January 16, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Dk. Bashiru ataja mambo 3 kuimaliza corona, ataka Kigogo apuuzwe

Chuo cha Uongozi cha CCM, kilichopo KIbaha

Spread the love

KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Bashiru Ally ametaja mambo makubwa matatu yanayowezesha Tanzania kushinda vita ya mapambano ya maambukizi ya ugonjwa unaosababishwa na virusi vya corona (COVID-19). Anaripoti Mwandishi Wetu, Pwani … (endelea).

Pia, mtendaji mkuu huyo wa chama tawala, amekemea vikali baadhi ya watu kutumia mitandao ya kijamii kueneza uongo, chuki na husda kwa wengine, akitolea mfano akaunti ya twitter inayojiita Kigogo 2014.

Dk. Bashiru amesema hayo leo Jumamosi tarehe 23 Mei, 2020  akiwa safarini kwenda Dodoma kutoka Dar es Salaam, alipopita kufanya ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa Chuo cha Mafunzo  ya Uongozi cha Mwalimu Nyerere unaendelea eneo la Kwa Mfipa, Kibaha, mkoani Pwani.

Awali, ujenzi huo ulipaswa kukamailika June, 2020, lakini utakamilika Agosti, 2020 kutokana na changamoto ya ugonjwa wa Corona kufanya baadhi ya vifaa vilikuwa vikiagizwa kutoka nje ya nchi kukawia kufika nchini humo.

Akiwa hapo, amewapongeza viongozi wa Serikali akiwamo Rais wa Tanzania, John Magufuli kwa jitihada za kupambana na corona kwa kutumia maarifa zaidi.

Dk. Bashiru ametaja mambo hayo kuwa ni, ni moyo wa kujitolea akisema, “wananchi wengi wa Tanzania inapofika wakati wa kulinda uhai wa nchi yao, huwa wapo mstari wa mbele, hata vita ya Kagera ilikuwa hivyo.”

Pia, ni elimu ya kujitegemea, “elimu hii ni elimu ya kujiamini, kwamba sisi ni watu na tupo sawa na watu wengine, awe mweupe au mweusi, mtu ni mtu, sasa ufahamu kuwa mimi ni mtu.”

“Hii ni elimu kubwa na kama huwezi kufahamu kuwa binadamu wote ni sawa na hakuna mwenye hati miliki ya maarifa huwezi ukajitegemea, na huwezi ukajiamini,” amesema Dk. Bashiru

Jambo la tatu, Dk. Bashiru amesema, ni kuwa na viongozi jasiri na viongozi ambapo ni wachapa kazi na wenye kumbukumbu za namna ambavyo nchi iliasisimiwa, sasa na hayo mambo matatu ndio tayazingatie katika mafunzo ya chuo hiki.”

Katika hatua nyingine, Katibu Mkuu huyo amepita kukagua ujenzi wa ukumbi wa mikutano ofisi za CCM mkoa wa Pwani ambapo pamoja na mambo mengine, amekemea vikali kwa watu kutumia mitandao ya kijamii kueneza uongo, chuki na husda kwa wengine, akitolea mfano akaunti ya twitter inayojiita Kigogo 2014

“Wamezuka watu wanatumia mitandao ya kijamii kukibeza chama na Serikali, mimi siwezi kupuuza kwa sababu hiki ni chama ambacho kinaongoza nchi na kina rekodi iliyotukufu,” amesema Dk. Bashiru.

“Kuna mtu anajiita kigogo 2014, alisema katibu wetu wa Rombo kafa, kumbe mtu mzima na analea watoto wake, jamani mitandao ya kijamii iwe na taarifa za kujenga, taarifa ziwe za kweli,  wapuuzeni watu wanaoiandika CCM kwa kutumia akaunti inaitwa Kigogo 2014,” amesema.

Ameendelea kuwasisitiza wanaCCM kutotumia mitandao ya kijamii kuchafuana, badala yake watumie mitandao hiyo kujengana na kuelimishana.

Dk. Bashiru Ally, Katibu Mkuu wa CCM

Ziara hiyo imeongozwa na Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Pwani, Ramadhani Maneno na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa chama na Serikali wakiwemo wajumbe wa halmshauri kuu ya taifa ya CCM, Haji Abuu Jumaa, Anna Agatha Msuya.

Wengine waliokuwepo ni, Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Ashumpta Mshana, Mwenyekiti wa Vijana wa Mkoa wa Pwani, Samaha Seifu Said, na Katibu wa CCM wa Mkoa wa Pwani, Ally Makoa.

Baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi huo, katika kikao kilichojumisha Kampuni ya Ujenzi ya CRJE na viongozi wa chama mkoa wa Pwani, Dk. Bashiru ametumia fursa hiyo kueleza siri ya Tanzania kuelekea kushinda vita dhidi ya majanga mbalimbali ikiwemo janga la korona.

“Kuna watu walikuwa wanadhani kwa kuwa hatuna simu ya kuwatambua watu wenye corona kwa kuwafuatilia, hatuna ventileta nyingi, hatuna vyumba vya ICU vingi lakini tunauzoefu wa uongozi wa kisiasa wakati wa vita.”

“Na wakati ule nazungumza hakukuwa na mbaya, lakini kuna kipindi hali kidogo ilikuwa mbaya, lakini kutokana na uzoefu na ujasiri wa Rais wetu na mwenyekiti wetu kwa kufuata nyayo za waaasisi wa Taifa letu, nafasi ya kushinda vita hii kwa sasa ni kubwa,” amesema.

Dk. Bashiru amesema, nchi nyingine zinapambana na corona kwa shida nyingi, sio tu kuvaa barakoa, sabuni na kujifukiza kama hapa kwetu Tanzania. Wakati nchi nyingine wanapambana na corona na shida ya chakula inawaandama.”

“Sisi hapa tunachakula cha kutosha, na hiyo ndio maana ya kujitegemea, wataalamu hatujaletewa wote ni wa kwetu. Hivyo, Watanzania tujiamini, tunaweza, na tulishaweza mengi tusidharirishane, tushirikiane, tuheshimiane, waasisi wa taifa hili walishatujengea misingi imara,” ameongeza.

error: Content is protected !!