Moses Joseph Machali, mbunge wa zamani wa Kasulu Mjini (NCCR-Mageuzi)

Ewe Machali nani aliyekuroga?

Spread the love

NANI aliyemroga Moses Joseph Machali, mbunge wa zamani wa Kasulu Mjini (NCCR-Mageuzi), aliyeongoza jimbo hilo kipindi kimoja cha 2010-2015?, anaandika Shabani Matutu.

Hili ni swali la kwanza kunijia baada ya kupata taarifa kwamba mwanasiasa huyo kijana ameacha siasa za upinzani na sasa anahamia Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Machali,  Novemba 21,2016 aliutangazia umma kwamba sasa ameamua kukumbatia sera, taratibu, kanuni na miongozo yote ya CCM, chama tawala.

Wakati akitangaza haya, Machali alikuwa ni mwanachama wa ACT-Wazalendo, chama alichojiunga nacho baada ya kushindwa kuishi ndani ya nyumba ya NCCR-Mageuzi.

Uamuzi wake huo wa kuhama chama haukunishtua, kwanza ni haki yake kikatiba na pili, hiyo imekuwa kawaida yake tangu aingie katika siasa za ushindani za upinzani.

Kabla ya kutangaza kuhamia CCM, amewahi kupita katika Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), NCCR- Mageuzi na ACT.

Kilichonishtua ni uamuzi wake wa kuhamia CCM, chama ambacho mara kadhaa amekuwa akinukuliwa akiapia kutojiunga nacho akiwa hai kwa manano yake aliwahi kusema, “Mimi kurudi CCM labda niwe maiti”.

Kutokana na kauli hiyo, hivyo baada ya kusoma taarifa yake, ilifanya nipate mshtuko huku nikibaki nikijiuliza kama ni kweli Machali atakuwa mzima au maiti.

Jambo hilo lilinifanya nichukue simu na kumpigia ofisa habari wa ACT – Wazalendo, Abdallah Khamis, nikamuuliza kama Machali ni maiti au mzima, akanijibu ni mzima, akaniuliza kuna nini, sikumjibu kitu zaidi ya kukata simu.

Baada ya kujua ni mzima, nikajiuliza sasa kwa nini Machali amechukua uamuzi wa kujiunga na CCM, chama ambacho wakati akiwa NCCR, aliwahi kusema ni chama cha mashetani, nikajiuliza je, mwanasiasa huyo nini kimemkuta hadi kuamua kujiunga na mashetani, au nayeye amegeuka shetani?

Inashangaza kwamba Machali huyu amekuwa akiwaaminisha wananchi kwa maneno ubaya wa CCM, huku akienda mbali na kuwaponda vijana wanaojiunga CCM, kuwa ni wale wenye njaa, sasa najiuliza imekuwaje ajiunge na CCM au naye njaa imeshamkamata, baada ya kukosa ubunge?

Mwalimu Julius Nyerere amewahi kusema, “mtu aliyezoea kula nyama ya mtu, hawezi kuacha” na ndivyo inavyotokea kwa Machali.

Huyu amekuwa na tabia ya kuhamahama vyama tangu alipojiingiza katika siasa na historia inaonesha amekuwa akiweka mbele maslahi yake.

Machali amekuwa na ugonjwa wa kutoishi maneno yake na ndiyo sababu hata alipokuwa NCCR-Mageuzi, aliwahi kudaiwa kuhamia ACT- Wazalendo, lakini alikana akieleza kwamba hicho ni chama cha “ajabu,”  lakini baadaye aligombea ubunge kwa kupitia chama hicho.

Alifanya hivyo kwa sababu aliamini angeweza kusaidiwa na kiongozi wa chama hicho, Zitto Kabwe kupata ubunge, lakini baada ya kushindwa, sasa anaona sehemu pekee ambayo anaweza kupata nafasi hiyo itakuwa CCM. Naamini akikosa tena mwaka 2020 atahamia chama kingine.

Nimeumia sana na kujiuliza je, huyu kweli ndiye Machali aliyemchongea kwa viongozi wa NCCR, David Kafulila, kiasi cha kuponea chupuchupu kuvuliwa uanachama wake kwa kile alichokisema kwamba alikuwa akitumwa na Zitto Kabwe kuvuruga chama.

Kwa hoja alizotoa Machali, katika andiko lake kwa Watanzania, akitoa sababu za kujiunga na CCM, hazikuwa na mashiko, labda angekuwa mjanja angeweza kuwa mkweli na kusema ameamua kurejea huko ili akatafute ubunge katika uchaguzi mkuu ujao baada ya kuukosa ACT.

Kwa mfano, Machali anaelezea sababu za kujiunga CCM kuwa zimechangiwa na utendaji wa serikali ya awamu ya tano, chini uongozi wa Rais John Pombe Magufuli.

Anasema, Rais Magufuli ameonesha dhamira safi ya kuiendeleza nchi, huku akijisahaulisha kwamba mwaka mmoja pekee, katika uongozi huu, maisha yamekuwa magumu kwa Watanzania wengi.

Machali ni shahidi kwamba hali hiyo inaweza ikawa ni miongoni mwa sababu za mwenyewe kuona akimbilie CCM, ili kupooza ugumu wa maisha anaokabiliana nao baada ya kukosa ubunge.

Sitaki kuamini kwamba Machali niliyekuwa namjua kuwa ni mjenga hoja mzuri, ameshindwa hata kutambua kwamba serikali hii imeweka rekodi ya kuwakamua wananchi kuliko nyingine zilizopita kwa kuwatoza kodi kila mahali, ikiwemo kwenye vocha, kwenye huduma za pesa mtandao.

Ama kweli “adui muombee njaa, lazima atainua mikono juu hata kama alikuwa shujaa” ni sehemu ya maneno yanayopatikana katika wimbo ‘Darubini’ ulioimbwa na msanii Selemani Msindi, almaarufu ‘Afande Sele’ ukionesha namna ambavyo unavyoweza kuwanyong’onyeza watu wasiojiamini na kujikuta wakikata tamaa.

Nasikitika kijana Machali kufikia wakati akifananisha uongozi wa Rais Magufuli ule wa Mwalimu Nyerere na aliyekuwa waziri mkuu, Edward Moringe Sokoine, jambo ambalo hata yeye anajua ufananishaji huo ni urefu wa mbingu na ardhi.

Nasema hivyo kwa sababu Machali anajua hali ya uchumi inavyotia huruma kwa mujibu wa ripoti za Benki Kuu Tanzania (BoT), pamoja na miradi ya maendeleo kutengewa Sh. 824.4 bilioni, lakini Serikali kwa kukosa fedha zimetumika Sh. 387 bilioni pekee kwa mwezi Septemba.

Sitaki kuamini kwamba Machali amejiweka ‘upofu’ wa kushindwa hata kupitia ripoti ya BoT na kubaini kwamba uchumi wa nchi umeporomoka kwa makusanyo ya mapato ya ndani kwa Septemba 2016 kwa asilimia 16, ambako Mamlaka ya Kodi (TRA) ilipanga kukusanya Sh. 1.3 trilioni, ila ikaambulia kukusanya asilimia 84 ya lengo.

Uchumi anaosema Machali umemfurahisha kujiunga CCM ni huu ambao hadi Desemba 2015, dola moja ilikuwa Sh. 1,600 na sasa mwaka mmoja wa Rais Magufuli, thamani ya fedha imeshuka na dola ni sawa na Sh. 2,150.

Sitaki kuwa sehemu ya wale wanaofikiri kwamba haya aliyoamua Machali yanaweza kuhusishwa na matukio kadhaa ya kifamilia aliyodaiwa kuyafanya mwanasiasa huyo kijana.

Ninaweza kuungana na wale wanaomshukuru Machali kwa kuchukua uamuzi huo mapema, jambo ambalo limemshinda Profesa Ibrahim Lipumba ambaye amekuwa akisumbua upinzani wakati akijua anaunga mkono kila kitu cha CCM kwa manufaa binafsi.

Makala hii ilitoka kwenye gazeti la MwanaHALISI la toleo 367 namba la tarehe 28 Novemba – 4 Desemba, 2016.

NANI aliyemroga Moses Joseph Machali, mbunge wa zamani wa Kasulu Mjini (NCCR-Mageuzi), aliyeongoza jimbo hilo kipindi kimoja cha 2010-2015?, anaandika Shabani Matutu. Hili ni swali la kwanza kunijia baada ya kupata taarifa kwamba mwanasiasa huyo kijana ameacha siasa za upinzani na sasa anahamia Chama Cha Mapinduzi (CCM). Machali,  Novemba 21,2016 aliutangazia umma kwamba sasa ameamua kukumbatia sera, taratibu, kanuni na miongozo yote ya CCM, chama tawala. Wakati akitangaza haya, Machali alikuwa ni mwanachama wa ACT-Wazalendo, chama alichojiunga nacho baada ya kushindwa kuishi ndani ya nyumba ya NCCR-Mageuzi. Uamuzi wake huo wa kuhama chama haukunishtua, kwanza ni haki yake kikatiba na…

Review Overview

User Rating: Be the first one !

About Mwandishi Wetu

Leave a Reply

Your email address will not be published.

error: Content is protected !!