Tuesday , 19 March 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Kesi ya Mbowe: Shahidi wa Jamhuri afungua ‘darasa’ kortini
Habari za SiasaTangulizi

Kesi ya Mbowe: Shahidi wa Jamhuri afungua ‘darasa’ kortini

Spread the love

SHAHIDI wa saba katika kesi ya uchochezi inayowakabili viongozi tisa wa Chadema,Victoria Wihenge amefungua ‘darsa’ kortini kwa kueleza hatua mbalimbali zinazochukuliwa kuelekea kwenye chaguzi. Anaripoti Faki Sosi … (endelea).

Akitoa maelezo yake, upande wa utetezi muda wote ulikuwa umetega sikio kumsikiliza Wihenge ambaye amejitambulisha kuwa ni Ofisa wa Uchaguzi katika Manispaa ya Kinondoni.

Wihenge alianza kutoa ushahidi wake leo tarehe 21 Agosti 2019 saa 8:15 mchana hadi saa 9:45. Hata hivyo, wakili Simon Wankyo alimuongoza shahidi huyo kuiomba mahakama kumruhusu kwenda kuona na daktari kutokana na kuwa na ahadi naye saa 10 jioni. 

Hakimu Mkazi Mkuu wa mahakama hiyo, Thomas Simba ameahirisha shauri hilo na kusema, litaendelea kesho tarehe 22 Agosti 2019 saa 5 asubuhi.

Kabla ya kuahirishwa kwa shauri hilo, akiongozwa na Wakili Wankyo, shahidi huyo ameieleza mahakama, aliajiriwa mara ya kwanza 2003 katika cheo cha Maendeleo ya Jamii wilayani Mpwapa kwa miaka sita (mpaka 2009).

Ameieleza mahakama kuwa alibadilishiwa majukumu na kuwa Ofisa Utumishi kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapa mwaka 2009, alifanya kazi mpaka 2012 alipohamia Halmashauri ya Wilaya ya Kinondoni katika nafasi hiyo hiyo.

Amedai kuwa, amefanya kazi kama ofisa utumishi kwenye Wilaya ya Kinondoni mpaka mwaka 2016.

Ameeleza, majukumu yake kwa muda huo ilikuwa ni kusimamia utawala bora kwenye Kata na Mitaa ya Manispaa ya Kinondoni.

Mwaka 2014 alikuwa msimamizi msaidizi wa uchaguzi kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu mwaka 2015.

Ameeleza, majukumu yake akiwa Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi kwa mwaka 2014 na 2015, yalikuwa kusimamia wasimamizi wa uchaguzi kwenye kata na mitaa katika uchaguzi wa jimbo na kata.

Na kwamba mwaka 2016, alianza rasmi kutekeleza majukumu ya Ofisa Uchaguzi wa Manispaa ya Kinondoni mpaka sasa akiwa mahakamani hapo.

Amedai kuwa, yeye ndio mratibu wa shughuli zote za uchaguzi katika Manspaa ya Kinondoni.

Victoria ameieleza mahakama kuwa anaratibu Uchaguzi Mkuu, uchaguzi mdogo na uchaguzi wa marudio.

Amefafanua kazi yake ya uratibu kwamba, ni kufuata ratiba ya tume ya uchaguzi kwa mujibu wa sheria inayomuongoza kutekeleza majukumu yake.

Amedai, ratiba hiyo ni pamoja na kuchukua fomu za uteuzi na siku ya kurudisha fomu hizo , siku za kampeni pamoja na siku ya uchaguzi.

Victoria ameeleza, kwenye kampeni anazingatia kamati ya ratiba ya kampeni, kamati ya maadili pia ratiba hiyo inazingatia viwanja vya kampeni na viongozi kuzingatia maadili kwa kupindi chote cha kampeni.

Ameitaja sura ya 343 fungu la 124 (A) ya sheria za uchaguzi, kuwa ndio muungozo wa kamati ya maadili maadili ya kampeni kwa viongozi.

Amedai, kamati hiyo ina mjumbe mmoja kutoka kila chama kinachogombea na msimamizi msaidizi wa uchaguzi wawili wanaoteuliwa na Tume ya Uchaguzi, pia ni watumishi wa umma na kwamba mmoja anakuwa mwenyekiti na mwengine katibu.

Ameieleza mahakama kuwa, majukumu ya kamati hiyo ni kuratibu shughuli za kampeni kwa maana kupanga viwanja kwa uwiano na jukumu la kuamua kubadilisha kampeni.

Ameeleza, wajumbe wanaotoka kwenye vyama vya siasa wanachaguliwa na makatibu wa vyama vyao kwa maelekezo ya barua ya msimamizi wa uchaguzi.

Shahidi huyo amedai, majukumu ya kamati ya maadili ni pamoja na kusimamia maadili ya viongozi wa vyama vya siasa na serikali kipindi chote cha uchaguzi.

Ameeleza, mambo muhimu ya kuzingatia kwenye uchaguzi ni sheria, kanuni na taratibu pia ratiba ya uchaguzi ambayo yatazingatiwa na msimamizi wa uchaguzi , ofisa uchaguzi, wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi na wadau wa uchaguzi ambao ni vyama vya siasa pamoja na wananchi.

Amedai kuwa, Januari 2018 anakumbuka Mkurugenzi wa Tume ya Uchaguzi alitangaza uchaguzi mdogo wa ubunge katika jimbo la Kinondoni kwamba utafinyika tarehe 17 Februari 2018.

Ameeleza, Mkurugenzi wa Manspaa ya Kinondoni ambaye ni msimamizi wa uchaguzi, aliitisha kikao cha wadau wa uchaguzi.

Alipoulizwa kikao kilifanyika lini na wadua ni kina nani, alijibu “vyama vya siasa ndio wanakuwa kwenye hiko kikao ambapo mwenyekiti na katibu, anakuwa kaishachaguliwa…

“Mimi ndio nilikuwa katibu wa kikao hiko na wajumbe wengine ni wasimamizi wasaidizi wa kata na mitaa.”

Ameleeza, kwa kuwa kikao hiko ni cha kwanza vyama vyote vya siasa vilivyo sajiliwa, vinahaki ya kuhudhuria.

Amevitaja vyama 19 vya siasa vilivyosajiliwa kuwa ndivyo vilivyohudhuria na kuvitaja vichache kama vile Ada-Tadea, AFP, CUF, CCM, UMD , Demokrasia Makini, TLP, Chadema , na NRA.

Amedai, wahudhuriaji walikuwa ni wenyeviti na makatibu wa vyama hivyo ngazi ya wilaya.

“Lengo la kikao hiko ni kuvitaarifu vyama vya siasa juu ya uwepo wa uchaguzi wa mbunge jimbo la Kinondoni.

“Tuliipitia ratiba ya uchaguzi kwa maana ndio ajenda kuu iliyojadiliwa…tunapitia ratiba ili vyama vijue tarehe ya uchaguzi, kipindi cha kampeni, siku ya kufanya uteuzi pamoja na kipindi cha kuchukua fomu,” ameeleza Victoria.

Amedai, kikao hiko kiliwafanya wajumbe wakajiandae na uchukuaji fomu na uteuzi ambapo fomu zilianza kuchukulia tarehe 14 mpaka tarehe 20 Januri 2018.

Ameeleza, tarehe 20 Januari 2018 vyama vya siasa vilitakiwa virejee na jina moja litakalowasilishwa kwenye kamati ya maadili.

Watuhumiwa kwenye kesi hiyo namba 112 ya mwaka 2018 ni Freeman Mbowe, mwenyekiti wa chama hicho Taifa; Dk. Vincent Mashinji, Katibu Mkuu; John Mnyika, Naibu Katibu Mkuu Bara na Salum Mwalimu, Naibu Katibu Mkuu Zanzibar.

Wengine ni Ester Matiko, Mbunge wa Tarime Mjini; Ester Bulaya, Mbunge wa Bunda Mjini; Peter Msigwa, Mbunge wa Iringa Mjini; John Heche, Mbunge wa Terime Vijijini.

Upande wa Jamhuri umewakilishwa na Faraja Nchimbi, Wankyo Simon na Dk Zainab Mango ambapo upande wa utetezi ukiongozwa na Prof. Abdallah Safari, Peter Kibatala, Dickson Matata, Jeremiah Mtobesya na Fedreck Kihwelo.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaTangulizi

Askofu Bagonza: CDF Mabeyo amepasua masikio yetu

Spread the loveMJADALA kuhusu safari ya mwisho ya maisha ya Hayati Rais...

Habari za Siasa

10 matatani kwa kutorosha madini ya bil 1.5

Spread the loveJeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya kwa kushirikiana na Kikosi...

Habari za Siasa

Wagombea 127 wa udiwani kutoka vyama 18 kuchaguliwa kesho

Spread the loveWagombea udiwani 127 kutoka vyama 18 vya siasa wanatarajiwa kupigiwa...

BiasharaHabari za Siasa

Zanzibar mbioni kuanza uchimbaji mafuta na gesi baharini

Spread the loveSERIKALI ya Zanzibar, imekamilisha mchakato wa uchimbaji wa mafuta na...

error: Content is protected !!