Tuesday , 19 March 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Ilani ya Chadema 2020 hii hapa
Habari za Siasa

Ilani ya Chadema 2020 hii hapa

Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Chadema
Spread the love

MKUTANO Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), umepitisha Ilani yake ya Uchaguzi Mkuu 2020. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Ilani hiyo imepitishwa leo Jumanne tarehe 4 Agosti 2020 na wajumbe wa mkutano huo uliofanyika kwenye Ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam.

Akisoma muhtasari wa ilani hiyo mbele ya wajumbe hao, John Mrema, Mkurugenzi wa Itifaki na Mambo ya Nje Chadema, amesema ilani hiyo inakwenda kwa kauli mbiu ya ‘Maendeleo na Haki’ kama ilivyoelezwa na Baba wa Taifa Hayati Julius Nyerere.

“Ilani yetu imejikita hapo, tuwe na maendeleo lakini watu wawe na haki zao, sio maendeleo ya kuvunjia watu nyumba, hakuna fidia halafu unasema maendeleo.

“Na tuwakumbushe wajumbe wa mkutano mkuu maneno ya Baba wa Taifa mwaka 1971 alioandika kwenye muongozo wa TANU, alisema kitendo chochote kinachowapa uwezo wa kuamua maendeleo yao wenyewe ni maendeleo yenyewe,” amesema Mrema.

 Akiichambua sehemu ya ilani hiyo, Mrema amesema imelenga kufanya ugatuaji wa madaraka ya uongozi kutoka Serikali Kuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa hadi kwa wananchi.

“Chadema tunasema ugatuaji wa madaraka bahati mbaya hii picha imekaa chini, ukiona utaona hali ya sasa mtu mmoja amejilimbikiizia yote mpaka imekuwa mzigo kwake, sisi Chadema tunasema tutagatua madaraka kwa kushusha mamlaka kamili kwa serikali za majimbo au kanda, mitaa, vijiji na vitongoji kuzipa uwezo wa kufanya maamuzi kamili kwa kutumia furza za maendeleo zinazopatikana maeneo husika,” amesema Mrema.

Mrema amesema, iwapo Chadema kitafanikiwa kushinda kwenye uchaguzi huo, ndani ya siku 100 Serikali yake itaunda Serikali za majimbo.

“Serikali Kuu haitakumbatia kila kitu katikati kama ilivyo sasa mabaraza ya madiwani hayana nguvu, makusanyiko yanabaki Serikali Kuu, Chadema tunasema hapana, tunaenda kushusha madaraka, tugawane Taifa lisonge mbele.

John Mnyika, Katibu Mkuu wa Chadema

“Tuanenda kuunda Serikali z a majimbo, kama majimbo yanashughulika na zao la pamba kuwe na waziri wa pamba sababu anaijua pamba.”

Akielezea muhtasari wa ilani hiyo, Mrema amesema Serikali ya Chadema itarejesha mchakato wa upatikanaji Katiba Mpya, ulioasisiwa na Jaji Joseph Warioba.

“Serikali ya Chadema itarejesha mchakato wa Katiba Mpya kuanzia ilipoishia Rasimu ya Jaji Warioba, tunakwenda kuchukua yale maoni mliyosema wananchi, tuendelee hapo kwa ajili ya kuipatia nchi katiba mpya na hiyo tutafanya ndani ya siku 100 za kwanza,” amesema Mrema.

Sambamba na hilo, Mrema amesema Serikali ya Chadema itaifufua Tume ya Pamoja ya Fedha za Muungano.

“Serikali ya Chadema itakeleza matakwa yaliyopo sasa kuhusu Tume ya Pamoja na Fedha za Muungano ili kila nchi ipate mgawanyo wa fedha kwa mujibu wa sheria, Zanzibar ipate haki yao,” amesema Mrema.

Kwa upande wa Haki za Binadamu, Ilani ya Chadema inaeleza kwamba serikali yake itapeleka Miswada ya Sheria bungeni kwa dhumuni la kufuta sheria kandamizi zinazokiuka haki za binadamu.

Kwa mujibu wa ilani ya Chadema, Serikali ya chama hicho itaanzisha itapeleka bungeni muswada wa Sheria ya Maridhiano sambamba na kuanzisha Tume ya Maridhiano, ili kuunganisha Taifa.

 “Siku 100 tangu Rais wa Chadema atakapoapishwa, serikali itapeleka bungeni muswada wa sheria ya maridhiano, itaanzisha tume ya maridhiano kwa ajili ya kuondoa hofu ya uwezekano wa vitendo vya kikasi, bila ubaguzi wa kiitikadi, rangi kwa lengo la kuunganisha Taifa ambalo sasa limepa suka pasuka,” amesema Mrema na kuongeza:

“Serikali ya Chadema itaanzisha utaratibu wa mazungumzo kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa lengo la kufikia muafaka juu ya utafutaji na uchimbaji mafuta, gesi , usajili wa meli na uvuvi.”

 Muhtasari wa Ilani ya Chadema unaeleza, serikali ya chama hicho itapunguza kiwango cha marejesho ya mikopo kwa wanufaika wa mkopo wa elimu ya juu, kutoka asilimia 15 wanayotozwa sasa hadi kufikia asilimia 3.

Pia, itatanua wigo wa muda wa kurejesha mikopo wa miaka 25 tangu mnufaika anapopata ajira.

Kwa mujibu wa muhtasari wa ilani hiyo, Serikali ya Chadema itapeleka bungeni muswada wa mabadiliko ya sheria zinazosimamia sekta ya habari, pamoja na kuruhusu vikao vya bunge na mahakama kurushwa mubashara.

“Serikali ya Chadema itarejesha uhuru wa vyombo vya habari ikiwemo kuruhusu kurusha moja kwa moja vikao kamati za bunge na mienendo ya mashauri mahakamani.

“Kama bunge ni wawakilishi wetu wanajificha nini wakati wanajadili kwa niaba yetu sisi wananchi, kwa nini wakae gizani?” amesema Mrema.

Kwenye sekta ya elimu, Ilani ya Chadema inaeleza Serikali ya chama hicho itapeleka bungeni muswada wa Sheria ya Ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi juu ya utoaji elimu bure kuanzia shule ya awali hadi sekondari.

Tundu Lissu (kushoto) akijadiliana jambo na Lazaro Nyalandu

Kuhusu afya, Ilani ya Chadema inaeleza, Serikali yake itashirikiana na sekta binafsi kuweka utaratibu kutoa huduma ya afya za msingi bila malipo, ili kuokoa maisha ya wananchi.

Serikali ya Chadema kwa kushirikiana na sekta binafsi itawekeza katika kuboresha huduma za afya kwa kuongeza ajira za watumishi wa afya, kuboresha miundombinu na vifaa pamoja na  kuhakisha akina mama wajawazito,  watoto,  walemavu na wazee wanapewa kipaumbele cha kwanza katika huduma za afya.

“Fursa za ajira na ujira bora kwa vijana , serikali ya Chadema kwa kushirikiana na sekta binafsi inalenga kufungua fursa za ajira kwa vijana kwa kuboresha mazingira ya ujasiriamali, uwekezaji wa ndani katika sekta za kilimo uvuvi, ufugaji madini ujenzi wa viwanda vya kimkakati na utoaji wa mikopo isiokuwa na mashari magumu,” imeeleza Ilani ya Chadema.

Kuhusu migogoro ya ardhi, Ilani ya Chadema inaeleza “serikali ya Chadema inalenga kumaliza migogoro ya ardhi inayoendelea kuibuka mara kwa mara baina ya wananchi, mamlaka kwa mamlaka, wananchi na mamlaka za hifadhi, kwa kuanzisha mpango rasmi wa umilikishaji ardhi kwa  kila mwananchi na taasisi mbalkimbali.”

Uboreshaji wa miundombinu na maendeleo vijijini kwa kushirikiana na sekta binafsi kwa kuunganisha maeneo ya uzalishaji mali na masoko ya mazao ya kilimo, mifugo, uvuvi ili kukuza uwekezaji vijijini na kuongeza pato la taifa, ni sehemu ya ilani ya Chadema.

Ilani hiyo inaeleza kwamba,  Serikali ya Chadema itahakikisha vyombo vya ulinzi na usalama vinakuwa na zana za kisasa na zinazeondana na wakati, pamoja  na kupewa bajeti ya kutosheleza kwa  ajili ya mavazi, teknolojia na marupurupu.

1 Comment

  • Habari ya kuelekea uchaguzi mkuu ujao!Naomba ilani ya CHAMA CHA DEMOKRASIA NA MAENDELEO maana nimejaribu kuitafuta mtandaoni bila mafanikio

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

BiasharaHabari za Siasa

Zanzibar mbioni kuanza uchimbaji mafuta na gesi baharini

Spread the loveSERIKALI ya Zanzibar, imekamilisha mchakato wa uchimbaji wa mafuta na...

Habari za Siasa

Wizara ya afya yataja mafanikio 10 miaka mitatu Samia madarakani

Spread the loveWIZARA ya Afya imetaja mafanikio 10 iliyoyapata ndani ya miaka...

Habari za Siasa

Mbozi walilia kuwa manispaa, majimbo 3

Spread the loveHALMASHAURI ya wilaya ya Mbozi mkoani Songwe imeeleza dhamira yake...

Habari za Siasa

Wabunge waitaka TPDC kuongeza kasi ya kuunganisha wateja gesi asilia

Spread the love  KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini...

error: Content is protected !!