Friday , 29 March 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Duni: Ningali na nguvu, salam zao CCM
Habari za Siasa

Duni: Ningali na nguvu, salam zao CCM

Spread the love

BABU Juma Duni Haji, mmoja wa wanasiasa wakongwe nchini, amechukua fomu ya kugombea nafasi ya Makamu Mwenyekiti akitarajia kuwa mmoja wa viongozi wa juu wa Chama cha ACT Wazalendo. Anaripoti Jabir Idrissa, Zanzibar…(endelea).

“Ningali na nguvu za kutumikia siasa ambayo niliianza tangu nikiwa shule wakati huo hapa kwetu Zanzibar tuna Afro Shirazi Party (ASP),” alisema baada ya kupokea fomu kwa Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho Zanzibar, Hamad Yussuf Mussa.

Duni amesema amekuwa imara kila wakati kwa sababu haja na dhamira ya kuihami Zanzibar dhidi ya njama za kuiua ingali hai,” alisema mbele ya viongozi waandamizi wa chama hicho pamoja na waandishi wa habari kwenye ofisi ndogo ya makao makuu, Vuga mjini Zanzibar.

Duni amekuwa naibu kiongozi wa ACT Wazalendo tangu Septemba mwaka jana siku chache baada ya kujiunga akitokea Chama cha Wananchi (CUF) kufuatia kugubikwa na mgogoro ambao CCM kinatuhumiwa kuupandikiza kwa kumtumia mwenyekiti wake, Profesa Ibrahim Lipumba.

Duni amesema angali mwenye afya nzuri na kwa sababu siasa ndio njia halali ya kupigania maslahi ya Zanzibar kupitia vyama, anataka ridhaa ya wanachama wenzake ili aongoze jahazi.

Lakini Babu Duni amechukua fomu huku akitoa ujumbe maalum kwa viongozi na wanachama wa CCM wakati huu chama hicho kinapotimiza miaka 43 ya kuzaliwa baada ya kuunganishwa kwa ASP kilichokuwa cha Zanzibar na Tanganyika National Union (TANU) kilichokuwa Tanganyika hapo tarehe 5 Februari 1977.

Amesema wakati CCM iliundwa chini ya lengo kuu la kuendeleza maslahi ya kisiasa ya nchi mbili – Zanzibar na Tanganyika – lakini kwa sasa maslahi ya Zanzibar yamepuuzwa kutokana na nguvu za chama hicho kulalia upande wa Tanganyika.

Alisema baada ya 1977 taratibu mwelekeo wa chama kipya ulionekana kuidhoofisha Zanzibar ambayo kabla ilikuwa na nguvu zake kamili kisiasa na kiuchumi.

Amesema siku hizi ile turufu iliyokuwa nayo Zanzibar kisiasa ndani ya Muungano ulioasisiwa 1964, na hata ilipozaliwa CCM miaka 13 baadaye, haipo tena.

“Turufu leo ni kibogoyo hatafuni wala haimung’unyi. Viongozi wa upande ule wanawakemea wa Zanzibar kama tulivoona alipokuja ziara Polepole,” alisema. Humphrey Polepole ni Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM.

Amesema hata viongozi waliomtangulia Katibu Mkuu Dk. Bashiru Ali akiwemo Luteni Yusufu Makamba ilikuwa hivohivo wakionesha kuwa juu kimamlaka kuliko walioko Zanzibar.

Sasa hatuna kitu Zanzibar, alisema na kufafanua “hatuna kitu kwenye serikali na hatuna kitu kwenye chama. Tizama utaratibu uliowekwa wa kutumia maeneo ya ardhi yaliyochukuliwa na CCM kwa mgongo wa dola, mapato yake yanapelekwa Dodoma.”

Alisema wakati wa uongozi wa Mzee Abeid Amani Karume baada ya Muungano wa tarehe 26 Aprili 1964 aliwahi kuzuia msafara wa askari waliokuwa wa Zanzibar kupelekwa Msumbuji kuwakilisha Tanzania kwenye vita vya kuikomboa Msumbiji kwa kuwa hakushauriwa na Mwalimu Julius Nyerere.

Amimnukuu mzee Karume aliyekuwa Rais wa Zanzibar na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Duni alisema “wakiuliwa kule nitasema nini nitapoulizwa na wazazi wao.”

Amesema nani asojua namna maslahi ya Zanzibar yanavoamuliwa na CCM kutokea makao makuu yake Dodoma hata pale viongozi wa Zanzibar wanapokuwa na msimamo wao.

Aliwasihi Wazanzibari walio CCM wasifurahie tu umri wa chama chao bali wafikirie manufaa inayoyapata Zanzibar, nchi yao iliyopigania ukombozi wa maslahi yao kutoka kwa wageni.

Written by
Jabir Idrissa

+255 774 226248

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

Chadema yamtaka Rais Samia aunde tume kuchunguza mauaji mgodi wa Barick

Spread the loveRAIS Dk. Samia Suluhu Hassan, ameombwa aunde tume huru kwa...

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Nani anasema kuna hasara ATCL?

Spread the loveRIPOTI za makusanyo na matumizi ya fedha katika Kampuni ya...

Habari za SiasaTangulizi

CAG: Wastaafu, wenza wao chanzo NHIF kufilisika

Spread the loveRIPOTI ya ukaguzi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu...

Habari za SiasaTangulizi

Vikundi hewa 851 vyalamba bilioni 2.6 mikopo ya halmashauri

Spread the loveVIKUNDI hewa vya wajasirimali wadogo 851 kutoka katika halmashauri 19...

error: Content is protected !!