Thursday , 25 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa JPM atibua Chadema, kwenda kortini
Habari za Siasa

JPM atibua Chadema, kwenda kortini

Rais John Magufuli
Spread the love

CHAMA cha Chadema kimesema kitafungua shauri mahakamani, kupinga sheria mpya ya vyama vya siasa, iliyosainiwa na  Rais John Magufuli tarehe 19 Machi mwaka huu. Anaripoti Mwandishi Wetu…(endelea).

Taarifa hiyo imetolewa kwa umma leo  tarehe 22 Machi 2019, na Mkurugenzi wa Itikadi, Mawasiliano na Mambo ya Nje Chadema,John Mrema.

Katika Taarifa yake, Mrema amesema wanaipinga sheria hiyo kwa kuwa baadhi  ya vifungu vyake vinaifanya shughuli za kisiasa kuwa ni jinai kwa wanasiasa, huku vikimlinda na kumpa mamlaka makubwa msajili wa vyama vya siasa.

Pia, amesema Sheria hiyo ni mbaya kutokana na baadhi ya vifungu vyake ama kukiuka Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na misingi ya utawala bora pamoja.

Pia vinakiuka mikataba mbalimbali  ya kimataifa ambayo Tanzania tumetia saini.

“Kama ilivyokuwa dhamira yetu ya awali ya kupeleka Shauri mahakamani.

“Nia na dhamira hiyo iko palepale. Na tunaendelea kushauriana na Vyama vingine vya Siasa na wadau mbalimbali njia nzuri zaidi ya kufungua shauri Mahakamani mapema iwezekanavyo,” amesema na kuongeza;

“Sheria hii imeenda kufanya shughuli za Kisiasa nchini kuwa ni jinai kwani kila kifungu cha Sheria hii kimeweka adhabu ya faini,  kifungo au vyote kwa pamoja kwa  Wanasiasa ila Msajili na Serikali na vyombo vyake hakuna kifungu hata kimoja ambacho kinawagusa kama wakikiuka utekelezaji wa Sheria hii.”

Akikazia kuhusu upungufu wa sheria mpya ya vyama vya siasa, Mrema ametaja vifungu takribani 10 ambavyo vina upungufu ikiwemo, Kifungu cha 3 (b).

Amesema, Kifungu hicho kimempa Msajili wa Vyama vya Siasa jukumu la kusimamia chaguzi za ndani za Vyama ikiwa ni Pamoja na teuzi za Wagombea wa nafasi mbalimbali.

” Hii inampa Msajili mamlaka ya kuingilia Vyama na kuviamulia ni nani awe Kiongozi wa Chama husika au mgombea wa nafasi ya kiserikali kama ngombea urais na ubunge.

“Hii ni kinyume   na Katiba ya nchi ambayo imetoa fursa na haki ya kujumuika kwa wananchi wake,” ameeleza Mrema.

Kifungu kingine alichotaja Mrema, ni kifungu cha 3 (g), ameeleza kuwa kinamfanya Msajili wa Vyama vya Siasa kuwa mshauri wa serikali kuhusu Vyama vya Siasa,  badala ya Vyama.

Hivyo kinamuondolea sifa muhimu ya kuwa mlezi wa Vyama na badala yake anaenda kuwa msimamizi wa Vyama.

“Kifungu cha 5A (i) kinampa Msajili wa Vyama mamlaka ya kuamua aina ya mafunzo ambayo Chama kinatakiwa kupata kutoka mashirika na taasisi  mbalimbali       za nje .

“Huku ni kuvinyima haki Vyama kupata utaalamu na mbinu za kisasa za kufanya siasa kwani Msajili anaweza kuzuia mafunzo kwa hisia tuu kuwa kama yakitolewa yanaweza kukifanya Chama husika kuwa na mbinu za kukiondoa Chama tawala madarakani ,” amesema na kuongeza Mrema.

“Aidha Vyama vya Siasa viko kwenye Muungano wa kiitikadi za kidunia na hivyo kuvifanya kunufaika na mafunzo mbalimbali   yanayotolewa kutokana na mirengo hiyo,kumpa Msajili uamuzi wa mwisho kuhusu mafunzo ya Vyama ni kuendelea kuzuia haki za Vyama kujumuika na kushirikiana.”

Kifungu kingine alichotaja Mrema kuwa kina upungufu ni Kifungu cha 5B (i).

Amesema kifungu hicho kinampa nsajili mamlaka ya kudai taarifa yoyote kutoka ndani ya Chama cha Siasa au Kiongozi wakati wowote hata kama taarifa hiyo ni mbinu na mikakati  ya ushindi ya chama husika.

Pia, na kama asipopatiwa basi chama au kiongozi anaweza kulipishwa faini ya kiasi cha shilingi milioni 10.

“Kifungu cha 6B (d) kinampa mamlaka Msajili ya kusajili Chama cha siasa Mtanzania mwenye miaka 18 lakini kwa mujibu wa katiba ya mwaka 1977, Sheria ya uchaguzi ya Mwaka 1985 na Ile ya serikali za Mitaa inamnyima haki ya kugombea nafasi ya Urais, Ubunge , Udiwani na uongozi kwenye Kijiji,  Mtaa au kitongoji kama mtu huyo hajafikisha miaka 40 kwa Urais au 21kwa nafasi nyingine.

‘Sheria hii inampa fursa mtu kusajili Chama lakini haruhusiwi kuwa kiongozi, hii ni kinyume na Tamko la ulimwengu la Haki za binadamu juu ya Haki ya kuchagua na kuchaguliwa,” amesema na kuongeza;

“Kifungu cha 8C (2) kinampa Msajili wa Vyama mamlaka ya kukisimamisha Chama cha siasa kwa sababu tu hakijampelekea kwa ufasaha orodha ya Wanachama wake.”

Amehoji ” hivi ingekuwaje kama Sheria hii ingekuwa inatumika kabla ya Maalim Seif kujiunga na ACT na Wana Chama wa CUF Zanzibar kuamua kumfuata?  Kingefutwa ACT au CUF Lipumba?

“Nani angehukumiwa kwa kupeleka orodha ambayo sio sahihi?  Vyama vya siasa ni taasisi ambazo zinabadilika kulingana na wakati na matukio na hivyo kufanya Wanachama wake kupungua au kuongezeka kutokana na matukio husika.”

Amesema, sio sahihi kuvisimamisha vyama kwa sababu tu ya orodha ya wanachama wake.

Sheria mpya ya Vyama vya Siasa imesainiwa na Rais John Magufuli tarehe 13 Februari 2019 na kuchapwa kwenye Gazeti la Serikali la tarehe 22 Februari, 2019.

 

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

Kilosa yawa mfano wa kuigwa miradi ya Mwenge nchini

Spread the love  KIONGOZI wa Mbio za Mwenge Kitaifa Godfrey Mzava amezitaka...

Habari za SiasaTangulizi

Biteko ataja vipaumbele 7 bajeti nishati 2024/25

Spread the love  NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Mwekezaji amwaga bil. 39 kujenga viwanda 3 vya uchenjuaji

Spread the loveKampuni ya Mineral Access System Limited (MAST) inayoiwakilishwa kampuni ya...

Habari za SiasaTangulizi

Mpwa wa Magufuli mbaroni kwa kusambaza picha za utupu

Spread the loveJESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limewakamata...

error: Content is protected !!