Friday , 29 March 2024
Home Gazeti Habari za Siasa CUF yakengeuka, yameza matapishi yake
Habari za Siasa

CUF yakengeuka, yameza matapishi yake

Mhandisi Mohamed Ngulangwa, Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Mahusiano na Umma CUF (kulia)
Spread the love

CHAMA cha Wananchi (CUF), kimebariki wabunge wake wawili waliotangazwa kuwa washindi katika katika uchaguzi mkuu uliyopita nchini Tanzania, kuhudhuria vikao vya Bunge. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Akizungumza na MwanaHALISI Online, Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Mahusiano na Umma wa chama hicho, Mhandisi Mohamed Ngulangwa, ameeleza kuwa kuruhisiwa kwa wabunge hao kwenda bungeni, kumezingatia kile alichokiita, “maslahi ya umma.”

“Chama kimetafakari na kubaini kuwa kikiwazuia wabunge wake hawa, kitadhurumu haki za wananchi waliowachagua. Lakini pia wabunge hao watashindwa kulipa gharama walizotumia katika kampeni,” ameeleza Ngulangwa.

Alipoulizwa wanawezaje kuruhusu wabunge kushiriki mikutano ya Bunge, lakini papo hapo uchaguzi uliotokana na wabunge hao wanadai kuwa siyo halali, Ngulangwa alisema, “siyo kwamba hatuwatambui.”

Alipoelezwa kuwa chama chake, tayari kimesema, hakitambui uchaguzi huo na matokeo yake, Ngulangwa alisema, “hatuwezi kuwaadhibu wananchi wa maeneo haya na hao wabunge wamegharamika na masuala ya uchaguzi.”

Katika uchaguzi mkuu wa 28 Oktoba mwaka huu, CUF kilitangazwa washindi katika majimbo ya Mtwara Vijijini, kusini mwa Tanzania, Mtambile na Pandani, kisiwani Pemba.

Prof. Ibrahim Lipumba

Waliotangazwa washindi katika majimbo hayo, ni Shamsia Mtamba (Mtwara Vijijini), Seif Salim Seif (Mtambile) na Mariam Omary (Pandani).

Hatua ya CUF kuruhusu wabunge wake hao kushiriki mikutano ya Bunge, inakinzana na msimamo wa chama hicho uliyotolewa na mwenyekiti wake, Prof. Ibrahim Lipumba, wa kutotambua matokeo ya uchaguzi huo, kwa madai kwamba kulikuwa na ukikwaji wa kanuni na sheria za uchaguzi.

Akifafanua msimamo huo, Ngulangwa amesema, licha ya chama chake, kutoyatambua matokeo hayo, hakiwezi kuwasusa wagombea wake waliotangazwa washindi.

Amesema, “…sisi hatuna msimamo mgumu kwa wale wawakilishi waliotokana na mchakato wa uchaguzi, kwa kuwa uchaguzi ni gharama. Wagombea wamekopa. Aliyepata nafasi muache akarudishe gharama zake.”

Ameongeza, “kuwazuia wagombea ubunge walioshinda kuendeleana majumu yao ni sawa na kumwadhibu mbunge husika pamoja na wapiga kura wake.

“Hatuwezi kumpa yeye adhabu, lakini hatuwezi kuadhibu wananchi waliopata chaguo lao. Wale waliochaguliwa wakatangazwa hatuwazuii kuendelea.”

Amesema, “wale ambao wamepigiwa kura na kura zao hazikuibiwa au ziliibiwa zikabaki nyingi na kutangazwa washindi, tuna sema ni washindi halali malalamiko yetu yako kwa wagombea wetu wengi ambao wameporwa ushindi wao.”

Mhandisi Ngulangwa amesema CUF kinaendelea kupambana kuhakikisha wagombea wake waliodhurumiwa kwenye uchaguzi huo wanapata haki zao.

“Tunachojali ni wale waliodhurumika, kama kuna viti kumi unatakiwa kupata ukapata kimoja haimaanishi unapaswa kukitupa. Tunaamini unashika kimoja ulichonacho wakati unapambana kupata vingine ulivyodhurumiwa,” amesema Mhandisi Ngulangwa.

Kuhusu nafasi za wabunge Viti Maalumu, Ngulangwa amesema, CUF hakitakubali kupokea viti hivyo kwa kuwa mchakato wa uchaguzi mkuu uliozaa viti hivyo, haukuwa halali.

“Viti maalum hautoki jasho unapewa, kwa kuwa hatutambui uchaguzi huu, hatutambui viti maalum sababu hakuna viti maalumu anawakilisha wananchi,” amesema Ngulangwa.

Mpaka sasa, ni ACT- Wazalendo pekee ambacho kimeweza kuwazuia wabunge wake watatu waliotangazwa washindi katika uchaguzi huo wanaoulalamikia kusheheni kasoro, ndio wameweza kuzuia kushiriki mkutano wa Bunge.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Nani anasema kuna hasara ATCL?

Spread the loveRIPOTI za makusanyo na matumizi ya fedha katika Kampuni ya...

Habari za SiasaTangulizi

CAG: Wastaafu, wenza wao chanzo NHIF kufilisika

Spread the loveRIPOTI ya ukaguzi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu...

Habari za SiasaTangulizi

Vikundi hewa 851 vyalamba bilioni 2.6 mikopo ya halmashauri

Spread the loveVIKUNDI hewa vya wajasirimali wadogo 851 kutoka katika halmashauri 19...

Habari za SiasaTangulizi

Mashirika matano yapata hasara mabilioni ya fedha

Spread the loveMASHIRIKA matano ya Serikali yanayojiendesha kibiashara, yamepata hasara ya mabilioni...

error: Content is protected !!