MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), imetangaza kuwa kuanzia tarehe Mosi Julai, 2017 bei ya mafuta itashuka kwa Sh. 37 kutokana na kushuka kwa gharama za usafirishaji wa mafuta katika soko la dunia, anaandika Yasinta Francis.
Titus Kaguo, Meneja Mawasiliano na Uhusiano wa Ewura amesema kuwa bei ya jumla na rejareja zimepungua kwa mafuta ya aina zote yani petroli, dizeli na mafuta ya taa.
“Kuanzia Julai mwaka huu, bei za jumla za petroli zinapungua kwa Sh. 37 kwa lita sawa na asilimia 1.92, dizeli shilingi 13.7 kwa lita sawa na asilimia 0.77 na mafuta ya taa shilingi 18.8 sawa na asilimia 1.10.
“Pamoja na ongezeko la ushuru wa mafuta ya petroli la shilingi 40 kwa lita, lakini kuanzia Julai mwaka huu bei za mafuta kwenye soko la ndani zitapungua kwa kiasi kikubwa,” amesema Kaguo.
Ewura imetangaza kuwa, bei ya mafuta ya petroli kuanzia Julai Mosi, 2017 itakuwa ni Sh. 2,014/- Dizeli Sh. 1,874/- na mafuta ya taa Sh. 1,806/-
“Ewura inawataka wanunuzi wahakikishe wanapata stakabadhi ya malipo inayoonesha jina la kituo, tarehe, aina ya mafuta yaliyonunuliwa na bei kwa lita, stakabadhi hiyo ya malipo itatumika kama kidhibiti cha mnunuzi wa mafuta endapo kutajitokeza malalamiko,” amesema Kaguo.
Leave a comment