Saturday , 20 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Hivi ACT-Wazalendo inawachoma CUF, CCM, Ofisi ya Msajili?
Habari za Siasa

Hivi ACT-Wazalendo inawachoma CUF, CCM, Ofisi ya Msajili?

Spread the love

BARUA ya Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini iliyotoka na kusambazwa jana tarehe 25 Machi 2019 kwenye mitandao ya kijamii na vyombo vya habari imezua mjadali mpana. Anaandika Mwandishi Wetu …(endelea).

Wapo wanaoshangazwa na vitisho vya msajili dhidi ya chama kinachoibuka kwa kasi nchini ACT-Wazalendo, wanaojadili mshangao huo wanaamini msajili anashindwa kuzuia mihemuko yake.

Hatua ya msajili kuivaa ACT-Wazalendo imetanguliwa na malalamiko kutoka Chama cha Wananchi (CUF) kwamba, bendera zao zinachomwa, CUF walikwenda mbali zaidi kwa kuomba Ofisi ya Msajili ifute usajili wa Chama cha ACT-Wazalendo.

Chama Cha Mapinduzi (CCM) nacho kikapokea mvumo wa zumari kutoka CUF. Dk. Bashiru Ally, Katibu Mkuu wa CCM alipokuwa katika Uzinduzi wa Mkakati Maalum wa CCM wa kukomaza demokrasia nchini uliofanyika jijini Dodoma mwishoni mwa wiki iliyopita, alitoa malalamiko yale yale ya CUF kuhusu kuchomwa kwa bendera zake.

Sasa imekuwa zamu ya Ofisi ya Msajili kutoa tuhuma kuhusu kuchomwa bendera za CUF. Taasisi hizo tatu (CUF, CCM na Ofisi ya Msajili) zimetoa tuhuma zinazofanana.

Hii ni sehemu ya barua yake msajili Jaji Francis Mutungi; “Aidha, baada ya Mahakama Kuu kutoa uamuzi wa kesi Na. 23 ya mwaka 2016, iliyokuwa inahoji uhalali wa Profesa Ibraimu Lipumba, Machi 18 mwaka huu, kumekuwa na matukio ya uvunjifu wa sheria.

“… ikiwamo kuchoma moto bendera za CUF, uliofanya na mashabiki wa aliyekuwa Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif, wanadai sasa ni wanachama wa ACT. Kitendo cha kuchoma bendera ya chama cha siasa ni kukiuka kifungu cha 11C, cha sheria ya vyama vya siasa.”

Kwenye barua hiyo msajili amekumbushia onyo lake la tarehe 18 Machi 2019 mwaka huu akikemea kitendo cha wananchi wa ACT-Wazalendo kutochukua hatua ya kukemea suala hilo, akisema chama hicho kimeafiki au kilitoa maelekezo kufanyika kwa vitendo hivyo.

“Kutokana na maelezo hayo, vitendo hivyo vinaakisi ukiukwaji wa dhahiri wa Sheria ya Vyama vya Siasa ambao pia unasababisha chama chenu kupoteza sifa za usajili wa kudumu.

“Hivyo, Msajili wa Vyama vya Siasa anatumia fursa hii kukufahamisha wewe na wanachama wa ACT-Wazalendo nia yake ya kufuta usajili wa kudumu wa chama chenu kwa sababu hizo zilizotajwa,” imeeleza barua ya msajili.

Swali linaloibuka hapa ni kwamba, waliochoma bendera za CUF walikuwa wanachama wa CUF ama ACT-Wazalendo.? Hapa Jaji Mutungi asaidiwe.

Amesema, waliokuwa wanamuunga mkono Maalim Seif ndio waliochoma bendera hizo; sawa lakini je wakati wanafanya hivyo walikuwa wanachama wa chama gani?

Muda mfupi baada ya Maalim Seif kuhama, waliochoma bendera hizo walikuwa bado ni wanachama wa CUF. Hawa wanaweza kufanya hivyo kutokana na CUF kushindwa kutatua mgogoro wake na hata Maalim Seif akaamua kuondoka, njia ya kuonesha hasira zao kwa chama chao (CUF) ikawa kuchoma bendera.

Ama walifanya hivyo kwa kuonesha kuchoshwa na chama chao wenyewe kutokana na sababu wanazoweza kujua wenyewe, lakini jambo a kuzingatia hapa ni kuwa, wakati wanafanya hivyo walikuwa ni wafuasi ama wanachama wa CUF.

Kama hivyo ndivyo, ACT-Wazalendo inawajibikaje kwa wafuasi wa CUF kuchoma bendera zao wenyewe? ACT-Wazalendo wanayo mamlaka gani ya kuingilia hisia za wanachama wa CUF kwa kile wanachokitenda kuonesha hisia zao?

Msajili anawezaje kuituhumu na hata kufuta Chama cha ACT-Wazalendo kwa vitendo vilivyofanywa na wafuasi wa CUF? Hapa busara inahitajika.

Jaji Mutungu anapaswa kusimama katika haki. Njia rahisi ya kuonesha anasimamia haki ni kufafanua moja ya hoja zake kwamba, waliochoma bendera za CUF ni wanachama ACT-Wazalendo.

Jaji Mutungi anapaswa kujua kwa dhati kabisa taasisi yake anaweza kuitumia vizuri, nchi ikabaki salama ama anaweza kuiendesha kwa namna ambavyo nchi ikatumbukia kwenye matatizo. Busara yake ndio mafanikio ya taifa letu katika utulivu wa kisiasa.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

Dk. Mwakyembe : Zanzibar waliongoza kutaka Serikali 2 za muungano

Spread the love  MWANASIASA mkongwe nchini, Dk. Harrison Mwakyembe, amesema mjadala wa...

Habari za SiasaTangulizi

Rais Samia ataja mikakati ya kufikia trilioni 2 biashara Uturuki, Tz

Spread the loveWakati Tanzania na Uturuki zikidhamiria kuongeza kiwango cha biashara hadi...

BiasharaHabari za Siasa

Mavunde aagiza Perseus kuharakisha fidia Sengerema

Spread the loveWaziri wa Madini, Anthony Mavunde ameipongeza Kampuni ya Perseus kwa...

Habari za Siasa

Kigogo Chadema awanyooshea vidole vigogo serikalini kuhusu ripoti ya CAG

Spread the love  MWANACHAMA wa Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Boniface Jacob, amedai...

error: Content is protected !!