DAKTARI Phillip Mpango, Waziri wa Fedha na Mipango amezitaka nchi za Afrika kutosalimu amri, kwa mataifa ya kigeni, yanayohatarisha uhuru wa kujitawala. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).
Dk. Mpango ametoa kauli hiyo jana tarehe 25 Oktoba 2019, katika Kongamano Maalumu la Vita vya Kiuchumi na Hatma ya Afrika, lililofanyika jijini Dar es Salaam.
“Kamwe tusisalimu amri, kwa wale wanaojaribu kupinda mikono yetu na kuhatarisha uhuru wetu wa kujitawala,” amesema Dk. Mpango.
Waziri huyo wa fedha ameeleza kuwa, nchi za Afrika zimepata uhuru wa kisiasa lakini zimekosa uhuru wa kiuchumi.
“Tumepata uhuru wa kisiasa, lakini uhuru wa kiuchumi bado. Fikra za utegemezi, uhisani bado zipo. Inabidi tuzipige vita. Lakini pili, Afrika lazima izingatie misingi ya usimamizi wa uchumi. Ni lazima nchi zetu tuzielekeze kupanua wigo wa kiuchumi kwa upande wa uzalishaji masoko na mtaji,” amesema Dk. Mpango.
Profesa Palamagamba Kabudi, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki amesema nchi za Afrika zilizoamua kujitegemea ziko vitani kutokana na vitimbi vya mataifa yaliyoendelea.
“Tuko vitani, tunaishi kwenye nchi za vitimbi hasa kwa mataifa yanayoamua kujitegemea,” amesema Prof. Kabudi.
Leave a comment