahama juu mkutano wa Zitto, umezitoa hizo nyenzo mbili?

Shahidi: Sijazitoa.

Kibatala: Ni sahihi kuwa haukutilia maanani maudhui ya content ya Youtube?

Shahidi: Ni sahihi mpaka kesho nilipona mihemko ya wananchi.

Kibatala: Umemtajia Hakimu hakimu juu namba za gari?

Shahidi: Sikutaja.

Kibatala: Ulimtajia hakimu aina ya gari uliokuchukuwa kutoka Osterbay hadi Kimara?

Shahidi: Sikutaja.

Kibatala: Ulimtajia hakimu majina ya dereva?

Shahidi: Sijataja.

Kibatala: Ukiwa Manzese, uliona kundi la watu na ukasema na hali zao kama walikuwa ya mihemko.

Walikuwa wanaelekea kufanya jinai au kama Arsenal na Manchester?

Shahidi:  Kawaida.

Hali ya mabishano yale walionekana kuwa wanakwenda kufanya tukio la kihalifu. Hali ya hasira, lakini kawaida.

Kibatala: Ulifanyika uhalifu juu ya majadiliano hayo?

Shahidi: Hapana hawakufikia hali ya kufanya uhalifu.

Kibatala: Ndio maana haukutuma vikosi vya kufuatilia niliweka wachunguzi.

Kibatala: Ulisema au hukusema kuhusu kuweka wachunguzi?

Shahidi: Sikuongozwa.

Kibatala: Mtu uliyemchagua kuwa atakupa ulisema, anaitwa nani?

Shahidi: Shabani Hamisi.

Kibatala: Hukuona umuhimu wa kumuita mtu mwengine kwa ajili ya kuwa shahidi?

Shahidi: Huyo mwenyewe shahidi.

Kibatala: Alitafutwa mtu wa tatu hakutafutwa?

Shahidi: Wanini sasa.

Kibatala: Unafahamu rais wa nchi aliandikiwa barua na raia aliyelalamika kubambikiwa kesi na upelelezi ukafanyika akaachiwa baada ya Rais kuingilia kati?

Shahidi: Sijui.

Hakimu Shahidi ameihalisha kesi hiyo mpaka kesho saa 3:00 asubuhi na kuendelea na ushahidi wa shahidi huyo. MwanaHALISI Online itakuwepo mahakamani kueleza neno kitakachotokea.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

BiasharaHabari za Siasa

Zanzibar mbioni kuanza uchimbaji mafuta na gesi baharini

Spread the loveSERIKALI ya Zanzibar, imekamilisha mchakato wa uchimbaji wa mafuta na...

Habari za Siasa

Wizara ya afya yataja mafanikio 10 miaka mitatu Samia madarakani

Spread the loveWIZARA ya Afya imetaja mafanikio 10 iliyoyapata ndani ya miaka...

Habari za Siasa

Mbozi walilia kuwa manispaa, majimbo 3

Spread the loveHALMASHAURI ya wilaya ya Mbozi mkoani Songwe imeeleza dhamira yake...

Habari za Siasa

Wabunge waitaka TPDC kuongeza kasi ya kuunganisha wateja gesi asilia

Spread the love  KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini...

error: Content is protected !!