Thursday , 25 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Huu ndiyo ugonjwa uliosababisha kifo cha Mwalimu Bilago
Habari za Siasa

Huu ndiyo ugonjwa uliosababisha kifo cha Mwalimu Bilago

Spread the love

MWALIMU Kasuku Kasuku Bilago (54), mbunge wa Buyungu, wilayani Kakonko, mkoani Kigoma (Chadema), aliyefariki dunia Jumamosi iliyopita na kuzikwa jana Jumatano. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Mwalimu Bilago amekutwa na mauti, kwenye hospitali ya taifa ya Muhimbili, alikokuwa akipatiwa matibabu.

Alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa kuota kinyama sehemu ya haja kubwa unaofahamika kwa jina la hemorrhoids au piles-(bawasiri).

Mwalimu Bilago alipelekwa Muhimbili Jumatano iliyopita – tarehe 23 Mei – ili kupatiwa ya matibabu ya ugonjwa huo. Amekuwa akisumbuliwa na ugojwa huo kwa takribani wiki mbili.

Bawasiri, ni ugonjwa unaosababishwa na kuathirika kwa mishipa ya damu ya ndani na nje ya sehemu ya haja kubwa.

Wanaopatwa na ugonjwa huu, huwasababisa kuvuja damu kutokana na kupasuka mishipa kwenye njia ya haja kubwa; na kumfanya mgonjwa kutoka kinyama au uvimbe.

“Tatizo hilo huwaathiri watu wote, lakini zaidi watu wazima. Karibu asilimia 50 ya watu wote wako katika hatari ya kupata tatizo hili katika umri wa miaka 30 na 50,” ameeleza daktari bingwa mkoani Dodoma ambaye hakupenda kutajwa jina.

Akizungumzia msiba huo, mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Zuberi Kabwe amesema, amepokea kwa mshutuko mkubwa kifo cha Mwalimu Bilago.

Zitto anasema,“…Kigoma tumepata pigo lingine. Mwalimu Kasuku Bilago, amefariki dunia. Ni uchungu usioelezeka kumpoteza kiongozi huyu aliyekuwa na mapenzi ya dhati kwa mkoa wetu, nchi yetu na taaluma ya ualimu.”

Alisema, “Mungu amlaze mahala pema peponi ndugu yetu…”

Kabla ya kupelekwa jijini Dar es Salaam, Mwalimu Bilago alipatiwa matibabu katika hospitali ya DCMC iliyoko eneo la Nyuka, mjini Dodoma, ambako alifanyiwa upasuaji.

Katika uwanja wa ndege wa Dodoma, mbunge huyo alisindikizwa na baadhi ya wabunge wenzake pamoja na maofisa kutoka ofisi ya Bunge.

Miongoni mwa wabunge waliokuwapo uwanja wa ndege kumsindiza, ni pamoja na mbunge wa Ubungo, Saed Kubenea; mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche na mbunge wa viti Maalum mkoani Dodoma, Immaculate Sware Semesi.

Wengine waliokuwapo, ni mbunge wa Viti Maalum mkoani Geita, Upendo Peneza, mbunge wa Viti Maalum kutoka Zanzibar, Mariam Msabaha na Gimbi Masaba, mbunge wa Viti Maalum kutoka mkoani Simiyu.

Akizungumza kwa taabu wakati akitolewa kwenye gari la wagonjwa ili kupandishwa ndege, Mwalimu Bilago aliwataka wabunge wenzake walioko Dodoma kuendeleza kile alichokiita, “mapambano ya ukombozi wa wananchi.”

Alisema, “…nakwenda Dar es Salaam kupata matibabu. Nawaombeni sana mniombee kwa Mungu ili niweze kupona haraka. Niombeeni ili niweze kuungana nanyi mapema zaidi katika harakati hizi.”

Aliongeza, “ninawaacha hapa nikiwa na ombi moja kwenu. Endelezeni mapamba haya ya kuwakomboa wananchi na udhalimu wa CCM (Chama Cha Mapinduzi) na serikali yake hadi haki ipatikane. Msikubali kurudi nyuma.”

Akijibu kauli ya Bilago, Kubenea alisema, “nenda katibiwe Mwalimu. Sisi tutafanya pae ulipoishia. Usihofu.”

Alisema, “hatutakuangusha. Tutafanya kama unavyoelekeza. Tunakuombea na Mungu atajalia utarejea ukiwa mzima na mwenye afya tele.”

Kwa mujibu wa taarifa za kitabibu, kuna aina mbili za ugonjwa huu – bawasili ya ndani na bawasili ya nje.

Bawasili ya ndani, hutokea ndani ya mfereji wa haja kubwa na yaweza kumtokea bila kuambatana na maumivu. Wengi hawafahamu kuwa wanasumbuliwa na tatizo hilo.

“Aina hii hutokana na kuvimba na kuharibika kwa mshipa wa ndani katika mfereji wa haja kubwa. Hutokea wakati wa haja na kurudi yenyewe ndani baada ya kujisaidia; kuna Bawasiri ambayo huwa ngumu kurudi,” anaeleza.

Akizungumzia Bawasili ya nje, mtaalamu huyo wa utabibu anasema, hutokea katika eneo la mwisho kabisa la mfereji wa haja kubwa,

Anasema, aina hii ya Bawasiri, huambatana na maumivu makali na muwasho wa ngozi katika eneo la tundu.

Anasema, “hapa mishipa ya damu (vena) hupasuka na damu kuganda na kasababisha aina ya bawasiri iitwayo Thrombosed hemorrhoids.”

Anasema, chanzo halisi cha ugonjwa huu hakijapatikana. Hata hivyo, anasema kuna vitu vinavyotajwa kusababisha ugonjwa huo.

Anataja vitu hivyo, kuwa ni pamoja na kuharisha kwa muda mrefu, kutopata choo, umri mkubwa, mtu kuwa na uzito mkubwa na kukaa kitako kwa muda mrefu.

Dalili za ugonjwa huo, ni ngozi kuwasha katika eneo la tundu la haja kubwa; kupata maumivu makali wakati wa kujisaidia na uvimbe katika eneo la tundu la haja kubwa.

Nyingine, ni kutoka kinyama katika eneo la tundu na kinyesi kuwa na damu na kunuka; matibabu ya Bawasiri hutegemea aina ya Bawasiri iliyompata mgonjwa.

“Lakini tiba iliyozoeleka, ni kukatwa kinyama na kuendelea na lishe ya chakula. Hata hvyo, tiba hii si nzuri kwa sababu huwa haitibu chanzo cha tatizo na hivyo huwa rahisi ugonjwa kujirudia,” anaeleza mtabibu.

Anasema, “tiba nzuri ni kutumia dawa ambayo hubandikwa mahali penye tatizo.

Anasema, “pamoja na hayo, Bawasiri ni ugonjwa unaoweza kuepukika kwa kula mbogamboga, matunda na nafaka zisizokobolewa.”

Mwalimu Bilago alikuwa mwiba mkali kwa serikali bungeni kutokana na uwezo wake mkubwa wa uchambuzi wa bajeti, hasa katika suala la elimu.

Akichangia bajeti ya wizara ya elimu katika mkutano wa Bunge uliyopita, Mwalimu Bilago ambaye kitaaluma ni mwalimu alieleza kwa kina sababu za wanafunzi wa shule binafsi kufaulu na shule za umma kutofanya vizuri.

Taarifa tulizozipata wakati tukienda mitamboni zinasema, kuna uwezekano mkubwa Mwalimu Bilago akazikwa kesho kutwa Alhamisi, kufuatia kuibuka kwa “mvutano kati ya chama chake na uongozi wa Bunge.”

Mvutano wa sasa unatokana na hatua ya Chadema kupanga kumzika mbunge wake Alhamisi huku Bunge likipanga msiba kufanyika siku ya Jumatano.

Mbali ya kuwa mbunge, Mwalimu Bilago alikuwa mwenyekiti wa Chadema wa Kanda ya Magharibi na Mjumbe wa Kamati Kuu (CC) ya chama hicho.

Mwalimu Samson Kasuku Bilago, alizaliwa tarehe 2 Februari mwaka 1964.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

Kilosa yawa mfano wa kuigwa miradi ya Mwenge nchini

Spread the love  KIONGOZI wa Mbio za Mwenge Kitaifa Godfrey Mzava amezitaka...

Habari za SiasaTangulizi

Biteko ataja vipaumbele 7 bajeti nishati 2024/25

Spread the love  NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Mwekezaji amwaga bil. 39 kujenga viwanda 3 vya uchenjuaji

Spread the loveKampuni ya Mineral Access System Limited (MAST) inayoiwakilishwa kampuni ya...

Habari za SiasaTangulizi

Mpwa wa Magufuli mbaroni kwa kusambaza picha za utupu

Spread the loveJESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limewakamata...

error: Content is protected !!