Friday , 29 March 2024
Home Habari Mchanganyiko Jafo aagiza waliotafuna Bil 2.9 Ulanga wakamatwe
Habari Mchanganyiko

Jafo aagiza waliotafuna Bil 2.9 Ulanga wakamatwe

Suleiman Jafo, Waziri wa Tamisemi
Spread the love

OFISI ya Rais Tawala za mikoa na Serikali za mitaa (Tamisemi) imebaini matumizi mabaya ya fedha za serikali Sh. 2.98 bilioni katika halmashauri ya Ulanga mkoani Morogoro na kuagiza waliohusika wote wavulime nyadhifa zao na vyombo vya dola viendele na hatua kwa mujibu wa sheria dhidi yao. Anaripoti Dany Tibason, Dodoma … (endelea).

Hayo yalibainishwa na Waziri wa nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Suleiman Jafo wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari juu ya uchunguzi maalum uliofanywa kwa halmashauri ya wilaya hiyo.

Jafo alisema kuwa Ofisi ya Rais Tamisemi ilifanya uchunguzi maalum katika halmashari 12 nchini ambazo ni Ulanga, Same, Mbulu, Meru, Itigi, Misungwi, Nyang’hwale, Serengeti, Bahi, Mpwapwa na Morogoro ambapo katika halmashauri ya Ulanga uchuguzi ulianza Novemba 13 hadi 23 mwaka huu.

Alisema uchunguzi huo ulifanyika kufuatia malalamiko ya wananchi mbalimbali pamoja na mbunge wa jimbo la Ulanga Goodluck Milinga kutokana na ubadhirifu uliokuwepo.

Aidha alisema kiasi hicho kimebainika kupotea kutoka na matumizi mabaya ya fedha za serikali ambapo watumishi wasio waadirifu katika halmashauri hiyo walikiuka taratibu na kufanya manunuzi hewa na kutumia vibaya fedha tofauti na malengo yaliyopangwa.

“Halmashauri hii imekuwa ikifanya udanganyifu katika taarifa za miradi ya maendeleo taarifa za mfuko wa wanawake na vijana, kwa ujumla inausimamizi mbovu wa mapato na kuwa na udhibiti hafifu wa makusanyo na matumizi ya fedha za Umma,” alisema Jafo.

Jafo alisema kuwa mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya Ulanga, Yusufu Daud Semguruka kwa nafasi yake ya afisa masuhuli alishindwa kusiomamia sheria ya fedha za serikali za mitaa katika kudhibiti na kuweka mifumo dhabiti ya kuhakikisha fedha ziko salama kuanzia makusanyo hadi matumizi yake.

“Hii ni pamoja na kushindwa kumsimamia mweka hazina wa halmashauri katika kutekeleza majukumu yake na kwa kushindwa kutekeleza majukumu hayo amesababisha hasara halmashauri ya Sh.  2,980,172,763.60,” alisema Jafo.

Alifafanua kuwa Rajabu Siriwa, ambaye alikuwa ni mweka hazina wa halmashauri hiyo alichangia kuhujumu mapato ya serikli kwa kuweka utaratibu ambao umeisababishia hasara serikali.

Alisema kuwa mweka hazina huyo aliidhinisha malipo ya Sh. 225,586,400 nje ya bajeti bila idhini ya ofisi ya Rais Tamisemi ambapo marekebisho hayo yalihusisha posho ya safari ya mkurugenzi mtendaji Sh. 192,000,000.

“Pia kukusanya mapato na kutoyapeleka benki, katika mfumo wa LGRCIS umeonyesha halmashauri ilikusanya fedha ambazo hazikupelekwa benki kabisa Sh. 760,686,732.43 fedha hizi hazijulikani matumizi yake halisi ni nini,” alihoji Jafo.

Aidha alisema kuwa mweka hazina huyo aliandaa taarifa zenye udanganyifu kwa utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayotumia fedha za makusanyo ya ndani.

“Halmashauri imeripoti kupeleka Sh. 301,442,686 uhalisia wamepeleka 113,406,106.34 na udanganyifu katika mfuko wa vijana na akina mama halmashauri inaripoti kupeleka Sh. 120,000,000 uhalisia wamepeleka Sh. 31,500,000 kwa mwaka 2017/18 na 2018/19 hadi novemba 2018 wakati uchunguzi unakamilika,” alisema.

Aidha Jafo alisema kuwa Mhandisi David Kaijage akiwa anakaimu ofisi ya mkurugenzi februri mosi mwaka huu hadi Februari nane alihusika kwenye kuihujumu halmashauri kwa mapato ya Sh. 470,000,000 yaliyopolelewa kutoka kiwanda cha kilombero Valley Teak Company kwa kuzirejesha kwa mlipaji siku hiyohiyo waliyopokea.

“Pia alisaini hati ya malipo kumlipa Bahari Phamarcy kwa siku ambayo hakuwa kaimu mkurugenzi na mkurugenzi alikuwepo”alisema.

Jafo aliagiza ofisi ya mkuu wa mkoa wa Morogoro kuhakikisha kuwa wakuu wa idara na vitengo waliohusika akiwemo Willy Ndabila ambaye amehamishiwa itilima,na Rajabu Siriwa ambaye amehamishiwa Gairo wavuliwe nyadhifa zao na mamlaka za nidhamu na vyombo vya dola viendele na hatua kwa mujibu wa sheria.

Aliongeza kuwa watumishi wote waliohamishiwa Halmashauri ya ulanga wakiwa na makosa yaani DPMU, Willy Ndabila na DT, Rajabu Siriwa warejee halamashauri ya Ulanga ili kuiwezesha halmashauri na vyombo vya dola kufanya kazi yake.

“Maelezo juu ya mkurugenzi huyu wa Ulanga yenyewe yatatolewa baadaye na serikali,” alifafanua Jafo.

Hata hivyo Jafo alisema kuwa mkuu wa mkoa wa Morogoro ahakikishe kuwa Ofisi ya Rais Tamisemi imepata maelezo kwanini wataalamu hao hawakuchukuliwa hatua stahiki zenye tija dhidi ya taarifa za mkaguzi wa ndani ya robo ya tatu ya mwaka wa fedha 2017/18 kabla ya Januari 15 mwakani.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari Mchanganyiko

Puma Energy Tz: Watanzania tudumishe amani kuvutia uwekezaji

Spread the loveKAMPUNI ya Mafuta ya Puma Tanzania imewakutanisha wadau mbalimbali katika...

Habari Mchanganyiko

DAWASA waanza utekelezaji agizo la Samia

Spread the loveMamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam...

Habari MchanganyikoKimataifa

Zuma akataliwa kugombea urais

Spread the loveTUME Huru ya Uchaguzi Afrika Kusini (IEC) imemwondoa rais wa...

Habari Mchanganyiko

Mtandao watetezi wa haki za mazingira Tanzania waundwa

Spread the loveMTANDAO wa watetezi wa haki za mazingira nchini Tanzania, umeundwa...

error: Content is protected !!