June 22, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Familia ya Karume Z’bar yataka kurudi Ikulu

Balozi Ali Karume

Spread the love

FAMILI ya Sheikh Abeid Aman Karume, Rais wa Kwanza wa Zanzibar, inataka kurejea Ikulu ya Zanzibar. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Ally Abeid Aman Karume, Mtoto wa Sheikh Abeid Karume, amechukua fomu ya kuwania urais wa visiwa hivyo (Unguja na Pemba) leo tarehe 15 Juni 2020.

Karume amechukua fomu baada ya leo Chama Cha Mapinduzi (CCM), Zanzibar kufungua mlango wa uchukuaji fomu kugombea kuteuliwa ili kupeperusha bendera ya chama hicho kwenye uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 2020.

Kwenye uchaguzi huo, Dk. Ali Mohammed Shein atahitimisha safari yake ya vipindi viwili madarakani – (2010-2020) – ambapo kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania, rais anaruhusiwa kukaa madarakani kwa muda wa vipindi viwili tu (miaka 10).

Iwapo atateuliwa na baadaye kuchaguliwa kuwa rais wa visiwa hivyo, atakuwa ni mtoto wa pili wa rais wa kwanza wa visiwa hivyo kushika madaraka hayo akitanguliwa na kaka yake Aman Abeid Karume (2000-2010).

Mpaka sasa, wanachama wawili wa CCM visiwani humo, ndio waliojitokeza kuchukua fomu ya kuomba ridhaa ya chama hicho kugombea, mbali na Karume, mwingine ni Bakari Juma.

Makada hao wamekabidhiwa fomu hiyo na Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar Idara ya Oganaizesheni.

Aman Abeid Karume, Rais Mstaafu wa Zanzibar

Akizungumza baada ya kukabidhiwa fomu, Karume ameahidi kufuata nyayo za baba yake, kama atapata nafasi ya kugombea urais na kuchaguliwa na Wazanzibar kuwa rais wao.

Amesema, endapo CCM itampa ridhaa ya kugombea urais wa Zanzibar, ataendeleza dhamira ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kulinda muungano sambamba na kuendeleza sera ya chama chake.

“Iwapo nitateuliwa, nategemea kuendeleza dhamira ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kulinda muungano wetu na kuendeleza Sera ya CCM, Dk. Ally Shein, rais wangu amefanya kazi ya kupigiwa mfano hasa kuendeleza sera zilizoanzishwa na Abeid Karume, nia yangu ni kuendeleza yote mazuri,” amesema Karume.

Karume ambaye kwa sasa ni Waziri wa Vijana Utamaduni, Michezo visiwani Zanzibar, amesema endapo atapata nafasi ya kuwa rais wa nchi hiyo, ataboresha utolewaji wa huduma za kijamii, ikiwemo afya, elimu makazi ya watu, ugawaji wa ardhi kwa wananchi wote.

“Nitahakikisha afya inaendelea kupatikana bila malipo,  elimu ipatikane bila malipo, ugawaji ardhi uendelee kwa wananchi wanaohitaji kwa masuala ya kilimo na ujenzi.  Nitajenga makazi bora, Mzee Karume amejenga nyumba nzuri lakini nimeona zinahitaji ukarabati, hilo naahidi tutalifanya pamoja na mengineyo,” amesema Karume.

Zoezi hilo la uchukuaji na urejeshaji fomu ndani ya CCM ambalo litaenda sambamba na utafutaji wadhamini kwa watia nia,  limefunguliwa leo na linatarajia kufungwa tarehe 30 Juni 2020.

error: Content is protected !!