Thursday , 28 March 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Kampuni ya LZ Nickel yafuatayo nyayo za Barrick
Habari za SiasaTangulizi

Kampuni ya LZ Nickel yafuatayo nyayo za Barrick

Spread the love

KAMPUNI ya LZ Nickel Limited ya nchini Uingereza, imefuata nyayo za Kampuni ya Madini ya Barrick Gold Corparation, kwa kuingia ubia na Serikali ya Tanzania, na kuanzisha kampuni ya pamoja ya uchimbaji madini. Anaripoti Mwandishi Wetu, Kagera … (endelea).

Wakati Kampuni ya Barrick ikishirikiana na Serikali ya Tanzania kuunda Kampuni ya Madini ya Twiga Minerals, Kampuni ya LZ Nickel Ltd na serikali hiyo imeunda kampuni ya ubia ya Tembo Nickel.

Pamoja na kampuni tanzu ya Tembo Nickel Corporation Ltd, ambayo itasimamia kampuni ya uchimbaji madini hayo itakayoitwa Tembo Nickel Mining Corporation Ltd, na kampuni ya uchenjuaji madini itakayoitwa Tembo Nickel Refining Company Ltd.

Serikali ya Tanzania na Kampuni ya LZ Nickel Ltd, zimeingia mkataba wa uchimbaji madini ya Nickel katika eneo la Kabanga mkoani Kagera, sambamba na uanzishwaji Kiwanda cha uchenjuaji madini wilayani Kahama mkoa wa Shinyanga.

Hafla ya utiaji saini mkataba huo imefanyika leo Jumanne tarehe 19 Januari 2021, wilayani Bukoba Mkoa wa Kagera na kushuhudiwa na Rais John Magufuli.

Akizungumza katika hafla hiyo, Rais Magufuli ameagiza Wizara ya Madini kuhakikisha mradi wa uchimbaji madini ya Nickel katika eneo hilo, unaanza mara moja.

“Inawezekana tungeanza kuchimba 1976, Ngara na Kagera tusingekuwa na umasikini namna hii, niwaombe wizara ya madini ielekeze spidi kubwa, kujua ina mali kiasi gani.

Na hivi wamesema hii ni first class product (bidhaa daraja la kwanza), wapiga kelele waache wapige kelele, sisi tunakwenda mbele,” amesema Rais Magufuli.

Rais Magufuli amesema mapato yatakayopatikana katika kampuni hiyo, yatagawiwa asilimia 50 kwa 50 kwa kila upande kama ilivyo kwa kampuni ya Twiga Minerals ambapo Tanzania imeingia ubia na Kampuni ya Barrick.

“Kwa sasa tumeanzisha kampuni Tembo Nickel, ni matumaini yangu kama alivyozungumza kiongozi wa kampuni hiyo, amezungumza mapato yawe sawa kwa sawa.

Na mimi nimeshukuru kama ilivyo Barrick, mapato tunayo pata sisi asilimia 50 na wao 50, na huyu amezungumza hivyo hivyo,” amesema Rais Magufuli.

Rais Magufuli amesema LZ Nickel Ltd imeahidi kujenga kiwanda cha uchenjuaji ambapo Serikali itapata mgawo wake kwa kila madini yatakayochenjuliwa kiwandani hapo.

“Nimefurahi kwamba wameamua kujenga smelter (kiwanda cha uchenjuaji), smelter ndio jibu rahisi ya kutoibiwa Tanzania. Madini ya Nickel yatakapochimbwa yatakuja na madini mengine ambayo yako pale Kabanga,” amesema Rais Magufuli.

Hata hivyo, kiongozi huyo wa Tanzania amesema Serikali itaendelea kufanya mazungumzo na kampuni hiyo, ili kuhakikisha Tanzania ina nufaika na mradi huo sambamba na kudhibiti mianya ya upotevu wa madini.

“Lakini pia nina matumaini mazungumzo yatakavyokuwa yanaendelea, awamu nyingine baada ya kuangalia mali asili iliyomo, Watanzania hatutapunjika.

Yatakapochimbwa yale yakapelekwa Kahama kwenye smelter yatachujwa, shaba itawekwa mahali pake, Platinum, Niko na Kobati yanakuwa mahali pake, inawezekana kuna dhahabu pia inakuwa mahala pake. Kila dini litakalouzwa na sisi tutakuwa na hisa zetu,” amesema Rais Magufuli.

Awali, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba Kabudi, alielezea masharti iliyopewa kampuni ya LZ Nickel Ltd na Serikali ya Tanzania, kabla ya kuingia ubia katika mradi huo.

Prof. Kabudi ametaja masharti hayo kuwa ni, kuhakikisha Serikali haitakuwa na deni lolote katika mradi huo, ijenge kiwanda cha uchenjuaji madini na ikubali kuanzisha kampuni ya ubia kati yake na serikali.

Pia, ikubali kugawana na serikali sawa kwa sawa faida itakayotokana na uchimbaji, uchenjuaji na uuzaji madini hayo, bila kujali umiliki wa asilimia za hisa.

Akielezea utendaji wa kampuni hiyo, Prof. Kabudi amesema kampuni hiyo itakuwa chini ya usimamizi wa pamoja na kwamba Serikali ya Tanzania itasimamia shughuli za uchimbaji na usafishaji madini yatakayochimbwa.

“Ofisi na uendeshaji wa kampuni ya ubia na kampuni zake tanzu zilizoundwa zitakuwa Tanzania chini ya usimamizi wa pamoja, hivyo Serikali itakuwa jicho la karibu la usimamizi wa mwenendo wa shughuli za uchimbaji na usafishaji madini ya Nickel,” amesema Prof. Kabudi.

Prof. Kabudi amesema fedha zitakazotokana na mradi huo, zitahifadhiwa nchini Tanzania.

“Fedha zote zitokanazo na madini hayo zitahifadhiwa katika benki zilizopo Tanzania, ili kuimarisha akiba ya fedha za kigeni ndani ya nchi na hivyo kuimarisha uchumi,” amesema Prof Kabudi.

Prof. Kabudi amesema Serikali itakuwa na asilimia za hisa zisizopungua 16.

Amesema utafiti uliofanyika unaonesha mauzo ya madini yatakayochimbwa yatakuwa Dola za Marekani 664 Mil.

“Makisio ya awali yanaonesha uzalishaji utakuwa na wastani wa mauzo yenye thamani ya zaidi ya Dola za Marekani Milioni 664 kwa mwaka,” amesema Prof. Kabudi.

Katika ushirikiano baina ya Serikali ya Tanzania na Kampuni ya Barrick, serikali hiyo ina miliki asilimia 16 za hisa katika kampuni ya madini ya Twiga, wakati Barrick ikimiliki hisa 84.

Ubia huo baina ya Serikali ya Tanzania na Barrick ulikuwa ni utekelezaji wa Sheria mpya ya madini ya mwaka 2017.

Kampuni ya Twiga Minerals imeundwa kwa ajili ya kusimamia migodi mitatu (Buzwagi, North Mara na Bulyanhulu), iliyokuwa chini ya Kampuni ya Acacia.

Hatua hiyo ilichukuliwa baada ya mgogoro ulioibuka kati ya Kampuni ya Barrick na Serikali ya Tanzania, kufuatia sakata la makontena ya mchanga wa dhahabu, yaliyozuiwa katika Bandari ya Dar es Salaam, kwa tuhuma za ukukwaji wa sheria.

Sakata hilo lilisababisha Rais Magufuli aunde tume ya kuchunguza mwenendo wa biashara ya madini, baada ya kubaini udanganyifu wa viwango vya madini yanayo safirishwa nje ya nchi, uliosababisha Serikali kupoteza mapato.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaTangulizi

Mashirika matano yapata hasara mabilioni ya fedha

Spread the loveMASHIRIKA matano ya Serikali yanayojiendesha kibiashara, yamepata hasara ya mabilioni...

Habari za SiasaTangulizi

CAG aibua madudu halmashauri 10, TANESCO na MSD

Spread the loveRIPOTI ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali...

Habari za Siasa

Alichokisema Rais Samia baada ya kupokea ripoti ya CAG, TAKUKURU

Spread the loveRAIS Dk. Samia Suluhu Hassan, amesema Serikali yake itafanyia kazi...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Kapinga kuongoza usambazaji wa mitungi ya gesi 10,000 ya Taifa Gas

Spread the loveNaibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga ameahidi kuongoza kwa ufanisi...

error: Content is protected !!