Friday , 19 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Masha: Serikali iruhusu wapelelezi wa nje
Habari za SiasaTangulizi

Masha: Serikali iruhusu wapelelezi wa nje

Lawrence Masha, Kada wa Chadema na Aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani wa Awamu ya Nne Tanzania
Spread the love

UCHUNGUZI utakaofanywa na wachunguzi wa nje ya Tanzania kuhusu matukio ya kihalifu yanayoendelea nchini, utatoa nafasi nzuri kwa serikali ya Dk. John Magufuli kufuta hisia nzito walizonazo umma za kuhofu kuwa matukio hayo yana mkono wake, anaandika Jabir Idrissa.

Ni kauli ya Lawrence Masha, mwanasheria na waziri wa zamani wa Mambo ya Ndani, mbele ya waandishi wa habari katika mkutano uliofanyika leo makao makuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Kinondoni, Dar es Salaam.

“Utaratibu wa Serikali ya Tanzania kuruhusu wachunguzi wa taasisi za nje za kiuchunguzi si mgeni; na wala kuwapa nafasi wachunguzi wa mataifa ya nje kwenye matukio yanayotokea sasa, si fedheha kwa serikali na nchi,” amesema Masha ambaye pia ni wakili wa Mahakama Kuu, na kiongozi mwandamizi wa Chadema.

Masha hakutaja tukio hata moja la kihalifu lililowahi kuchunguzwa na wachunguzi au wapelelezi wa nje ya nchi. Lakini, kumbukumbu zinaonesha kuwa ndani ya miaka mitano kuanzia 2010, yapo matukio yalichunguzwa na wapelelezi wageni.

“Marekani imeendelea lakini huchukua wachunguzi wa nje muda mwingine, mfano Uingereza na sehemu nyingine, sio kwamba wao hawawezi kazi,” amesema Masha.

Tukio la kwanza ni la kuuliwa kwa risasi kwa Padre Evarist Mushi wa Kanisa Katoliki Zanzibar, la Februari 17, 2013, ambalo lilichunguzwa na wapelelezi wa Shirika la Upelelezi la Marekani – Federal Bureau of Investigation (FBI).

Tukio jingine lililowahi kuchunguzwa na wapelelezi wa nje ya Tanzania, ni la mapema Agosti 2013 la kumwagiwa tindikali vijana wawili wa kujitolea wa Uingereza waliokuwa wakifanya kazi ya ualimu visiwani Zanzibar.

Katie Gee, mwenye umri wa miaka 22, na Kirstie Trup 18, walikuwa wakifundisha watoto yatima mjini Zanzibar, walipokutwa na kadhia hiyo walipowasili tu hotelini kwa ajili ya chakula cha usiku.

Ilikuwa ni eneo la Shangani, karibu na Hoteli ya kitalii ya Africa House. Makachero wa Scotland Yard, kikosi mashuhuri kwa uchunguzi wa matukio ya jinai cha Uingereza, waliingia nchini kwa siri na kuchunguza tukio hilo.

Masha amesema uchunguzi wa vyombo vya nje utaipa heshima Tanzania kuwa imejenga imani kwa umma na jumuiya ya kimataifa kwamba haina cha kuficha katika matukio hayo.

Amesema analiamini Jeshi la Polisi Tanzania na kwamba wataalamu wake wengi wa upelelezi wamepata mafunzo nchini Marekani na Uingereza, lakini anaamini litasaidiwa iwapo matukio kadhaa yenye utata katika mazingira ya kutokea kwake yatachunguzwa na wapelelezi wa kigeni.

Waziri huyo wa zamani katika serikali ya awamu ya nne chini ya Jakaya Kikwete, ametoa kauli hiyo wakati shinikizo kwa serikali kutakiwa kuruhusu uchunguzi wa taasisi za kimataifa zinazidi kusikika. Ukiacha vilio vya ndani ya nchi, asasi mbalimbali za kutetea haki za binadamu zimepata kushawishi kuruhusiwa kwa wachunguzi wa mataifa ya nje.

Shinikizo zilianza tangu pale aliposhambuliwa Tundu Lissu kwa risasi za moto akiwa anawasili nyumbani kwake eneo la Area D, mjini Dodoma alikokuwa akihudhuria vikao vya Bunge. Lissu alishambuliwa mchana kweupe Septemba 7, na watu waliokuwa wakimfuatilia tangu alipokuwa ukumbini mwa Bunge.

Tangu tukio hilo litokee, vyombo vya ulinzi na usalama vimekuwa vikitoa kauli nyepesi kuliko uzito wa tukio lenyewe kwa namna lilivyovuta hisia za umma ndani na nje ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Lissu alishambuliwa kwa risasi zaidi ya 30 akiwa ndani ya gari, nje ya nyumbani kwake, siku chache baada ya mwenyewe kueleza kuwa amekuwa akifuatiliwa na watu aliowaita wa “ulinzi na usalama” na akamsihi Inspekta Jenerali wa Polisi

Simon Sirro na Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa (TISS), Dk. Modestus Kapilimba wawatake vijana hao waache kumfuatilia.

Kwa sasa Lissu anaendelea na matibabu maalum katika moja ya hospitali kubwa za nchini Kenya.
Matukio ambayo umma ungependa yakachunguzwa na wapelelezi wa nje, mbali na hilo, ni la kutekwa na kuteswa kwa Dk.

Steven Ulimboka, tukio la Juni 2012, kushambuliwa kwa Absalom Kibanda aliyekuwa Mhariri Mtendaji wa Tanzania Daima, na ambaye alikuwa ndio kwanza amehamia New Habari House, kutoweka kwa Benson Saanane, aliyekuwa katibu wa Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na kuchomwa kwa njia ya mlipuko wa bomu ofisi za kampuni ya uwakili ya IMMMA ya Dar es Salaam.

Pia kuna matukio kadhaa ya utekaji wasanii.

Written by
Jabir Idrissa

+255 774 226248

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

BiasharaHabari za Siasa

Mavunde aagiza Perseus kuharakisha fidia Sengerema

Spread the loveWaziri wa Madini, Anthony Mavunde ameipongeza Kampuni ya Perseus kwa...

Habari za Siasa

Kigogo Chadema awanyooshea vidole vigogo serikalini kuhusu ripoti ya CAG

Spread the love  MWANACHAMA wa Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Boniface Jacob, amedai...

Habari za Siasa

Wabunge waikalia kooni TAKUKURU Bungeni

Spread the love  BAADHI ya wabunge wamelia na changamoto za utendaji wa...

Habari za SiasaTangulizi

Mpina ataka Waziri Majaliwa ajiuzulu, akosoa teuzi za mawaziri

Spread the love  MBUNGE wa Kisesa, Luhaga Mpina, amemtaka Waziri Mkuu, Kassim...

error: Content is protected !!