MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, imeamua kutazama upya ushahidi wa video iliowasilishwa na shahidi namba sita wa Jamhuri (koplo Charles), katika kesi ya uchochezi inayomuhusu Freeman Mbowe na wenzake. Anaripoti Regina Mkonde … (endelea).
Mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu wa mahakama hiyo Thomas Simba leo tarehe 20 Agosti 2019, mahakama hiyo imekubali video hiyo ioneshwe tena baada ya Wakili upande wa utetezi, Peter Kibatala kuomba ushahidi huo wa video urejewe akidai kuwa, Koplo Charles ameomba kwa zaidi ya mara nne kuuangalia kwa ajili ya kupata kumbukumbu ya maneno yaliyozungumzwa ndani yake.
Ombi hilo la Kibatala liliibuka mahakamani hapo, baada ya shahidi huyo kuieleza mahakama hiyo mara kadhaa, kwamba hakumbuki baadhi ya maneno na matukio yaliyoonekana katika ushahidi huo wa video.
Baada ya ombi hilo, Hakimu Simba alikubali ushahidi huo urejewe tena na kuiahirisha kesi hiyo kwa muda ili zoezi hilo lifanyike na kisha usikilizwaji wa kesi hiyo uendelee.
Jana tarehe 19 Agosti 2019 mahakama hiyo ilioneshwa kielelezo namba tano cha ushahidi wa video inayowaonesha washtakiwa hao tisa ambao ni viongozi wa Chadema akiwemo Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa chama hicho Taifa na Dk. Vicent Mashinji, Katibu Mkuu wa Chadema wakihutubia kwenye mkutano wa kufunga kampeni za uchaguzi wa marudio wa jimbo la kinondoni uliofanyika kwenye viwanja vya Buibui Kinondoni tareje 16 Februari 2018.
Pia, sehemu ya video hiyo hasa kipengele cha mwisho inaonesha watu kadhaa ikiwemo wafuasi wa Chadema wakiandamana kuelekea katika ofisi ya msimamizi wa uchaguzi wilaya ya Kinondoni.
Endelea kufuatilia MwanaHALISI Online kwa taarifa zaidi kuhusu muendelezo wa usikilizwaji wa kesi hiyo.
Leave a comment