Thursday , 25 April 2024
Habari za SiasaTangulizi

Ikulu yatuhumiwa

Jengo la Ikulu ya Tanzania
Spread the love

IKULU ya Tanzania, kupitia ofisi ya Katibu Mkuu Kiongozi, imewaandikia wafanyakazi wa iliyokuwa kampuni ya uchapishaji ya Printpak (T) Limited kuwaeleza kwamba suala la madai yao ya kutolipwa stahili zao inavyotakiwa “limehitimishwa.” Inaandika Timu ya Uchunguzi, MwanaHALISI Online.

Kwa mujibu wa barua ya ofisi ya Katibu Mkuu Kiongozi, Kumb. CAB258/536/01/A/9 ya tarehe 19 Julai 2017, serikali imeridhika kuwa ubinafsishaji wa kampuni hiyo iliyokuwa chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara, ulifuata taratibu sahihi zilizo chini ya sheria za Tanzania.

“… malipo ya mafao kwa wafanyakazi walioondolewa kazini mwaka 2001 imebainika kuwa kampuni iliuzwa kwa njia ya ufilisi mnamo mwezi Juni, 2001, kutokana na uzalishaji usiridhisha na kujiendesha kwa hasara.”

Barua hiyo iliyosainiwa na ofisa aliyetambulishwa kwa jina la A.S Mnongane, ambaye amesaini kwa niaba ya Katibu Mkuu Kiongozi, ingawa mtandao umeshindwa kumpata licha ya jitihada mbalimbali, imeeleza:

“Uuzwaji ulifanyika chini ya PSRC kupitia kampuni ya uwalaka wa Ufilisi ya ‘Globe Accountancy Service.’ Wakati inauzwa (Printpak) ilikuwa inadaiwa madeni ambayo yalilipwa kwa kuzingatia sheria ya makampuni, Sura ya 212 kwa kutumia fedha za mauzo zilizopatikana, na Serikali iliwalipa haki na stahili zenu za kisheria ikiwemo mafao ya watumishi wa Kampuni walioondolewa kazini kiasi cha Shilingi 148,215,969. Hivyo mnashauriwa kukubaliana na malipo mliyopata kuwa yalikuwa sahihi na hamkupunjwa mafao yoyote.”

“Kwa maelezo au ufafanuzi uliotolewa hapa juu, suala lenu sasa limehitimishwa,” imeeleza barua hiyo ambayo imepelekwa kwa Benjamin Mhanga ambaye barua inaonesha anatumia simu ya mkononi Na. 0783595412 na Siraji Chaptana aliyetajwa kutumia simu Na. 0756795917.

Kichwa cha maneno cha barua hiyo ambayo imenakiliwa kwa Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha na Mipango, anuani Jengo la Hazina (Treasury Square), 18 Barabara ya Jakaya Kikwete, S.L.P 2802, 40468, mjini Dodoma, kinasema: MALALAMIKO YETU KUHUSU UFISADI KATIKA KUUZA KAMPUNI YA PRINTPAK (T) LIMITED NA WAFANYAKAZI KUPUNJWA MAFAO YAO.

Benjamin Mhanga na Siraji Chaptana, kwa mujibu wa uchunguzi wa Mwanahalisi Online, ni ni miongoni mwa wafanyakazi zaidi ya 300 waliokuwa Printpak, na ambao waliteuliwa kwa ajili ya kufuatilia madai ya kutolipwa mafao stahili kwa mujibu wa sheria na taratibu za ubinafsishaji.

Maelezo ya Mnongane kutoka ofisi ya Katibu Mkuu Kiongozi, yanajibu malalamiko ya wafanyakazi hao yaliyowasilishwa ofisi hiyo kwa barua ya tarehe 10 Agosti 2016 na tarehe 21 Novemba 2016 yakilengwa kumfikia Rais.

Mtandao umepata barua ya awali inayoonesha pia kuandikwa na Mnongane, tarehe 11 Aprili 2017, yenye Kumb. CAB. 258/536/01/97 ikipelekwa kwa Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha na Mipango (wakati huo ikiwepo Mtaa wa Madaraka Na. 1, S.L.P 9111, 11478, Dar es Salaam, na nakala yake kutumwa kwa Katibu Mkuu, Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, anuani NSSF Waterfront, Ghorofa ya Kwanza, 35 Barabara ya Edward Sokoine, S.L.P 9503, 11469 Dar es Salaam.

Ofisa huyo aitwaye Mnongane, anasema kwenye barua yake hiyo, kwamba anawasilisha kivuli vha barua ya Mhanga na Chaptana wakiwakilisha wenzao 306 wa Printpak, wakilalamikia “Ufisadi katika uuzaji wa Shirika la Printpak (T) Limited; wafanyakazi kupunjwa malipo ya mafao yao na kukataa kutekeleza agizo la Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa kina na kuchukua hatua.”

Mnongane ndani ya barua yake hiyo, akibainisha bayana kufanya kazi Ofisi ya Katibu Mkuu Kiongozi, alielekeza ofisi ya Katibu Mkuu “kuwasilisha kwa Katibu Mkuu Kiongozi taarifa kuhusu suala hili.”

Wafanyakazi kadhaa wa iliyokuwa Printpak wamewasiliana na Mwanahalisi Online wakitaka msaada wa kufuatiliwa kwa suala lao baada ya kile walichokiona “hadaa waliyotendewa kupitia wawakilishi wao (Benjamin na Siraji).

“Hatukuridhika na majibu waliyoyaandika Ikulu. Tumeona tuje kuomba msaada kwenu wanahabari kwa sababu hali zetu zimeendelea kuwa ngumu kimaisha kutokana na kuamini tumedhulumiwa na serikali. Wala hatuna tatizo na serikali isipokuwa kufuatilia kwetu huku kunamaanisha kuwa uongozi wa juu kabisa wa serikali yetu usiamini maelezo ya juujuu kwa watendaji wake… ndio maana tumeomba mapema ufanywe uchunguzi wa kina.

“Tukiyapima majibu ya Ikulu, tunapata shaka nyingi. Ni kama vile Rais wetu hajaelezwa undani wa malalamiko yetu, isipokuwa wapo watendaji wa chini yake wanamficha… wanaandika majibu ya kutuondoa njiani. Wanatupa vitisho maana utasemaje suala hili limehitimishwa wakati sisi tunaohusika tunaamini kwa asilimia 100 kwamba hatujatendewa haki na serikali baada ya kudhulumiwa”?

Kiini cha malalamiko ya wafanyakazi wa iliyokuwa Printpak, ni kutolipwa stahili zao inavyotakiwa. Wanalalamika kuwa ubinafsishaji wenyewe uliendeshwa kifisadi huku ukifanywa bila ya kushirikisha viongozi wa lililokuwa tawi la wafanyakazi (TUICO) lililokuwa Printpak, ambao “walitishwa kwa kila namna na menejimenti wasifuatilie maslahi yetu wafanyakazi.”

Kupitia gazeti la MwanaHALISI, ambalo serikali ya Rais John Magufuli imelifungia kwa amri ya Naibu Waziri wa Habari, ya tarehe 19 Septemba 2017, iliwahi kuripotiwa malalamiko hayo kwa njia ya barua ya wasomaji, lakini kulitoka “amri” kwa watendaji wa mlangoni Ikulu kuwanyamazisha wawakilishi hao wawili wa wafanyakazi wa Printpak.

Gazeti la MwanaHALISI huko nyuma liliwahi kuripoti kwa urefu malalamiko ya wafanyakazi wa Printpak wakieleza serikali haikutenda haki katika kushughulikia maslahi yao. Utaratibu wa kubinafsisha ulikiukwa; mali za Printpak zikiwemo majengo mbalimbali ya ofisi, kiwanda na nyumba za kuishi, ziliuzwa kifisadi; serikali ilisamehe visivyo deni la zaidi ya Sh. bilioni moja ililokuwa inadaiwa kampuni ya Tanzania Standard (Daily News); na wafanyakazi walioondolewa walipunjwa kwani baadhi tu walilipwa nauli ya mizigo.

Wafanyakazi wengi waliokuwa Printpak ni wazee, baadhi wakiwa wameshafariki dunia kabla ya kulipwa stahili zao kisheria. Suala hilo lilifika bungeni kwa malalamiko kuwasilishwa Kamati ya Hesabu za Serikali iliyokuwa chini ya uenyekiti wa Zitto Zuberi Kabwe, mbunge wa Kigoma Kusini. Ilipoonekana hakuna hatua madhubuti ya ufuatiliaji baada ya jukumu kuweko Wizara ya Fedha, ndipo lilipofikishwa Ofisi ya Rais (Ikulu).

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

Prof. Muhongo akomalia matumizi nishati jadidifu kuondoa uhaba wa umeme

Spread the love  MBUNGE wa Musoma Vijijini (CCM), Profesa Sospeter Muhongo, ameendelea...

Habari za Siasa

Kilosa yawa mfano wa kuigwa miradi ya Mwenge nchini

Spread the love  KIONGOZI wa Mbio za Mwenge Kitaifa Godfrey Mzava amezitaka...

Habari za SiasaTangulizi

Biteko ataja vipaumbele 7 bajeti nishati 2024/25

Spread the love  NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Mwekezaji amwaga bil. 39 kujenga viwanda 3 vya uchenjuaji

Spread the loveKampuni ya Mineral Access System Limited (MAST) inayoiwakilishwa kampuni ya...

error: Content is protected !!