Saturday , 20 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Deus Kibamba: Hakutakucha hadi tukorome
Habari za SiasaTangulizi

Deus Kibamba: Hakutakucha hadi tukorome

Deus Kibamba
Spread the love

WADAU mbalimbali wa masuala ya haki ya kikatiba ya uhuru wa kujieleza jana walikusanyika kwenye ukumbi wa Kilimanjaro, katika Hoteli ya Seashells, Makumbusho, jijini Dar es Salaam, kwa azma ya kuendesha majadiliano kuhusu tatizo linalokua kwa kasi la kusinyaa kwa uhuru wa kujieleza nchini Tanzania. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Katika mkusanyiko huo ulioandaliwa na Kituo cha Sheria na Haki za Binaadamu Tanzania (LHRC), yalitolewa maoni yaliyoashiria kuongezeka kwa vikwazo vya kuitumia haki hiyo ya uhuru wa kujieleza nchini na washiriki kuhimizana haja ya kuchukuliwa hatua madhubuti za kukabiliana na vikwazo hivyo.

Mwelekeo wa majadiliano ulijionesha wazi kuwa ni imani ya washiriki kuwa vikwazo vinavyoathiri utekelezaji wa haki hiyo ya uhuru wa kujieleza vinatokana na mwenendo wa uongozi katika serikali ya awamu ya tano chini ya Chama Cha Mapinduzi (CCM). Mfano hai wa hilo ni uamuzi wa serikali kuwasilisha bungeni muswada wa sheria ambao pamoja na mambo mengine unapendekeza kubadilishwa sheria inayotoa haki ya wananchi kuanzisha asasi za kiraia.

Majadiliano hayo yalichagizwa na mkurugenzi wa zamani wa Jukwaa la Katiba Tanzania, Deus Kibamba, aliyetanguliwa na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Wakili Fulgence Massawe, ambaye alifungua rasmi mkutano ulioshirikisha viongozi wa vyama vya siasa, waandishi wa habari na wahariri wanaowakilisha Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), pamoja na asasi kadhaa za kiraia zikiwemo zile zinazowakilisha vijana na wanawake.

Akifungua majadiliano hayo, wakili Massawe ambaye pia ni mwanachama wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), alisema sasa imekuwa ni mtindo kwa uongozi wa serikali kupeleka miswada ya sheria bungeni bila ya kutumia utaratibu wa kushirikisha wananchi.

Wakili Massawe amesema utungaji wa sheria unapaswa kuwa shirikishi kwa kuwa kwa asili yake, hukusudiwa kusaidia kuondoa matatizo katika jamii. Amesema amepata uzoefu wa kutosha wa namna sheria zinazotungwa katika miaka ya karibuni zinavyokiuka misingi ya katiba ya nchi. Udhaifu huo unachochea haja ya wananchi kuwa mstari wa mbele kutumia mhimili wa Mahakama kuzipinga sheria mbaya.

Akiwasilisha mada ya Hali ya Ushiriki wa Wananchi Tanzania, Kibamba ambaye pia ni mchambuzi maarufu wa masuala ya kidemokrasia barani Afrika, alisema bado anaamini mamlaka ya kiutawala nchini ni ya wananchi; bali wanayagawa kwa baadhi ya raia wenzao kupitia utaratibu wa kuchagua viongozi.

Kibamba amesema analiona tatizo kubwa katika miaka ya karibuni, hususan baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, la kupotea kwa fursa na nafasi ya wananchi kuzungumza kama mabosi wa viongozi. “Hii kasoro naiona licha ya kwamba wanaoongoza huyapata mamlaka kutoka kwa wananchi… haya mamlaka ni ya kikatiba kabisa lakini inasumbua kukuta pana matukio ya kuwashambulia wananchi haohao wanaotoa mamlaka kwa watawala,” alisema.

Kadhalika, amezungumzia visa vya kushambuliwa wananchi wanaotoa maoni kuhusu wanavyoongozwa, kutofanyiwa uchunguzi kamilifu. “Ninamnukuu Rais wetu akishangaa Jeshi la Polisi kushindwa kuwa makini katika uchunguzi wa matukio na kulitaja hasa tukio la kutekwa kwa MO (Mohamed Dewji) kama mfano wa uoni wa Rais John Magufuli kuhusu udhaifu wa uchunguzi wa matukio ya kijinai nchini,” alisema.

Kibamba hajakata tamaa; wala haamini kuwa milango yote imefungwa. Anasema “Milango haijafungwa yote, ipo mingine inasubiri wananchi kuitumia kupigania kubakia na mamlaka yao katika nchi yao. Katiba haiwezi kubadilishwa ili ubosi wa wananchi wa Tanzania upunguzwe. Hii haiwezekani.”

Anahimiza umuhimu wa wenye maarifa kuwafikia wananchi na kuwasaidia kutambua wajibu wao katika kukabiliana na vitisho vya kunyimwa haki ya uhuru wa kujieleza na kushirikishwa katika kufikiwa maamuzi ya mambo yanayohusu hatima yao katika nchi yao.

Anahitimisha: “Japo najua kuna upenyo wa uchumi duni, hili lina njia yake kulitatua; lazima Katiba yetu itumike kuzipima sheria zinazokandamiza uhuru wa wananchi kujieleza. Niseme basi, ukiniuliza inakuaje kama hali ndio hiyo, nitasema lipo giza nene ila ndio kunakucha lakini sasa kutakuchaje pasina wananchi kukoroma (kuzungumza hisia zao)?”

Bob Chacha Wangwe alitoa uzoefu wake wa kupigania haki akigusia alivyofungua madai mahakamani kupinga sheria mbaya wakati Clara ambaye ni mwenye ualbino, alisikitikia namna walioua watu wenye ulemavu huo wanavyoendelea kufaidi maisha. “Kila tunakokwenda tunajikuta hatuko huru na tunakosa amani kwa sababu waliowaua wenzetu wangali hai wakati wamehukumiwa kunyongwa. Tutaridhika wakinyongwa angalau mmoja ili wanaofikiria kuua wengine wafikiri mara mbili,” alisema.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

Dk. Mwakyembe : Zanzibar waliongoza kutaka Serikali 2 za muungano

Spread the love  MWANASIASA mkongwe nchini, Dk. Harrison Mwakyembe, amesema mjadala wa...

Habari za SiasaTangulizi

Rais Samia ataja mikakati ya kufikia trilioni 2 biashara Uturuki, Tz

Spread the loveWakati Tanzania na Uturuki zikidhamiria kuongeza kiwango cha biashara hadi...

BiasharaHabari za Siasa

Mavunde aagiza Perseus kuharakisha fidia Sengerema

Spread the loveWaziri wa Madini, Anthony Mavunde ameipongeza Kampuni ya Perseus kwa...

Habari za Siasa

Kigogo Chadema awanyooshea vidole vigogo serikalini kuhusu ripoti ya CAG

Spread the love  MWANACHAMA wa Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Boniface Jacob, amedai...

error: Content is protected !!