January 15, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Kanisa Anglikana: Tuepushe visasi

Spread the love

VYAMA vya siasa nchini, vimetakiwa kumaliza tofauti zao kwa kukaa meza moja na kuzungumza ili kuweza kufikia mwafaka wa kupata amani badala ya kutunishiana misuli na kulipiza visasi. Anaandika Danson Kijage, Dodoma…(endelea).

Kauli hiyo imetolewa na Dk. Dikson Chilonganya, Askofu wa Kanisa la Anglikana, Dayosisi ya Kati wakati wa mahubiri katika ibada ya kumbukizi ya kuzaliwa kwa Yesu Kristo kwenye Kanisa Kuu la Roho Mtakatifu Anglikana lililopo Jijini Dodoma.

Akihubiri kanisani hapo amesema, Tanzania ni nchi ya amani na amani hiyo imejengwa na waasisi waliotangulia, hivyo inatakiwa kulindwa ili nchi iendelee kuonekana kisiwa cha amani.

“Amani inaweza kuonekana kama jambo dogo kwa kuwa hakuna vita, lakini vita inaweza isiwepo lakini watu wakawa hawana amani kutokana na kutokuwa na nyuso za furaha kwa yale wanayokutana nayo.

“Hatuwezi kutafuta amani kwa mapambano au mabavu na wakati mwingine tumeona viongozi wa kisiasa wakijitamba kutafuta amani kwa kutumia mabavu au kwa njia ya mabavu, jambo ambalo haliwezi kusaidia kama hawatatafuta amani kwa njia sahihi ya kumtanguliza Mungu na kukaa meza moja,” amesema Askofu Chilongani.

Pia amesema, ili kuweza kutunza amani ya nchi ni lazima kujiepushe na tabia ya kulipiza visasi pamoja na kuwa na roho ya kutokuwa na makubaliano.

Askofu Chilongani amesema, lazima kuomba amani na kuitunza huku akisisitiza kuwa, Amani iliyopo Tanzania isichezezewe.

“Tuzungumze Amani pale panapooneka hakuna amani, kaeni meza moja ili kuweza kujadili changamoto mbalimbali ambazo zipo ili ziweze kutatuliwa kwa mazungumzo.

“Ikumbukwe kuwa, hata ndani ya vyama vya siasa haiwezekani kupatikana kwa amani kama viongozi wa kisiasa hawataweza kukaa meza moja. Hakuna amani ambayo inaweza kupatikana kwa ubabe au mtutu wa bunduki.

“Jambo lingine muhimu ni kuhakikisha tunakuwa watendaji wa amani sambamba na kujiepusha katika kulipiza visasi,” amesema Askofu Chilongani.

error: Content is protected !!