MWANDISHI wa habari Josephat Isango amefariki dunia mapema asububi leo, anaandika Hamisi Mguta.
Taarifa za kifo chake zimethibitishwa na mdogo wake aitwae Christopher ambaye amekuwa akimuuguza.
Christopher amezungumza na Mhariri wa gazeti la MwanaHALISI Jabir Idrissa na kusema Isango amefia hospitalini Ikungi mkoani Singida.
Isango alilazwa hospitalini hapo kwa wiki mbili sasa akisumbuliwa na kifua. Hata hivyo uchunguzi wa afya yake ulibaini ana tatizo kwenye moyo.
Aliwahi kuugua akiwa jijini Dar es Salaam na baada ya muda mfupi aliamua kusafiri kwenda Singida, mkoa wa nyumbani kwao.
Isango amekuwa mwandishi wa habari maarufu kutokana kuhusika na matukio ya kuvutana na polisi.
Mwaka 2015 alishambuliwa na polisi wa FFU eneo la mbele ya makao makuu ya Jeshi la Polisi katikati ya jijini Dar es Salaam alipokuwa na waandishi wengine wakisubiri kuwasili kwa viongozi wakuu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).
Viongozi wa Chadema waliitwa na Jeshi hilo kwa ajili ya mahojiano kuhusiana na tuhuma za kuchafua amani.
Kwa karibu miaka miwili, Isango alifanyakazi kampuni ya Hali Halisi Publishers Ltd (HHPL) inayomiliki na kuchapisha gazeti la MwanaHALISI na kuendesha mitandao ya kijamii.
Alihamia akitoka kampuni ya Free Media inayomiliki na kuchapisha gazeti la Tanzania Daima. Lakini alipata kuandika habari na makala MwanaHALISI kwa njia ya kujitegemea tangu mwaka 2008.
Isango, mzaliwa wa kijiji cha Kisasida, mkoani Singida, alisomea uandishi wa habari Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine Nyegezi jijini Mwanza.
Alikuwa mmoja wa waandishi wenye ujasiri wa kukabiliana na mazingira magumu ya kazi.
Alipoamua kuhama MwanaHALISI mhariri wake alisema itamchukua muda mrefu kupata mwandishi kijana mkakamavu kama Isango.
Leave a comment