JESHI la Polisi limeanza kumhoji msanii Godfrey Tumani maarufu kama ‘Dudubaya’ kufuatia tuhuma zinazomkabili za kumdhihaki aliyekuwa Mkurugenzi wa Vipindi na Uzalishaji Clouds Media Group, Marehemu Ruge Mutahaba. Anaripoti Regina Mkonde … (endelea).
Kamanda wa Polisi Kinondoni, Mussa Taibu leo tarehe 28 Februari 2019 amesema Dudubaya anashikiliwa na polisi kwenye kituo cha Oysterbay jijini Dar es Salaam kwa ajili ya mahojiano.
Kamanda Taibu amesema Jeshi la Polisi limefungua jalada la uchunguzi wa tuhuma za matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii, na kwamba wakijiridhisha na madai hayo, hatua zaidi za kisheria zitafuata.
Jeshi la Polisi limechukua hatua hiyo baada ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe jana kuagiza msanii huyo kuchukuliwa hatua kwa kumdhihaki Mrehemu Ruge.
Dudubaya alisambaza katika mitandao ya kijamii video aliyojirekodi akitamka maneno ya kejeli dhidi ya marehemu Ruge, baada ya taarifa za kifo cha Ruge kusambaa.
Ruge alifariki dunia usiku wa tarehe 26 Februari 2019 nchini Afrika Kusini alikokuwa anapatiwa matibabu ya tatizo la figo lililomsumbua kwa zaidi ya miezi minne, ambapo alianza kutibiwa katika Hospitali ya Kairuki iliyoko jijini Dar es Salaam, na baadae akapelekwa India kisha kupelekwa Afrika Kusini ambako umauti ulimfika.
Leave a comment