Thursday , 28 March 2024
Home Gazeti Habari za Siasa CUF yaeleza itakavyomtumia Lwakatare kuiangamiza Chadema
Habari za Siasa

CUF yaeleza itakavyomtumia Lwakatare kuiangamiza Chadema

Spread the love

CHAMA cha Wananchi (CUF) nchini Tanzania kimesema, kitamtumia Wilfred Lwakatare, Mbunge wa Bukoba Mjini, kuvimaliza vyama vya upinzani, hususan Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), katika Uchaguzi Mkuu Oktoba 2020. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Hayo amesema Maftah Nachuma, Makamu Mwenyekiti wa CUF Bara, leo Jumamosi tarehe 30 Mei 2020, wakati anamkaribisha Lwakatare, katika Ofisi za chama hicho, Buguruni jijini Dar es Salaam.

Lwakatare mbunge kupitia Chadema amerejea CUF, baada ya kuvuliwa uanachama wa Chadema hivi karibuni, kwa tuhuma za utovu wa nidhamu.

Chadema iliamua kumfukuza Lwakatare, baada ya mbunge huyo kukaidi maagizo  ya kutohudhuria vikao vya bunge kwa muda wa siku 14, kuanzia Mei 3 hadi 17, 2020.

Chadema ilitoa agizo hilo, ili wabunge wake wajiweke karantini, ikiwa ni tahadhari dhidi ya maambukizi ya ugonjwa wa homa kali ya mapafu, inayosababishwa na Virusi vya Corona (Covid-19).

Pamoja na Lwakatare, wengine waliovuliwa uanachama ni David Silinde (Momba), Joseph Selasini (Rombo) na Anthony Komu (Moshi Vijijini).

Hata hivyo, wabunge hao wote, wamekata rufaa ofisi ya msajili wa vyama vya siasa wakipinga uamuzi huo wa chama chao.

Katika hafla ya kumpokea Lwakatare, Nachuma amesema aliimaliza CUF katika Kanda ya Ziwa alipohamia Chadema, na kwamba chama chake kitamtumia tena Lwakatare kujiimarisha tena katika kanda hiyo.

“Alipohamia Chadema, Lwakatare alitumaliza kanda ya ziwa. Tunakuomba utakaporudi uvae njuga, kama ulivyosema unaenda kufanya mkutano mkubwa wa kuimaliza Chadema kanda ya ziwa,” amesema Nachuma.

Amesema chama hicho kimezaliwa upya, baada ya kumpokea Lwakatare, ambaye ni mwiba kwa Chama cha Mapinduzi (CCM), Chadema na ACT-Wazalendo.

“Tulipitia magumu, lakini tulihakikisha waliotaka kukiharibu wanakimbilia vichochoroni. Wadhamini walifanya kazi kubwa kuhakikisha CUF inabaki salama. Lakini leo hii CUF inazaliwa upya baada ya kumpokea Lwakatare ambaye ni mwiba wa CCM, Chadema na ACT-Wazalendo,” amesema

Nachuma ambaye pia ni mbunge wa Mtwara Mjini amesema, Lwakatare hajarudi CUF kwa ajili ya kupata cheo, bali ameamua kurudi nyumbani kutokana na mapenzi aliyokuwa nayo.

“Hakuna anayetaka vyeo hapa. Mwenyekiti yupo, viongozi wengine wapo. Cheo gani tena mtu anataka kuchukua hapa? Mpaka wakati ufike mtu anahaki ya kutaka cheo chochote. Hawa wamekuja kufuata itikadi ya vyama. Kupambana na vyama manyang’au, kuondoa CCM madaralani na Chadema kwenye majimbo yote, na ACT-Wazalendo wasipate kabisa,” amesema Nachuma.

Nachuma amesema kuwa, mkakati wa CUF kwa sasa ni kuhakikisha vyama vya upinzani vinashinda uchaguzi huo, hasa wa majimbo katika jiji la Dar es Salaam.

Awali, Mohamed Ngulangwa, Mkurugenzi wa Habari CUF, ameeleza namna chama hicho kilivyomshawishi Lwakatare, kurejea nyumbani.

Amesema, CUF kupitia Rukia Kassim, Katibu wa wabunge wa chama hicho, kiliunda kamati maalumu ya kumshawishi mwanasiasa huyo arudi nyumbani.

“Katibu wa wabunge, Rukia Kassim aliunda kamati maalumu ya watu wanne kuandaa mapokezi. Nao kwa pamoja walishirikiana kuhakikisha kila siku wanamkabili kurudi nyumbani na kuacha adha zinazomkabili alikotoka,” amesema Ngulangwa.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaKimataifa

Mwanaye rais jela miaka miaka 6 kwa dawa za kulevya

Spread the loveMwanawe rais wa zamani wa Guinea-Bissau amehukumiwa kifungo cha miaka...

Habari za SiasaTangulizi

Mapya yaibuka wamasai waliohamishwa Ngorongoro kwenda Msomera

Spread the loveMAPYA yameibuka kuhusu zoezi la Serikali kuwahamisha kwa hiari wamasai...

Habari za Siasa

Rais Samia ampongeza mpinzani aliyeshinda urais Senegal

Spread the loveRAIS wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, amempongeza mwanasiasa wa...

Habari za Siasa

Ushindi wa mpinzani Senegal wakoleza moto kwa wapinzani Tanzania

Spread the loveUSHINDI wa aliyekuwa mgombea  urais wa upinzani nchini Senegal, Bassirou...

error: Content is protected !!