Waziri wa zamani wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi

Habari ya mwisho ya Marehemu Edson Kamukara

Karamagi, Hamad Rashid matatani

*Wadaiwa kujimilikisha kampuni walimokaribishwa

Na Edson Kamukara

KAMPUNI mpya ya simu za mkononi, inayolenga kutumia teknolojia ya kisasa zaidi kuliko makampuni yaliyopo nchini hivi sasa, imemeguka kabla ya kuanza biashara.

Nazir Karamagi, aliyejiuzulu uwaziri wa nishati na madini kwa kashfa iliyohusisha mkataba wa kufua umeme kati ya serikali na kampuni ya Richmond; na mbunge wa Wawi, Hamad Rashid Mohamed (CUF), wametajwa kuwa katikati ya mgogoro unaomega kampuni hiyo.

Hamad Rashid ndiye anatajwa na nyaraka kuwa mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi ya 4G Mobile Ltd.

Inadaiwa mmeguko huo unatokana na waliokaribishwa kuwekeza katika kampuni hiyo, inayoitwa 4G Mobile Ltd, “kujimilikisha” kampuni na “kuwafukuza” wamiliki waanzilishi.

Wamiliki waanzilishi ni Watanzania wawili, Mohamed Ally Shilla kupitia kampuni yake ya Liberty Commercial Agency & General Supplies Limited; na Seleman Shaaban Mvungi.

Hivi sasa Shilla, ambaye ni mkurugenzi na mwazilishi, amefukuzwa katika kampuni. Mwanzilishi mwenzake, Mvungi ndiye amebaki; lakini bado wawili hao wanashirikiana kukabailiana na kile wanachoita “njama za kunyang’anywa kampuni.”

Kampuni ya 4G Mobile inatokana na kampuni iliyoitwa Talktel Communication Limited iliyopata usajili Na. 6115 kutoka Wakala wa Usajili wa Kampuni (BRELA), 13 Julai 2007. Talktel ilibadilishwa jina mwaka 2011 na kuwa 4G Mobile Limited.

Sasa pande mbili zinavutana. Kila upande una wakurugenzi wake, akaunti zake za benki na umiliki wa hisa zinazodaiwa kugawiwa bila kufuata utaratibu. Bali pande zote mbili zinatuhumu BRELA kwa zinachodai “kuchakachua taarifa zetu.”

Anayetuhumiwa kuwanyang’anya waanzilishi kampuni ni Karamagi. Anadaiwa kukumbatiwa na Mwenyekiti wa Bodi, Hamad Rashid Mohamed. Madai makubwa ni kujigawia hisa na kugawa nyingine bila kufuata taratibu; na mwenyekiti wa bodi kushindwa kutoa taarifa kwa kila kinachotendeka.

Mmeguko huo unahusishwa pia na watoto wawili wa Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa (TISS), Rashid Othman. Wakati upande mmoja unatambua Salehe Rashid Othman kuwa ndiye mwanahisa; upande mwingine unamtambua Said Rashid Othman.

Karamagi alikaribishwa 4G Mobile na kusaini mkataba wake 6/1/2010, akigawiwa hisa 10,000 za Sh. 1,000,000 kila moja. Baadaye kampuni iliamua kushusha thamani ya hisa hadi Sh. 200,000 ili kuvutia wawekezaji wengi.

Kwa hatua ya kushusha thamani ya hisa, zile hisa 10,000 za Karamagi zilizidishwa mara 5 na kupata hisa 50,000. Kwa mujibu wa nyaraka zilizosajiliwa BRELA, Karamagi tayari amelipia hisa 14,336.

Wengine waliogawiwa hisa na waanzilishi ni Kisia Omari (2,000) tarehe 1 Agosti 2008; Hamad Rashid (3,000) tarehe 1/8/2008; Shaah Mahadhy (700) tarehe 2 Agosti 2008; na Zakaria Hans Pope (1,125) tarehe 30 Agosti 2010.

Fomu Na. 210a zilizosajiliwa BRELA kati ya Julai 3 na 5, 2011, zinaonyesha kuwa Shilla na Mvungi, ndio waliwateua, Karamagi, Said R. Othman, Salim M. Said, Shaah H. Mahadhy na Vitus J. Mfugale kuwa wakurugenzi.

Lakini kwa taarifa ambazo MAWIO imeona katika ofisi ya BRELA, Juni 2 mwaka huu na zinazoitwa “nyaraka za mabadiliko” (amendments); kuna wakurugenzi wapya wa 4G Mobile Ltd – walioteuliwa na wengine waliokuwamo kuondolewa. BRELA ilipokea nyaraka hizo 8/5/2015 na kuzisajili 11/5/2015.

Aprili 15, 2011, Karamagi aliwasilisha kwa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) maombi ya leseni ya 4G Mobile Ltd na TCRA ilitoa tangazo kwa umma kupitia gazeti la The Guardian.

Tangazo hilo, lilitofautiana na lile la awali wakati Talktel ikiomba leseni ambapo wanahisa na hisa zao katika asilimia ni Talktel Communication INC (38), Melvin Fields (20), Ruzeda Fields (3) na Howard Cohen (2) wote raia wa Marekani.

Wengine ni Liberty Commercial Agency & General Supplies Limited (17.5) na Selleman Mvungi (17.5) wote raia wa Tanzania.

Wanahisa waliotajwa, na hisa zao kwenye mabano ni, Hamad Rashid (245), Nazir Karamagi (8,315), Joseph M. Mfugale (125), Kisia O. Almassi (1), Salim M. Said (3015) na Said Rashid Othman (1896).

Wengine ni Seleman S. Mvungi (10), M/s Liberty Commercial Agency & General Supplies Limited (5), Vitus Joseph Mfugale (1), Amos G. Nkhoma (1), Zakaria Hans Pope (865), Shaah H. Mahadhy (1) na M/s Semilt Company Limited (1).

Leo hii pande zote mbili ziko mahakamani. Upande wa waanzilishi unapinga akina Karamagi kufungua akaunti benki wakati tayari kampuni ina akaunti Na. 00010362191160 ya mwaka 2008 katika Benki ya AZANIA jijini Dar es Salaam.

Akina Karamagi wako mahakamani wakilalamikia Shilla, Mvungi na Kisia Almasi kwa wanachoita “kugushi nyaraka za 4G Mobile Ltd.

Kuhusu watoto wa kigogo wa TISS, Karamagi anasema, “…sasa hapo ukaulize BRELA, maana nasi wametuvuruga. Wamechomeka jina la mtu ambaye si mwenzetu (akimaanisha Salehe) badala ya Said. Hata hivyo, nyaraka zilizopo zinamtambua Salehe.

Alipoulizwa mbona kwenye gawio la hisa aliyeorodheshwa ni Salehe badala ya Said anayemtaja, Karamagi alisema, “sisi tunamtambua Said, ndiye analipia hisa.”

Msajili msaidizi wa BRELA, Noel J. Shani, amekiri kampuni hiyo kumeguka pande mbili, akisema tarehe 6 Novemba 2014, “…tulikutana na pande mbili na kupitia nyaraka zote za 4G Mobile tangu 14/7/2011 hadi 13/7/2014 ili kuangalia hali ya kampuni.”

Baada ya kikao, BRELA iliainisha hoja nne na kushauri pande hizo zifungue kesi Mahakama Kuu kuomba tafsiri ya kisheria kuhusu:

  • Thamani ya hisa; ni Sh. 1,000,000 au 200,000.
  • Nani katibu halali wa kampuni kati ya Michael Masaka na Protase Tehingisa.
  • Nani wanahisa katika kampuni na hisa zao.
  • Taarifa za mwaka zilizowasilishwa na wakurugenzi wa sasa.

inaendelea wiki ijayo…

Karamagi, Hamad Rashid matatani *Wadaiwa kujimilikisha kampuni walimokaribishwa Na Edson Kamukara KAMPUNI mpya ya simu za mkononi, inayolenga kutumia teknolojia ya kisasa zaidi kuliko makampuni yaliyopo nchini hivi sasa, imemeguka kabla ya kuanza biashara. Nazir Karamagi, aliyejiuzulu uwaziri wa nishati na madini kwa kashfa iliyohusisha mkataba wa kufua umeme kati ya serikali na kampuni ya Richmond; na mbunge wa Wawi, Hamad Rashid Mohamed (CUF), wametajwa kuwa katikati ya mgogoro unaomega kampuni hiyo. Hamad Rashid ndiye anatajwa na nyaraka kuwa mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi ya 4G Mobile Ltd. Inadaiwa mmeguko huo unatokana na waliokaribishwa kuwekeza katika kampuni hiyo, inayoitwa 4G…

Review Overview

User Rating: 3.1 ( 1 votes)
0

About Masalu Erasto

Visit Us On FacebookVisit Us On TwitterVisit Us On Youtube