DEREVA wa Mbunge wa Jimbo la Kyaddondo Mashariki nchini Uganda, Robert Kyagulanyi Bobi Wine, Yasin Kawuma amefariki baada ya kupigwa risasi na watu wanaodaiwa kuwa na polisi. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).
Bobi Wine amedai kuwa dereva wake ameuawa kwa kupigwa risasi na polisi akiwa ndani ya gari la mbunge huyo, wakidhani kuwa aliyekuwa kwenye gari ni yeye.
Mbunge huyo ambaye pia ni msanii wa muziki nchini humo, ameandika katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter kuwa walikuwa eneo linalojulikana kama Arua kwenye kampeni wakati mauaji hayo yalitokea.
Bobi Wine na viongozi kadhaa wa upinzani walikuwa eneo hilo kumuunga mkono mgombea huru Kassiano Wadri anayeshiriki katika uchaguzi mdogo wa kuziba nafasi ya Mbunge wa jimbo hilo, Ibrahim Abiriga aliyeuawa.
Police has shot my driver dead thinking they've shot at me. My hotel is now coddoned off by police and SFC. #Arua pic.twitter.com/fw0GeV0vU9
— BOBI WINE (@HEBobiwine) August 13, 2018
Wakati wa kampeni hizo zikiendelea kulizuka vurugu kati ya wafuasi wa Wadri na wale wa mpinzani wake katika uchaguzi huo wa chama cha NRM, Tiperu Nusura.
Msemaji wa polisi Emilian Kayima, anasema watu waliokuwa wamevaa shati za kampeni za mgombea Wadri, walianza kuurushia mawe msafara wa rais hali ambayo ilisababisha polisi kufyatua risasi.
“Mwendo wa saa kumi na mbili jioni msafara wa rais ulishambuliwa na wahuni katika manispaa ya Arua wakati rais alikuwa anaondoka uwanja wa Boma ambapo alikuwa amefanya mkutano wa mwisho,” amesema Kayima.
Leave a comment