Friday , 19 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Huyu ndiye Rais Hussein Mwinyi
Habari za Siasa

Huyu ndiye Rais Hussein Mwinyi

Dk. Hussein Ali Mwinyi, Rais wa Zanzibar
Spread the love

DAKTARI Hussein Ali Mwinyi, ameanza rasmi safari ya siku 1826 ya kuwaongoza Wazanzibar. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Dk. Mwinyi ameanza safari hiyo ya miaka mitano leo Jumatatu tarehe 2 Novemba 2020 baada ya kuapishwa na Jaji Mkuu wa Zanzibar, Omar Othuman Makungu kuwa Rais wa visiwa hivyo.

Rais Mwinyi amechukua nafasi ya Rais mstaafu Ali Mohamed Shein, ambaye amemaliza muda wake wa uongozi wa miaka kumi uliopo kwa mujibu wa Katiba aliouanza 3 Novemba 2010 hadi leo 2 Novemba 2020.

Kabla ya kuapishwa kuwa Rais wa Zanzibar, Dk. Mwinyi alikuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.

Safari ya kuwatumikia Wazanzibar aliianza Jumatano ya tarehe 17 Juni 2020 alipojitosa kuchukua fomu ya kuomba uteuzi wa nafasi hiyo ndani ya Chama Cha Mapindiuzi (CCM).

Kuanzia leo hadi 2 Novemba 2025 ni sawa na siku 1826.

Dk. Hussein Ali Mwinyi, Rais wa Zanzibar akiapishwa

Jumla ya wana CCM walichukua fomu ambapo hadi ya mwisho wa mchakato, tarehe 10 Julai 2020, wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM chini ya Mwenyekiti wa chama hicho, John Pombe Magufuli walimpitisha kuwa mgombea urais.

Dk Mwinyi alipitishwa kwa kupata kura 129 (asilimia 78.65) akifuatiwa na Shamsi Vuai Nahodha aliyepata kura 16 na Dk. Khalid Salum Muhamed aliyepata kura 19.

Dk. Mwinyi aliyekuwa mbunge wa Kwahani, aliyezaliwa tarehe 23 Desemba 1966 huko Unguja, Zanzibar, ni mtoto wa Mzee Ali Hassan Mwinyi (Rais wa Pili wa Tanzania).

Katika uchaguzi mkuu uliofanyika tarehe 27 na 28 Oktoba 2020, Dk. Mwinyi alichuana na wagombea wa vyama vingine vya upinzani 16 akiwemo Maalim Seif Sharif Hamad wa ACT-Wazalendo.

Maalim Seif aligombea mara ya sita nafasi ya urais tangu alipofanya hivyo kwa mara ya kwanza 1995, 2000, 2005, 2010 na 2015 wakati zote akiwa CUF na mwaka huu alikuwa ACT-Wazalendo

Dk. Mwinyi alitangazwa mshindi na tarehe 29 Oktoba 2020 na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jaji Hamid Mahmoud Hamid kwa kupata kura 380,402 sawa na asilimia 76.27 ya kura zote 382,402.

Jaji Hamid alisema, Maalim Seif Sharif Hamad wa ACT-Wazalendo alipata kura  99,103 sawa na asilimia 19.87.

Safari yake kwenye siasa

Dk. Mwinyi alijitosa kwenye siasa mwaka 1999 na mwaka mmoja baadaye 2000, akawania Jimbo la Mkuranga mkoani Pwani kupitia Chama Cha Mapinduzi na kushinda.

Alipokuwa mbunge, Rais wa wakati huo, Benjamin Wiliam Mkapa (sasa marehemu) alimteua kuwa Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, alikaa katika wadhifa huo hadi mwaka 2005.

Katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005, Dk. Mwinyi aligombea tena ubunge na safari hii haikuwa Mkuranga bali alirejea nyumbani Jimbo la Kwahani, Zanzibar.

Dk. Mwinyi alichuana na wagombea sita wa vyama vingine lakini kutokana na jimbo hilo kuwa ngome ya CCM, aliibuka mshindi kwa kupata kura 6,239 (asilimia 85.6) akifuatiwa na Mussa Haji Khamis wa CUF aliyeambulia kura 921 (asilimia 12.6).

Kipindi hicho, ilikuwa ni awamu ya kwanza ya Serikali ya awamu ya nne chini ya Rais Jakaya Mrisho Kikwete.

Dk. Mwinyi aliteuliwa kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, alidumu hadi mwaka 2008 alipopelekwa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa alikokaa hadi mwaka 2010.

Aliporejea tena Kwahani mwaka 2010 kusaka ubunge alishinda ambapo Rais wa wakati huo, Jakaya Mrisho Kikwete akamteua kushika Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kabla ya kumpeleka Wizara ya Afya tena mwaka 2012 na miezi 19 baadaye (yaani Januari, 2014), akarejeshwa tena Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.

Dk. Hussein Mwinyi, akiwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa

Baada ya awamu ya Kikwete kuhitimishwa, kwenye uchaguzi mkuu uliofanyika tarehe 25 Oktoba 2015, Dk. Mwinyi aligombea katika jimbo hilo tena, alishinda.

Historia na uwezo wake ulimsukuma Dk. John Pombe Magufuli, Rais wa awamu ya tano alipoingia madarakani tarehe 5 Novemba 2015 kumteua katika baraza lake la mawaziri na kumpa nafasi ya Waziri wa Ulinzi.

Dk. Mwinyi ni miongoni mwa mawaziri wachache wa Rais Magufuli ambao katika kipindi chote cha miaka mitano, hakukumbana na ‘kutumbuliwa’ au kuhamishwa wizara tangu alipoteuliwa tarehe 10 Desemba 2015.

Nini kimemfanya apitishwe na CCM?

Mambo yaliyosaidia kumvusha Dk. Mwinyi kizingiti cha mchujo wa wagombea 31 na hatimaye kuteuliwa ni uzoefu wa kutosha, tena wa kuongoza wizara nyeti kabisa.

Tangu mwaka 2001 hadi leo, Dk. Mwinyi ameweza kuhimili vishindo vya uongozi wa wizara tofauti zikiwamo zile nyeti (Ulinzi na Afya).

Mara zote yalipofanywa mabadiliko ya mawaziri wakati wa Hayati Mkapa, Kikwete hata Dk. Magufuli, yeye aliendelea kuwemo.

Dk. Hussein Mwinyi, akiwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa akiwa bungeni

Kurejeshwa kwake mara kadhaa kwenye Wizara ya Ulinzi kulimfanya aonekane kama mtu anayeijua vizuri nchi hivyo anafahamu mambo mengi nyeti tofauti na wanasiasa wengi.

Hata yeye alipozungumza kabla ya upigaji kura ndani ya CCM ili kumpata mmoja atakayepeperusha bendera ya chama hicho, aliwaeleza wajumbe wa halmashauri kuu kuwa, endapo watamchagua, atahakikisha ana enzi Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar pamoja na Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Dk. Mwinyi alisema, ataendeleza yale yote yaliyoanzishwa na watangulizi wake na ndiyo alivyosema leo baada ya kuapishwa ambapo amemshukuru mtangulizi wake, Dk. Ali Mohamed Shein na kuahidi yale yote aliyoyaanzisha.

Safari ya elimu

Dk. Mwinyi alianza safari yake ya elimu ya Msingi jijini Dar es Salaam kati ya mwaka 1972 – 1976, Shule ya Msingi Oysterbay, Dar es Salaam.

Kati ya mwaka 1984–1985 wazazi wake walimhamishia Misri na akasoma katika Shule ya Msingi “Manor House Junior” ambako alihitimu elimu ya msingi.

Shule hii ilikuwa na hadhi ya “Middle School za Tanzania” kwa wakati huo. Mwinyi alipelekwa Misri kwa sababu baba yake, Ali Hassan Mwinyi, alikuwa balozi wa Tanzania nchini Misri wakati huo.

Aliporejea Tanzania, alipelekwa Shule ya Sekondari Azania na kuendelea na masomo ya kidato cha kwanza hadi nne mwaka 1982 – 1984.

Alipohitimu kidato cha nne alipelekwa Shule ya Sekondari Tambaza kusoma kidato cha tano peke yake mwaka 1984 -1985.

Dk. Mwinyi tangu zamani ni mtu wa kupenda kusaidia watu, aliomba na kuchaguliwa kusomea utabibu wa binadamu. Alianza masomo ya udaktari nchini Uturuki mwaka 1985, kwenye Shule ya Utabibu ya Chuo Kikuu cha Marmara na kuhitimu Shahada ya Utabibu wa Binadamu mwaka 1992.

Kwa sababu hakumaliza kidato cha sita, alipokuwa huko ughaibuni alipitia masomo ya mwaka mmoja ya kujiandaa na udahili wa Chuo Kikuu “Pre University Studies.”

Chuo cha Marmara kinapokea hata wanafunzi wa kidato cha nne kuanza kusomea shahada ya utabibu, lakini lazima wapitie mwaka mmoja wa maandalizi kama alivyofanya Dk. Mwinyi.

Alipohitimu shahada ya kwanza, alirejea Tanzania na kufanya kazi kwa mwaka mmoja katika Hospitali ya Taifa Muhimbili. Mwaka 1993, Dk. Mwinyi aliendelea na masomo ya juu ya utabibu kwa kuunganisha.

Rais John Magufuli akizindua kitabu cha Rais Mstaafu Benjamin Mkapa, wengine ni wastaafu, Jakaya Kikwete na Ali Hassan Mwinyi

Safari hii akipelekwa Uingereza katika Hospitali ya Hammersmith ambako alihitimu shahada ya uzamili ya utabibu mwaka 1994 na kuunganisha shahada ya uzamivu ya udaktari hapohapo Hammersmith na kuhitimu mwaka 1997.

Alirejea nchini kwa mara nyingine na kufanya kazi katika Hospitali ya Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Herbert Kairuki (HKMU) kwa miaka miwili hadi mwaka 1999.

Mwaka 2000, Dk. Mwinyi alizidisha nguvu yake ndani ya CCM kwa kugombea ujumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC), akashinda na mwaka 2007 aligombea tena NEC na kushinda.

Marais waliomtangulia

Dk. Mwinyi ameapishwa kuwa Rais wa nane wa Zanzibar tangu kulipofanyika Mapinduzi Matufuku tarehe 12 Januari 1964.

Marais wengine walimtangulia na miaka yao kwenye mabano wa kwanza ni;  Abeid Karume (26 Aprili 1964- 7 Aprili 1972), Aboud Jumbe (7 Aprili 1972- 30 Januari 1984), Ali Hassan Mwinyi (30 Januari 1984- 24 Oktoba 1984), Idris Abdul Wakil (24 Oktoba 1985- 25 Oktoba 1990).

Salmin Amour (25 Oktoba 1990- 8 Novemba 2000), Aman Abeid Karume (8 Novemba 2000- 3 Novemba 2010) na Dk. Ali Mamohed Shein aliingia 3 Novemba 2010 hadi leo Jumatatu anapokabidhi madaraka kwa Dk. Mwinyi.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

Tume huru ya uchaguzi yatangaza ajira watendaji daftari wapiga kura

Spread the love  TUME Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), imetangaza nafasi...

Habari za SiasaTangulizi

Chadema yatangaza ruti awamu ya pili maandamano

Spread the love  CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimesema awamu ya...

Habari za Siasa

CCM yamkana mwenyekiti UVCCM aliyetaka wapinzani wapotezwe

Spread the love  CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimejitenga na kauli ya mwenyekiti...

Habari za SiasaTangulizi

Rais Samia kutunukiwa udaktari wa heshima Uturuki

Spread the loveBaraza la Chuo Kikuu cha Ankara, ambacho ni cha pili...

error: Content is protected !!