Wednesday , 24 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Zitto kuvuliwa Ubunge, zigo aachiwa AG
Habari za SiasaTangulizi

Zitto kuvuliwa Ubunge, zigo aachiwa AG

Zitto Kabwe, Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalando
Spread the love

JOB Ndugai, Spika wa Bunge, ameanza kuchonga njia ya kumvua ubunge Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe. Anaripoti Danson Kaijage, Dodoma … (endelea).

Spika Ndugau baada ya kusikiliza hoja za wabunge, amehitimisha kwa kulihamisha sakata la Zito kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Prof. Aderlardus Kilangi, kuangalia kama suala hilo lina ujinai ndani yake au la.

Sakata hilo limetokana na mbunge wa Siha, Dk. Godwin Mollel kuomba kutoa hoja ya kuhailisha Bunge kwa ajili ya kujadili jambo la dharura.

Dk. Mollel akiwa bungeni alianza kwa kusema: “Mheshimiwa Spika nasimama kwa kanuni ya 47 (1) ili kuomba kuahirisha shughuli za Bunge ili kujadili jambo la dharura. Hapa juzi mwenzetu Zitto ameandika barua kwenye Benki ya Dunia na kuiomba benki hiyo zizuie fedha ambazo zingekuja kusaidia elimu Tanzania.

“Lakini wa kiasi cha fedha kingeweza kutumika kujenga shule tano kubwa kwa kila wilaya, lakini tungeweza kuwaweka bwenini watoto zaidi ya 2,000 wa kike ambao mwisho wa siku hata kiwango cha mimba kwa taifa letu kingeshuka.

“Lakini ikumbukwe Mheshimiwa Spika tumeapa hapa bungeni kwa kutumia Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na katiba hiyo imetaja dhahiri maadui wa taifa letu ikiwemo umasikini, ujinga na maradhi.

“Na ukigusa kwenye eneo hili la elimu ina maana umefuta ujinga, umaskini na maradhi, sasa kwa kutumia na kwa sababu amevunja katiba yetu, sujui utuelezaje kwa sababu hii ni tabia tunatakiwa sasa tutafute namna ya kuishughulikia kwenye taifa letu.”

Dk. Mollel aliomba kutoa hoja hiyo na kuomba wabunge wenzangu wamuunge mkono ili waone sababu kwani hata Marekani wamemjadili Rais wa pale tu alipoonekana haaminiki anapotoka nje ya mataifa mengine kuhusu maslahi ya taifa lao, lakini Mbunge mwenzetu anazunguka duniani ‘ku-sabotage’ taifa hili kiuchumi na kuathiri usalama.

Baada ya Dk. Molleli kutoa hoja yake Mbunge wa Viti Maalum, Salome Makamba (Chadema) alisimama na kuomba kuhusu utaratibu. “Nasimama kwa kanuni ya 48 (4) ambayo inasema jambo lolote haitahesabiwa kuwa ni lenye maslahi kwa umma iwapo utatuzi wake unategemea hatua zaidi kwa utekeezaji peke yake.

“Jambo alilolieta Mbunge mwenzangu Dk. Mollel kwanza tu wengine hatuna taarifa lakini pili jambo hili lina utaratibu wake mahususi, kwa sababu hizo kulileta ndani ya Bunge hili kama hoja ya dharura ni kukiuka kanuni.

“Kwa hiyo kama Dk. Mollel anadhani kwamba Mheshimiwa Zitto Zuberi Kabwe amekiuka utaratibu wa kibunge na jambo hili linatakiwa kushughulikiwa zipo njia za kisheria zinazoweza kushughulikia jambo hilo hivyo basi alipeleke kwenye vyombo vya kisheria badala ya kuleta kama hoja ya dharura ndani ya Bunge lako tukufu,” alieleza Mollel.

Akijibu hoja hiyo, Spika Ndugai amesema: “Navyoipima hapa hoja hii ni nzito maana ni hoja inayohusu usaliti kwa taifa kwa kadri lilivyotolewa na Mheshimiwa Mollel umesahau kusema nembo ya Bunge imetumika kufikisha ujumbe huo huko.

“Kwa hiyo kwa maana ya kanuni gani imevunjwa, basi liko swali hapa kama kuna kuvunjwa lakini is it okay?”alisema Ndugai na kuruhusu wajumbe kuchangia hoja hiyo.

Hamidu Bobali, Mbunge wa Mchinga, (CUF)

“Kama nimemuelewa Dk. Mollel amezungumza kwamba, Mbunge mwenzetu ameandika barua na mheshimiwa Spika mimi sijapata bahati ya kuona hiyo nakala ya barua, lakini nijuavyo pamoja na kuwa Mheshimiwa Zitto ni Mbunge ni kiongozi wa chama cha siasa, inawezekana kwenye nakala ya barua aidha amesaini kama kiongozi mkuu wa chama kama Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya  Muungano wa Tanzania.”

Peter Lijualikali, Mbunge wa Kilombero (Chadema)

“Hoja anayoileta Dk. Mollel kusema kwamba Benki ya Dunia imeinyima kwa sababu ya Zitto, kwanza ilipaswa Serikali ndio  ituambie, kwanza iadmmit ni kweli kwamba imenyimwa fedha hizi kwa sababu ya Zitto? Ni kweli kwamba tumenyimwa kwa sababu Zitto kasema?

“Serikali sijaona ime admit anywhere, sasa hoja hii inatoka wapi? wakati serikai haijasema chochote, hebu tujiulize Zitto alivyozungumza labda ni vya uongo, vipi? mpaka mabeberu hao wakakubali? mimi nataka serikali iseme kwamba Zitto amesababisha haya yote? Kila siku serikali inasema ina hela leo mnalalamika mnanyimwa hela mnakwana sasa.”

David Silinde, Mbunge wa Momba (Chadema)

“Kabla Bunge halijaingia katika mjadala ilikuwa ni vizuri sasa kwa serikali itoe maelezo juu ya jambo hilo, kwa sababu tunaona kwenye instagram, whatsaap na twitter kwamba hela zimezuiliwa.

“Mimi siamini kwamba serikali inafanyia kazi taarifa za mitandao haya yanayotokea nafikiri kikubwa kwanza tusubiri serikali itoe taarifa, kwa sababu kama ni kweli maana yake obviously kuna hatua ambazo sisi kama Bunge tutakuja kuzichukua.

“Mimi nilikuwa nataka kwamba Bunge lituelekeze kwa maana ya serikali alafu baada ya hapo tutakuwa kwenye nafasi nzuri ya kuchangia.”

Ally Kessy, Mbunge wa Nkasi (CCM)

“Zitto ametoa sababu kwamba akitaka Benki ya Dunia iinyime mkopo Tanzania kwa sababu watabagua wanawake. Kwa sababu anataka wanawake wenye mimba waliopewa mimba mashuleni waendelee na masomo. Uzinifu haukubaliki kabisa na Uislamu haikubali kabisa kuzini.

“Tumeshuhudia watoto wanaopata mimba ni watoto chini ya miaka 14 mpaka 16, ndio wamezidi zaidi nashangaa na akina mama wanasimama hapa. Mheshimiwa Salome wanasapoti kitu kama hicho na anapinga mtoto asiolewe chini ya miaka 18. Mnataka tuongeze watoto wa barabarani na  mitaani?

“Tukubaliane  hapa nani alikwenda shuleni akiwa na mtoto ananyonyesha, yuko wapi? Leo Zitto Kabwe anataka kutuletea masharti ya ajabu ajabu , hii nchi ni hatari. Ametangaza kabisa amesema mkopo tumenyimwa kwa sababu utabagua watoto wa  kike wajawazito wasiende mashuleni, Ndugu zangu huyu ni mtu hatari, haikubaliki.”

Alhaji Abdalah Bulembo, Mbunge wa Kuteuliwa (CCM)

“Usaliti, mkiwa vitani akitoka mtu mmoja akapeleka habari zenu upande mwingine hatakiwi kuvuka mpaka anatakiwa auawe hukuhuko alipo, anachokifanya Zitto ni usaliti mkubwa katika nchi yetu.

“Sasa nafasi ya kuvumilia mheshimiwa spika mimi si mwanasheria sijui taratibu za kibunge mbunge anapoisaliti nchi anatakiwa kurudi bungeni humu? hatakiwi huyu ni msaliti na Serikali mko pale na wanasheria lazima mnatakiwa kuliagalia”

“Wanasheria wapo humu hawa wasaliti wanaotoka Tanzania kwenda nje kuisaliti nchi yetu, mnaruhusuje passport zao kurudi nchini si warudie polisi pale ili tujenge heshima katika nchi? Mheshimiwa spika huyu bwana kazoea anatakiwa apate kiboko kizuri sana.”

Janeth Mbene, Mbunge wa Viti Maalum (CCM)

“Mimi kusema kweli bila hata kusema Serikali imesemaje au nini, ningependa kwanza kitu kinachonigusa ni maslahi ya taifa mtu anapotamka jambo lolote lile hasa anapokuwa kiongozi lazima ajiulize hii inasaidia vipi taifa langu.

“Kitendo alichokifanya mwenzetu Zitto ni usaliti lakini vilevile wazungu wanasema hakufikiria vizuri juu ya hili jambo. Nimemsikia BBC kwenye dira ya dunia kwa hiyo kitu ninachokiona ni kwamba amekuwa akitumia fact lakini anazitwist ili kujenga hoja ambayo ana ajenda nayo yeye na niliyoiona mimi ni ya kisiasa zaidi.

“Kutofautiana mitazamo kuhusu wanafunzi wanaopata ujauzito wakiwa shuleni haimpi uhalali yeye wa kwenda kufanya usaliti alioenda kuufanya lakini vilevile kitu ambacho mimi nilikiona kwa haraka sana na nikaona huu ni upotoshaji mkubwa ni kuzungumzia vile vyuo vya kijamii kuwa ni vya CCM.”

Mary Chatanda, Mbunge wa Korogwe Mjini (CCM)

“Ztito ni msaliti maana ametusaliti sisi wabunge kwa kutumia nembo ya Bunge kinyume kabisa na sheria, kwa sababu ipo kisheria sisi kama wabunge hatukumtuma kwenda kuandika aliyoandika kwa kutumia nembo ya bunge letu.

“Kwa hiyo mheshimiwa spika mimi nilikuwa nafikiri kwamba ndugu Zitto angeweza kutumia nembo ya chama chake au yeye binafsi bila kutumia ya bunge, mwenzetu huyo Zitto ametusaliti ni vizuri akapewa adhabu inayostahili.”

Stanslaus Mabula, Mbunge wa Nyamagana CCM

“Moja ya jukumu letu ni kuisaidia nchi hivyo kinga ni bora kuliko tiba, ifike sehemu wabunge tuondokane na hali ya ushabiki ambapo Bunge lazima lichukue hatua tufike sehemu kama wabunge tundokane na ubunge ambao hauwezi kutusaidia kama nchi.

“Maana fedha hizo zingetolewa zingesaidia kwa maana hiyo tungeepukana na kila mbunge anayesimama hakilia na habari ya maboma kwenye jimbo lake tumelia hapa kuhusu vyumba vya madarasa havitoshi watoto kidato cha kwanza hawajapokelewa.

“Serikali imefanya jitihada imepata wadau WB imekubali kuunga mkono jitihada kubwa zinazofanywa na serikali wapo tayari kutoa fedha leo mtu mmoja tuu anakwenda kuanza kupotosha taarifa hizi za upatikanaji wa fedha.

“Bunge kama lina namna ya kuchukua hatua ni lazima tufanye kazi iwe kazi ya kujenga nchi na sio kubomoa lazima tutoke huko.”

Alhaji Juma Nkamia, Mbunge wa Chemba (CCM)

“Zitto ni mbunge mwenzetu na hizi fedha pia zingeenda kusaidia wananchi wa Kigoma anakotoka yeye, lakini kwa lugha nyepesi tuu watu wa namna hii wanaitwa Massinaries yuko tayari kufanya lolote kwa sababu analipwa.

“Na mimi nimemshangaa mbunge mwenzangu mmoja pale (Salome) anasema kwamba Zitto pengine amezungumza kama kiongozi wa kisiasa ametumia nembo ya bunge siyo ya chama chake, na mimi nimeshangaa hata waliokuwa wanamhoji hawakuwa makini, vyuo hivi vya maendeleo ni vya Serikali na Zitto anajua na dunia inajua.

“Nukuu: Mwalimu Nyerere aliwahi kusema massinaries wana tabia ya kimalaya malaya na alisema tutawasaka watu wenye tabia za kimalaya malaya mpaka tuwamalize. Sasa hili alilofanya Massinary (Zitto) ni umalaya malaya wa kisiasa na matokeao yake tukiendekeza watu wa namna hii tutakwenda pabaya, nina uhakika hata alipokuomba kibali cha kusafiri nje hakusema anakwenda kufanya nini.

“Wamarekani mtu ambaye anasaliti taifa lao huwa wanamsaka hivyo nikuombe tufike hatua watu wa aina hii wanaoyumbisha nchi wachukuliwe hatua.”

Akijibu michango ya Wabunge Spika Ndugai alisema: “Kwakweli kama Spika tunasikitika kwa mambo ya namna hii na spika mstaafu mama Makinda ametoka hapa juzi kama mtakumbuka maneno yake akiwa mtu mzima ametuasa hasa wabunge vijana kwamaba katika taifa lolote utaifa ni jambo la kwanza.

“Kuona fahari kwenda nje na kuisaliti nchi yako ni jambo ambalo si sawa mkopo huo unahusiana na kuja kuboresha elimu ingekuwa ni jambo fulani jingine nitoe mfano gani sijui kitugani Kongwa ukitaka kuhoji hata umoja wa mataifa sawa.

“Sisi wabunge tunajua jinsi tulivyo na matatizo makubwa ya elimu kuna shule za sekondari baadhi yake watoto wanakalia vigoda vya miguu mitatu hawana madawati nyingine hazina vyoo.

“Ninapomsikia mtu anasema Benki ya Dunia wasitoe fedha serikali ikapata ili tuboreshe elimu, nashindwa hata kuelewa tatizo ni nini, hata uwe mpinzani vipi kuna mahali ambapo kidogo unasita, ndiyo maana Rais wa Marekani Trump (Donald), hivi sasa yupo kwenye lile bunge la juu baada ya kuhukumiwa lile bunge la wananchi wa Marekani.

“Kosa lake nini anashirikiana na nchi ya kigeni katika masuala ambayo yanaathiri interest za nchi yake, sasa sisi mbunge wetu anafanya makosa kama ya Trump kwa hiyo mimi limenisikitisha sana.”

Baada ya kusema hayo Spika Ndugai alihamisha suala hilo kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ili kuangalia jambo hilo lililofanywa na Zitto kama kuna ujinai ndani yake ili waweze kuchukua hatua stahiki.

Kwa upande wake, Prof. Kilangi baada ya maamuzi ya Spika Ndugai alisema: “Mheshimiwa spika maelekezo yako ofisi ya mwanasheria mkuu wa serikali imeyapokea na tutalifanyia kazi kwa mujibu wa sheria zilizopo.”

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Mwekezaji amwaga bil. 39 kujenga viwanda 3 vya uchenjuaji

Spread the loveKampuni ya Mineral Access System Limited (MAST) inayoiwakilishwa kampuni ya...

Habari za SiasaTangulizi

Mpwa wa Magufuli mbaroni kwa kusambaza picha za utupu

Spread the loveJESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limewakamata...

Habari za Siasa

Serikali kuanzisha mradi wa Gridi ya maji ya Taifa

Spread the loveWaziri wa Maji, Jumaa Aweso amesema katika mwaka wa fedha...

Habari za SiasaTangulizi

Shibuda amlima waraka mzito Bulembo

Spread the loveMKONGWE wa siasa nchini, John Shibuda amemshukia kada maarufu wa...

error: Content is protected !!