BODI ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu Tanzania (HESLB) imetangaza mwongozo wa utoaji mikopo na ruzuku kwa mwaka wa masomo wa 2019/2020. Anaripoti Regina Mkonde … (endelea).
Akizungumza na wanahabari leo tarehe 4 Juni 2019 jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Abdul-Razaq Badru amesema katika mwongozo huo kuna mabadiliko kadhaa ikiwemo kwenye sifa za waombaji, utaratibu wa kuomba mikopo na maelekezo mengine muhimu.
Badru amesema kutangazwa kwa mwongozo huo ni maandalizi ya kukaribisha maombi ya mikopo kwa mwaka ujao wa masomo wa 2019/2020, mchakato unaotarajiwa kuanza tarehe 15 Juni hadi 15 Agosti 2019.
Akitangaza mabadiliko hayo, Badru amesema wanafunzi husika hawatakiwi kuwa na chanzo kingine cha kugharamia masomo yake pamoja na kuwa na vyeti ikiwemo cha kuzaliwa na cha kifo cha mzazi, vilivyothibitishwa na Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) au Mamlaka ya Usajili wa Matukio ya Kijamii Zanzibar.
“Muombaji awe amepata udahili katika chuo kinachofahamika, lazima asiwe na chanzo kingine cha kugharamia masomo yake. Vyeti vya kuzaliwa au cheti cha kifo cha mzazi wake kiwe kimethibitishwa na Wakala wa Usajili wa Matukio ya Kijamii Zanzibar au RITA,” amesema Badru.
Badru amesisitiza kuwa, muombaji atakaye ambatanisha cheti kisichothibitishwa na mamlaka hizo atakosa vigezo vya kupata mkopo.
Amesema lengo la kuweka sharti hilo ni kudhibiti mianya ya udanganyifu kuhusu cheti cha kuzaliwa na cheti cha kifo cha mzazi.
“Kuna mamlaka za kiserikali zimepewa mamlaka ya kuthibitisha cheti cha kuzaliwa, sababu wakati mwingine kinaweza kughushiwa, lazima kila mwanafunzi aambatanishe cheti cha kuzaliwa na kama atakaye ambatanisha ambacho hakijathibitishwa, hicho hakiwezi kutumika wakati wa kutizama maombi yake na vile vile cheti cha kifo,” amesema Badru.
Leave a comment